METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, October 20, 2017

CHUMI AWAPONGEZA MAFINGA KUSHIKA NAFASI YA TANO KITAIFA MTIHANI WA DARASA LA SABA

Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kushika nafasi ya tano Kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Halmashauri ya Mji wa Mafinga ina miaka miwili toka ianzishwe na mwaka jana ilishika nafasi ya nne kitaifa katika matokeo ya mtihani wa darasa la saba.

Mbunge huyo amesema  ameupongeza Uongozi wa Halmashauri ya Mji, Waalimu, Watendaji, Waheshimiwa Madiwani, Wazazi na Wananchi kwa Ujumla.

Chumi amesema kuwa, pamoja na changamoto nyingi ikiwemo kutokuwa na gari madhubuti la Idara ya Elimu,  watendaji na waalimu waliendelea kuchapa kazi na kuifanya Mafinga kuendelea kung`ara.

`kwa hakika ninajivunia ushirikiano tulionao wana Mafinga, kuanzia watendaji, viongozi wa kuchaguliwa, waalimu, wazazi na wananchi kwa ujumla' alisema.

Aidha Mbunge huyo amewashukuru viongozi wa dini kwa kueleza kuwa mafanikio katika elimu dunia yanajengwa kwenye msingi wa malezi yenye kufuata maadili.

`Viongozi wetu wa dini, wamekuwa wakihubiri kuhusu malezi bora, lakini pia wamekuwa wakishirikiana nasi katika shughuli mbali mbali za elimu, na kila wanapopata nafasi, wamekuwa wakituasa kuwapa watoto malezi bora'

Akizungumzia mazingira ya utendaji kazi, Chumi alisema kuwa Idara ya Elimu haina gari hivyo kuwa kikwazo katika ufanisi wa kazi, hata hivyo alimshukuru Katibu Mkuu Tamisemi Injinia Musa Iyombe ambaye ameahidi kuwapatia gari la idara ya elimu.

Halmashauri ya Mji wa Mafinga ilianzishwa Julai 2015 baada ya kugawanywa kwa Halmashauri ya Wilay ya Mufindi, na sasa katika kipindi cha miaka miwili imeshika nafasi ya nne(2016) na nafasi ya tano (2017).

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com