METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, July 29, 2017

SHAKA AACHA GUMZO SENGEREMA AAGIZA UCHAGUZI UVCCM WAHENGA WAONDOLEWE

Na Mwandishi  Wetu, Mwanza

Hatimaye kata kumi  katika wilaya Sengerema Mkoani hapa zitarudia uchaguzi wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) baada ya kuthibitika kulikuwa na ukiukaji taratibu na kanuni za uchaguzi huku  baadhi ya wagombea kudanganya umri.

Hatua hiyo inafuata agizo lililotolewa juzi  na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka katika mkutano wake wa ndani uliofanyika katika ukumbi wa chuo cha Maendeleo Sengerema mjini akiwa ziarani  Mkoani Mwanza kwa siku sita ambapo alisema    ana taarifa za chaguzi hizo kuzongwa na hadaa katika wilaya hiyo.

Shaka alibainisha kuwa amepata taarifa yakinifu kuwa wapo wagombea waliowania nafasi mbali mbali katika kata  hizo hawakuwa na uhalali wala sifa ya kupitishwa ndani ya jumuiya  huku baadhi yao wakidanganya na kutowasilisha viambatanisho vyao kulingana na maelezo binafsi ya kila mgombea. 

Alisema chaguzi za jumuiya na chama zinapaswa kuheshimiwa kwa kadri maelekezo  yaliyotolewa na  ngazi husika na kutakiwa kila mtendaji anayesimamia uchaguzi kufuata kanuni,  taratibu bila kuzikiuka.

"Sikuja Mwanza kwa bahati mbaya, nina taarifa za kina na sahihi kuna matatizo katika uchaguzi zetu , kuna taratibu na matakwa ya kikanuni  yamekiukwa, wahenga wamedandia,  katibu wa ccm wewe ndiye mlezi wa jumuiya upo apa, nakuagiza katibu vijana wilaya nataka majibu ndani ya siku mbili kwanini kanuni imekiukwa sambamba na kutaka mchukue hatua kwa wahusika wote wa   kadhia hii  "Alisema Shaka  

Katibu wa CCM wilaya ya Sengerema Idd Shaaban Mkowa amekiri na kueleza  kuwa chaguzi hizo zitarudiwa tena upya na uteuzi wa awali umetenguliwa .

Mkowa alisema ni kweli Kaimu Katibu mkuu wa UVCCM katika hotuba yake akiwa wilayani sengerema alitaja kuwepo kwa ukiukaji kanuni na   taratibu hivyo baada ya kufuatilia imebainika kuchomoza kwa dosari kadhaa kinyume na taratibu za uchaguzi. 

"Tayari tumetangaza na kuwataka wanajumuiya wenye nia kuwania uongozi kwenye nafasi zilizothibitika kufanyika udanganyifu, waende  kuchukua fomu, wajaze na kuzirudisha ili hatua nyengine za uchujaji ziendelee "Alisema Mkowa .

Katibu huyo wa ccm wilaya alisema wanaofikiri wanaweza kukidanganya chama au jumuiya zake ili washike uongozi kwa njia za hadaa , hawataweza kwasababu chama kimekusudia kusimamia mageuzi ya kweli, kurudisha nidhamu , heshima na mipaka ya demokrasia 

Alizitaja Kata zinazorudiwa uchaguzi kuwa ni Kalebezo, Nyehunge, Nyakarilo, Kasenyi na Ibondo,  nyengine ni  Maisome, Nyamatongo, Chifunfu, Ngoma na Bukokwa 

Katibu UVCCM  wilaya hiyo  Adam Itambu alipoulizwa kuhusiana na kuharibika kwa chaguzi hizo alisema kulifanyika udanganyifu wa kifundi na isingewezekana haraka ngazi ya wilaya kubaini bila ngazi za juu kuwapekua wagombea hao na kuwabaini.

Itambu alisema marudio ya chaguzi hizo za  jumuiya hiyo  kwenye kata kumi wilayani kwake zinathibitisha  jinsi UVCCM  inavyofuatilia mambo na kuwa makini chini ya utendaji wa Kaimu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka. 

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com