Jalada la kitabu
cha ‘MIFUPA YA ALBINO’.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa ameshikilia Karunguyeye waliokaushwa nyumbani
kwa mganga wa jadi.
MWANDISHI wa habari mwandamizi nchini, Daniel Mbega, amekamilisha
kuandika kitabu kinachofichua siri zilizo nyuma ya pazia kuhusiana na mauaji ya
vikongwe na albino nchini Tanzania na barani Afrika kwa ujumla.
“Nimekamilisha, lakini nimekwama kidogo kuhusu fedha za uchapaji na
kama kuna taasisi yoyote au mtu anayeweza kunisaidia nitashukuru sana,” amesema
mwanahabari huyo.
“Yeyote mwenye nia njema na jamii ya Watanzania na anaguswa
kusaidia uchapaji wa kitabu hiki, ninaomba awasiliane nami kwa namba hii 0656-331974, kwani naamini kitabu hiki
kitakuwa msaada pia wa kiroho baada ya kujua mambo yanayofanywa hata na baadhi
ya viongozi wa dini wanaotumia ushirikina,” aliongeza.
Bw. Mbega amesema kwamba, katika utafiti wake huo alifanikiwa
kukutana na waganga wa jadi, wachawi na matapeli katika mikoa ya Shinyanga,
Geita, Simiyu, Mwanza, Kagera, Mara, Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa, ambako
alikaa kwa miezi miwili akifanya uchunguzi.
Aidha, amesema kwamba, katika uchunguzi wake huo alishiriki pia kikamilifu katika misako mbalimbali ya wahalifu walioshiriki kwenye matukio hayo na kushuhudia namna vyombo vya ulinzi na usalama vinavyotenda kazi.
Kunusurika kifo kwa ajali ama kuzingirwa na baadhi ya wananchi ni moja ya hatari alizokumbana nazo wakati wa uchunguzi wake, huku akisafiri umbali wa zaidi ya kilometa 40,000 katika kipindi hicho.
“Wakati mwingine nilikosa usingizi hata kwa siku tano mfululizo, nililazimika kusafiri mchana na usiku katika mazingira mengi hatarishi nikikusanya habari,” alisema.
Akaongeza: “Haikuwa kazi rahisi kuweza kufanya mahojiano na waganga wa jadi, achilia mbali wachawi ambao baadhi yao waliamua kujiweka wazi na kueleza mambo yanayotendeka katika ulimwengu wa giza na jinsi yanavyohusiana na mauaji ya wenye ualbino.”
Alisema katika uchunguzi huo alikumbana na mambo mengi ya ajabu ikiwa ni pamoja na kushika matunguli, pembe zinazofoka damu, damu na maiti, mifupa inayodhaniwa kuwa ya binadamu na mambo mengine kadha wa kadha.
Aidha, alisema kwamba, alizungumza pia na wanamichezo, baadhi ya viongozi wa dini ambao nao wanatumia nguvu za giza ambapo waganga walieleza jinsi nao wanavyoshiriki katika matukio hayo ya mauaji ya wenye ualbino.
“Ni mtandao mpana sana, siyo Tanzania tu, bali hata katika nchi jirani za Kenya, Malawi, Burundi, Msumbiji, Afrika Kusini na Swaziland… naamini kkitabu hiki kitaiamsha jamii na kubadilisha mitazamo ya watu mara watakapojifunza yale niliyoyakusanya kutoka kwa vinywa vya wahusika wenyewe,” amesema na kusisitiza kwamba amepanga kitabu hicho kiwwe mtaani mwishoni mwa mwezi Septemba ikiwa atapata msaada wa kufanikisha uchapaji.
Mganga wa jadi
akimpigia ramli mwandishi wa kitabu hiki (hayuko pichani) baada ya kutoa Shs.
2,000 akitaka amwangalizie kwanini 'mkewe' (askari mmoja wa kike aliyekwenda naye wakiwa kikazi) alikuwa hazai. Mganga alisema mwanamke huyo alikuwa 'amelogwa' na mwanamke aliyetaka kuolewa na mwandishi halafu yeye akamkataa, ambapo kiuhalisia hakuwepo mwanamke wa aina hiyo na hata huyo aliyekwenda naye walikutana kikazi na hawakuwa wakifahamiana kabisa.
Mtoto Baraka
Cosmas akiwa amelazwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mbeya baada ya kukatwa
kitanga cha mkono Machi 7, 2015.
Mwandishi Daniel Mbega (mwenye fulana nyekundu na kofia ya sweta) akiwa
sambamba na wanausalama katika nyumba ambamo Baraka Cosmas alikatwa kitanga cha
mkono Machi 7, 2015.
Mtuhumiwa Sajenti
Kalinga Malonji akiwa chini ya ulinzi baada ya kukishusha kiganja cha Baraka
Cosmas kwenye mti nyumbani kwake kijijini Hanseketwa, Mbozi siku ya Jumapili, Aprili 26, 2015. Sajenti tayari amehukumiwa miaka nane jela na wenzake wamehukumiwa vifungo vya hadi miaka 20 jela.
Mwandishi Daniel Mbega, akiwa kwa mganga huko Kachwamba, wilayani Chato
wakati akifanya uchunguzi wa mauaji ya albino.
0 comments:
Post a Comment