METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, December 28, 2017

MAVUNDE AJIBU KERO ZA WANANCHI WA HOMBOLO






Mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Anthony Mavunde amefanya ziara kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa kata ya Hombolo Bwawani huku akiwahakikishia wananchi wa Mkoyo kuwa wataanza kupata huduma ya maji safi na salama kabla ya mwaka mpya kutokana na mradi huo kukamilika kwa asilimia 95.

Mavunde amefanya ziara hiyo jana ambapo ametembelea kata hiyo na kufanya mikutano ya kusikiliza kero zinazowakabili wananchi, ambapo akiwa kijiji cha Mkoyo miongoni mwa kero walizolalamikia wananchi ni utekelezaji wa mradi ya maji.

Kutokana na malalamiko hayo, Mavunde amesema mradi huo umekamilika kwa asilimia 95 lakini bado kuna mapungufu machache  ambayo mkandarasi anatakiwa kurekebisha na kuukabidhi kwa wananchi ili waweze kupata maji safi na salama kabla ya mwaka mpya.

Kwa upande wa sekta ya Elimu, Mbunge huyo ameahidi kushirikiana na wananchi katika ujenzi wa shule mbili za msingi kwenye eneo la Ngh’ole na Ndachi kutokana na watoto wa wanatembea umbali mrefu kufuata elimu.

“Hivyo kwa kuanza tunaanza na nguvu ya wananchi kwenye ujenzi wa shule ambapo kwa upande wangu nitachangia matofali 1000 na mifuko 100 ya saruji kwa ajili kuanza harakati za ujenzi wa shule hizi,”amesema

Akiwa katika mtaa wa Hombolo bwawani,Mavunde ameahidi kununua mota yenye thamani ya Tsh 4,000,000 na kuwafungia wananchi ili waanze kupata maji kwenye Mradi wa Maji wa Mtaa wa Bwawani B ambao mota yake imekufa.

Aidha katika Mradi mkubwa wa Maji wa Hombolo ambao ulihujumiwa kwa kuibiwa solar panel,Mavunde amesema wamefanikiwa kuwakamata wezi waliohujumu mradi huo  na taratibu za kipolisi zinafanywa ili vifaa hivyo virejeshwe Hombolo na wananchi waanze kupata maji.

Kadhalika, Katika sekta ya miundombinu, Mbunge Mavunde amesema anatambua changamoto ya barabara ya Ihumwa- Hombolo  na kwamba ameongea na Wakala wa barabara (Tanroad) ili kuangalia namna ya kuipandisha hadhi kupitia kikao cha bodi ya barabara ili ijengwe kwa kiwango cha lami.

Aidha Mavunde kwa upande wa sekta ya Afya amesema kiasi cha Sh.Milioni 500 kimeingia kwa ajili ya kuboresha Kituo cha Afya Hombolo ili kiwe cha kisasa na wananchi hawatalazimika tena kufuata huduma Dodoma mjini.

Mbali na hilo, amewaomba wakulima wa zabibu wajiunge katika vikundi ili kuwatafutia fursa ya uanzishwaji wa viwanda vidogo vya kukamua zabibu ili waondokane na adha ya soko la zabibu na kushuka kwa bei ya zabibu.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com