METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, January 4, 2018

DC TANO MWERA AHAMASISHA WANANCHI KUCHANGIA UJENZI WA VYUMBA VYA MADARASA

Na Mwandishi Wetu, Simiyu

Mkuu wa Wilaya ya Busega Mhe Tano Mwera ahamasisha wananchi wa kata ya Lamadi kuchangia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Lukungu iliyopo ndani ya kata hiyo.

Akizungumza katika uwanja wa mkutano mjini Lamadi, Mhe Tano alisema kuwa Wilaya ya Busega inawanafunzi 1207 ambao wamekosa nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza kwa sababu ya ukosefu wa vyumba vya madarasa.

Kata ya Lamadi wanafunzi 486, Nassa wanafunzi 358 na Sogesca wanafunzi 363 , na hatuwezi kukubari wabaki nyumbani tutafanya kila linalowezekana ujenzi wa madarasa manne kila kata uwe umekamilika mpaka kufikia tarehe 15 Februari kwa ajili ya Second Selection.

Aidha, Mkuu wa Wilaya hiyo imeitaka kila kaya kuchangia elfu kumi kwa ajili ya ujenzi huo.

Vile vile ametoa rai kwa wananchi kuwa kuchangia maendeleo sio swala la hiari ni swala la lazima.

Alisema kuwa Elimu ni bure lakini jukumu la ujenzi wa miundombinu ya shule ya sekondari ni jukumu la wananchi wa kata kwa kushirikiana na serikali hivyo kila kaya ni lazima ichangie.

Pia Mhe Mwera ametoa onyo kali kwa wale wote wanaowapotosha wananchi kwa kuwaambia kutochangia kwa manufaa yao binafsi, kisiasa au kiuchumi, hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.

Aliongeza kuwa kiongozi yeyote awe wa upinzani au chama tawala akikwamisha michango hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

Alisisitiza kuwa Maendeleo hayana chama na kusema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli imejipanga kuhakikisha huduma zote za kijamii zinapatika bila tatizo lolote.

MWISHO

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com