KAYA 3899 ILEMELA ZANUFAIKA NA MPANGO WA TASAF AWAMU 3
Halmashauri ya manispaa Ilemela imefanya zoezi la uhawilishaji wa fedha za ruzuku za mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF ambapo kiasi cha shilingi 137,632,000.00 zimehawilishwa kwa kaya 3899 zilizo kwenye mpango ikihusisha mitaa 101 ya kata 18 za wilaya hiyo ikiwemo kata ya Kawekamo, Kirumba, Kitangiri, Ibungilo, Nyamanoro, Nyamhongolo, Pasiansi, Buswelu, Sangabuye, Kayenze, Mecco, Nyakato, Nyasaka, Shibula, Ilemela, Kiseke,Buzuruga na Bugogwa ukiacha kata ya Kahama ambayo haipo kwenye mpango
Akizungumza na wananchi wake wa kata ya Kawekamo Diwani wa kata hiyo Mheshimiwa Japhes Rwehumbiza amewaasa wananchi hao kuzitumia vyema fedha hizo kwa kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi itakayowasaidia kujikwamua kutoka katika lindi la umasikini ikiwa ni kutimiza lengo la Serikali la kuona fedha hizo zinawanufaisha wananchi wanyonge na masikini
''Niwaombe sana nendeni mkazitumie vizuri fedha hizi, msizitumie kwa kwenda kirabuni na kunywa pombe hapana! Kaanzisheni miradi mbalimbali itakayowatoa sehemu moja kwenda sehemu nyengine na hilo ndilo lengo la Serikali kutoa fedha hizi'' Alisisitiza
Aidha Mheshimiwa Japhes amewataka wataalamu wa maendeleo ya jamii kufatilia wananchi wote wanaonufaika na fedha za mpango wa TASAF ili kujiridhisha kama wanafanyia lengo lililokusudiwa sambamba na kutoa elimu kwa walengwa wasiokuwa na ufahamu wa kutosha juu ya kujinasua kiuchumi kwa kupitia mpango huo
Kwa upande wake mratibu wa TASAF manispaa ya Ilemela ndugu Frank Ngitaoh amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu ya matumizi bora ya fedha za ruzuku hiyo kabla ya kuendesha zoezi la uhawilishaji huku akiwaasa wananchi na viongozi kutoa ushirikiano katika kufikia malengo ya Serikali kupitia mpango huo
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
0 comments:
Post a Comment