Mkulima katika Kijiji cha Buigiri, Rahel Lenjima akielezea jinsi
anavyotafuta fedha kwa kukata kuni (kama zinavyoonekana kushoto) na
kuuza ili kupata fedha za kununulia chakula.
NJE ya nyumba ya Emmy Lenjima, katika kijiji cha Buigiri wilayani
Chamwino nashuhudia kichanja kilichosheheni kuni. Bibi huyu, Emmy (70),
anaendelea kupanga hizo kuni.
Ni muda wa mchana ambao katika maeneo ya vijijini, hukosi kushuhudia
moshi unaoashiria kupika kwa ajili ya maakuli, lakini nyumbani kwa bibi
huyu, hakuna dalili za kupikwa chochote. Mmoja wa wanakaya, Thomas
Madimilo, anaweka wazi: “Kila nyumba ina njaa... Ukibahatika kupata
chakula sasa hivi (saa 6:00 mchana), utegemee tena kula kesho yake.”
Madimilo anasema siku hiyo hawakuwa na mpango wa kupika chakula licha
ya kwamba, kila mmoja ametoka kuhemea chakula. Anasema hata hizo kuni
anazopanga Emmy, siyo tu kwa matumizi ya kupikia nyumbani, bali
huzitembeza kijijini ili apate fedha za kununulia chakula. Kaya hiyo ni
sehemu ya kaya katika vjijiji vya Chamwino, Chinangali II, Buigiri na
Mwegamile, wilayani Chamwino ambavyo ukosefu wa mavuno shambani,
umewachochea kujihusisha na uvunaji misitu kwa ajili ya kupata kuni na
mkaa ambao huuza ili kupata fedha za kununulia chakula.
Upungufu wa mvua unaochangiwa na ufyekaji misitu, umesababisha mazao
kukauka na hivyo kusababisha umasikini kuongezeka. Kwa kawaida, mazao
yakivunwa, hutumika kwa chakula na ziada huuzwa ili kupata fedha kwa
ajili ya mahitaji mengine.
Lakini sasa, hali ni tofauti. Wakazi hawa ambao wanakiri kupata mlo
mmoja kwa kuhangaika kufanya vibarua, katika kutafuta fedha za kununulia
chakula, wanasema ukataji kuni umeshika kasi.
Licha ya kwamba ukataji
misitu unachangia ukame na hatimaye ukosefu wa chakula, lakini kuni na
mkaa ndiyo ‘mradi’ ulio ndani ya uwezo wa wengi kama inavyoelezwa na
Emmy. “Tunasaidiana kutafuta hela za kununua chakula.
Wanaume wanakata kuni kuchoma mkaa na kufanya vibarua, sisi
tunachanja kuni zitusaidie kupata hela.” Wakati debe moja la mahindi
linauzwa kati ya Sh 10,000 na Sh14,000, akina mama hawa huuza mzigo wa
kuni kati ya Sh 500 na Sh 1,000 kulingana na ukubwa wa mzigo.
“Nikiuza zikaisha, narudi tena porini kuchanja,” anasema Rahel
Lenjima, bibi mwingine anayekadiriwa kuwa umri wa miaka 80, mkazi wa
kijiji cha Buigiri. Anasema siku zote alikuwa akikata kuni kwa matumizi
ya nyumbani lakini baada ya kukosa chakula, imebidi aungane na wengine
kukata kuni za biashara.
Wengi wa wakazi hawa hawafahamu juu ya athari za ongezeko la ukataji
miti kwa ajili ya mkaa na kuni katika kilimo na hatimaye ustawi wa
maisha yao. Cyprian Matangula anafafanua kuwa ukataji kuni kwa ajili ya
matumizi ya nishati ya kupikia ni jambo la kawaida kwa wanakijiji.
“Lakini sasa kuna ongezeko la watu wanaokata kuni na mkaa kwa ajili
ya kuuza ili kujiingizia kipato,” anasema Matangula na kusema sababu ni
hali ya upatikanaji chakula kuwa mbaya.
Matangula anakiri kufahamu
athari za ukataji kuni na uchomaji mkaa kuwa ni shughuli zinazoharibu
mazingira hivyo kuchangia ukosefu wa mvua.
Mwongozo wa mashirika ya MJUMITA, MVIWATA, TFCG, Action Aid na TOAM
kwa wakufunzi wa mafunzo ya kilimo hifadhi ya mazingira ngazi ya vijiji,
unaelezea pia kwamba uchomaji mkaa huharibu tabaka la ozoni na kuongeza
kwa kiwango cha joto duniani.
Mashirika haya chini ya Mradi wa Mabadiliko ya Tabia nchi, Kilimo na
kupunguza umasikini (CCAP), yanaelimisha katika mwongozo wake kuwa, kwa
kawaida miti hufyonza hewa ukaa. Kwa maana hiyo, miti ikikatwa hovyo,
hewa ukaa haitafyonzwa tena, badala yake itaenda kuharibu tabaka la
ozoni lililoko angani ambalo kazi yake ni kupunguza ukali wa miale ya
jua.
Baada ya uharibifu huo kiwango cha joto duniani huongezeka kwa kiasi
kikubwa na hivyo kusababisha madhara mengi kama vile ukame na ukosefu wa
mvua. Matangula anawakilisha wanakijiji wanaofahamu madhara ya ufyekaji
miti, lakini ukosefu wa chakula na fedha unawalazimisha kufanya hivyo
na hata yeye hana la kusaidia jamii yake.
Lucy Masigati mwenye umri wa miaka 56 anaeleza namna ambavyo hutembea
takribani saa moja kutafuta kuni. Emi Chiloya, mkazi wa Buigiri
anasisitiza: “Mapori yako mbali. Tunakwenda hadi huko vijiji vya mbali
ili tupate kuni kubwa kubwa.”
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwegamile chenye kaya 404, Jeremiah Mpandula
anasema misitu ya karibu na kijijini kwao imetoweka siyo tu kwa ukataji
kuni, bali pia kutokana na kilimo na ujenzi wa nyumba. Mpandula
anasema: “Miaka ya zamani, watu walichanja kuni karibu sana.
Tena kuni zenyewe za kutumia nyumbani. Sasa hivi hata hizo za kuuza
wanazipata kwa shida kwenye vichaka vichache vilivyosalia.” Hata hivyo,
mkazi wa Kijiji cha Chamwino, Richard Julius anasema biashara hiyo ya
kuni ni ya kuganga njaa tu.
“Wala huwezi kusema watu wanapata hela nyingi za kuwafanya wapate
mahitaji yote,” anasema Julius akishauri halmashauri isaidie kutatua
tatizo la umasikini unaotokana na ukosefu wa mvua ili ufyekaji misitu
usiendelee kushika kasi kwa lengo la kuganga njaa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya
Chamwino, Rugambwa Banyikila, kiwango cha ufyekaji misitu ni asilimia
mbili. Biashara ya mkaa ndiyo inachangia zaidi ufyekaji misitu kuliko
ukataji kuni.
Kwa mujibu wa mkuu huyu wa idara, Wilaya ya Chamwino ina eneo la
misitu ya asili yenye ukubwa kilometa za mraba 1960.96 na misitu ya
hifadhi ni kilometa za mraa 63.08.
Idara hupata ruzuku ya sh 400,000 kwa mwezi kutoka serikali kuu
ambazo hutumika kuanzisha vitalu vya miche, kupanda miche, kuitunza
pamoja na kusaidia katika doria za mara kwa mara kwa ajili ya udhibiti.
Hata hivyo, Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Dodoma
Network Environment (DONET), Emmanuel James, anasema udhibiti wa
uharibifu wa misitu unapaswa uangaliwe kwa jicho la kukomesha umasikini
unaowakabili wanavijiji. “Mabadiliko ya tabianchi tunayaangalia zaidi
kwa maisha ya watu na wanyama. Maisha ya watu yamekuwa duni. Umasikini
umeongezeka.
Wanapokosa chakula, tunaangalia rasilimali nyingine kama vile misitu.
Watu wasipopata mvua ya kutosha, misitu inaangaliwa zaidi kwa ajili ya
kukata mkaa na kuni,” anasema James. Ukataji kuni na uchomaji mkaa
katika vijiji hivi vya Chamwino, ni uharibifu wa mazingira ambao DONET
inasema unahitaji mipango thabiti ya kuukabili kwa kuwapa wakulima mbinu
za kupata fedha bila kuharibu misitu.
“Unaweza kuhifadhi mazingira na bado ukapata fedha. Usipohifadhi
mazingira, utapata fedha kwa haraka na zitapotea mara moja,” Katibu Mkuu
Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Faustine Kamuzora anasema.
Ukataji miti na uchomaji mkaa unachangia umaskini kwa sababu kadri
misitu inavyotoweka, ndivyo vyanzo vya maji vinavyokauka na ndivyo mvua
zinavyozidi kuwa haba. Ofisa Mifugo Mwandamizi wa Wizara ya Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Theresia Massoy anashauri wakulima kupanda miti kando
ya mashamba yao yenye matumizi mtambuka, ikiwamo miti ili kuzalisha hewa
ya nitrojeni.
Upandaji miti siyo kwa lengo la kupata kuni na mkaa kudhibiti
ufyekaji wa misitu, bali pia kuhifadhi rutuba ya udongo na kuhifadhi
maji katika mashamba. Ripoti ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2014
inaweka bayana kuwa uharibifu wa ardhi umechangia mavuno hafifu ya
kilimo na kutokuwepo kwa uhakika wa chakula ambako ni kinyume na Malengo
Endelevu ya Maendeleo (SDGs) yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka
2015.
Malengo haya endelevu ni kutokomeza umasikini kwa kuongeza kipato cha
watu. Lengo namba mbili linajielekeza kwenye kutokomeza njaa, kuwa na
uhakika wa chakula,lishe bora na kukuza kilimo endelevu.
HABARI LEO
Wednesday, October 25, 2017
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
KARIBU TUME YA MAENDELEO YA USHIRIKA
Popular Posts
-
Kiongozi wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change (FDC) nchini Uganda Kizza Besigye amekamatwa tena na maafisa wa polisi. ...
-
Mkuu wa Wilaya ya Songwe Samuel Jeremia Opulukwa akinawa mikono kabla ya kuingia katika Zahanati ya Saza itakayotumika kutibu endapo ata...
-
MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Tanzania (DCI), Robert Boaz Mikomangwa amesema Jeshi la Polisi nchini Tanzania na vyombo vingi...
-
Naibu waziri Kilimo Mhe. Omari T. Mgumba (Mb) akiwa ofisi ya mkuu wa mkoa wa arusha alipokutana na wataalamu wa kilimo ,ushirika na ...
Powered by Blogger.
0 comments:
Post a Comment