METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, August 6, 2017

Arusha, Mwanza wakamilisha ramani

 Na Halima Mlacha

SERIKALI iko katika mchakato wa kumalizia ramani za mipango miji yote nchini, huku baadhi ya miji, ikiwemo Mwanza, Arusha, Mtwara, Singida na Iringa ramani zake zikiwa zimekamilika.

Pamoja na hayo, pia imeanza mkakati wa kupiga picha za anga katika wilaya zote nchini na tayari wameanza na Jiji la Dar es Salaam, na picha hizo zitatumika kwa ajili ya kupanga miji na kutengeneza ramani ya msingi inayoonyesha hali halisi ya nchi.

Hayo yalibainishwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Moses Kusiluka, katika mahojiano maalum aliyoyafanya na magazeti ya serikali Daily News na HabariLeo.

Alisema serikali ililazimika kuandaa ramani mpya za mipango miji baada ya ramani nyingi zilizopo kupitwa na wakati na hali ya majiji mengi kutopangika ipasavyo. Alisema katika mchakato huo, alitaja miji ambayo bado ramani zake ziko katika hatua ya mwisho kuwa ni pamoja na jiji la Dar es Salaam na Dodoma, ambayo ililazimika ramani zake kuboreshwa zaidi kutokana na mkoa huo kuwa makao makuu ya serikali.

“Master Plan nyingi kwa ukweli zimekamilika, zipo chache zinaendelea katika hatua ya mwisho na zikikamilika, tunatarajia kufanya uzinduzi wa ramani hizo ndani ya miezi miwili au mitatu ijayo, na kupitia picha hizi sasa ramani zote na matumizi ya ardhi zitaandaliwa kieletroniki,” alisisitiza.

Akizungumzia picha za anga, alisema picha hizo ni muhimu kwa maendeleo ya Tanzania kwani pamoja na kutumika katika mipango ya matumizi ya ardhi, pia zitatumika kwa ajili ya kupanga miundombinu, majanga na mipango miji. Kwa upande wa upimaji viwanja, Dk Kasiluka alisema wizara hiyo ina mpango wa kuhakikisha maeneo yote nchini yanapimwa na wamiliki wa ardhi kupatiwa hati au hati za kimila.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com