
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (aliyesimama
kulia) leo akifungua mafunzo ya wiki moja ya Waegesha ndege
yanayofanyika kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga kinachomilikiwa na Mamlaka
ya Usafiri wa Anga (CATS) kilichopo kwenye Kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (TBI).
Wakufunzi Ralf Overduya (kushoto) na
Martiyn Ouwendyki kutoka Kiwanja cha Ndege cha Hague cha Uholanzi leo
wakianza kufundisha baadhi ya waegesha ndege wa Kiwanja cha ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) katika mafunzo yanayofanyika kwenye
Chuo cha Usafiri wa Anga kinachomilikiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga
Tanzania.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Bw. Richard Mayongela (wa tatu kulia)
akiwa kwenye picha ya pamoja na washiriki, wakufunzi na waandaaji wa
mafunzo ya waegesha ndege yaliyoanza leo kwenye Chuo cha Usafiri wa Anga
jijini Dar es Salaam. Wapili kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Bw. Johannes Munanka na
wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Mfuko wa Avi Assist wa Uholanzi Bw. Tom
Kok.
WAEGESHA ndege 10 wa Kiwanja cha Ndege
cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), leo walianza mafunzo ya siku
saba ya uegeshaji ndege kutoka kwa wakufunzi wa Kiwanja cha Ndege cha
Hague cha Uholanzi yanayofanyika katika Chuo cha Usafiri wa Anga (CATS)
jijini Dar es Salaam.
Akifungua mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TAA, Bw. Richard Mayongela amesema kuwa mafunzo hayo ni muhimu
kwani yatazidi kuwajengea uwezo na uzoefu washiriki hao.
Bw. Mayongela amewasisitiza washiriki
hao kuzingatia kila wanachofundishwa ili waweze kuwa mahiri na weledi
katika uongozaji wa ndege za ndani na nje ya nchi zinazotumia kiwanja
cha ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA).
“Waongoza ndege ni moja ya kazi
inayohusisha mawasiliano ya moja kwa moja kati ya watoa huduma ndani ya
kiwanja cha ndege, hivyo ni lazima tufikie viwango vinavyotakiwa kwa
mujibu wa sheria kimataifa,” amesema Bw. Mayongela.
Hata hivyo, amesema TAA inajukumu kubwa
la kuwaongezea uwezo watumishi wake kwa kuwapeleka kwenye mafunzo
mbalimbali ili kujijengea uwezo na maarifa.Bw. Mayongela amewashukuru
waendeshaji wa mafunzo hayo yanayotolewa na mfuko wa Avi Assist wa
Uholanzi, ambapo amewahahakikishia kuendeleza ushirikiano waliouanzisha
kwa kushirikiana katika utoaji wa mafunzo ya kada mbalimbali.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Waongoza ndege
cha JNIA, Bw. Lugano Mwinuka amesema mafunzo haya yamekuja wakati
muafaka, kwa kuwa walikuwa yakiyahitaji kwa muda mrefu, na sasa
anauhakika wa washiriki wataongeza ujuzi katika utendaji wao wa kazi.
Bw. Mwinuka amesema mafunzo hayo
yanatolewa kwa nadharia na vitendo, ambapo washiriki hao wamegawanywa
katika makundi mawili ya watu watano, ambao ni Earisner Waihula,
Emmanuel Nyaulingo, Anunciatus Alex, Fadhili Meena na Oscar Kibiki.
Watakaoingia kundi la pili ni pamoja na Denis Kinyaga, Zennobius Mwimba, Raynard Komba, Said Mussa na Meshack Elisante.
0 comments:
Post a Comment