Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Christopher Chiza
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Christopher Chiza
KAIMU Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Edwin Rutageruka amewakaribisha Watanzania kuhudhuria maonesho ya kimataifa ya biashara, maarufu Sabasaba, ili wakajionee mabadiliko yaliyopo, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kujiimarisha kiushindani.
Alisema hayo jana katika semina ya siku moja kwa washiriki wa maonesho hayo, iliyofanyika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana. Alisisitiza kuwa maonesho hayo ya 41 yatakuwa tofauti na miaka iliyopita.
“Sasa hivi kuna ushindani mkubwa katika maonesho ya biashara, tumeamua kujipanga na yapo mambo mengi tuliyofanyia marekebisho. Kuanzia vitambulisho vya washiriki ambapo mfumo unaotumika ni wa kielektroniki hadi utaratibu wa watazamaji kuingia kwenye maonesho hakutakuwa na foleni ndefu na hata ukataji tiketi utakuwa wa haraka,” alisema Rutageruka.
Aliongeza, “Tutakuwa na mikutano ya mara kwa mara kati ya wafanyabiashara ambao watabadilishana uzoefu na kupeana kazi, mshiriki atakayefanikiwa kumshawishi mwenzake hadi akapata mkataba wa kufanya naye biashara makubaliano hayo tutayasaini mbele ya mgeni rasmi siku ya kufunga maonesho ili ulimwengu mzima uone.”
Vilevile miongoni mwa maboresho ya maonesho ya mwaka huu ni kuwepo siku ya Afrika Mashariki, ambapo washiriki kutoka nchi wanachama watakutana na kubadilishana uzoefu juu ya uzalishaji bidhaa na biashara.
Vilevile, kutakuwa na siku ya kuonja asali, ambapo washiriki wanaofanya biashara ya asali, watawaonjesha wateja wao. Awali, akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TanTrade, Christopher Chiza alisema: “Ipo haja kuwepo na mwendelezo wa maonesho ya biashara na yasiwe wakati wa msimu tu kama hivi. Haya mabanda hayatakiwi kubaki matupu tuyatumie.”
Chiza pia aligusia umuhimu wa Tan- Trade, kutanua wigo wa maonesho katika ngazi ya kanda na maeneo ya kimkakati kama mikoa ya pembezoni mwa nchi ili kufikia mataifa jirani na wafanyabiashara wasioweza kufika Dar es Salaam.
“Takwimu zinaonesha viwanda vipo 49,243 lakini viwanda vidogo ni asilimia 85.13, asilimia 0.5 ni viwanda vikubwa na asilimia zilizobaki ni za viwanda vya kati na vidogo. Na wajasiriamali wanaotokana na viwanda vidogo wapo zaidi ya milioni 3.1.
“Hii inadhihirisha kuwa asilimia kubwa ya washiriki wa maonesho haya hawafiki au hawapo Dar es Salaam, tutafute namna ya kuwafikia huko huko walipo kwa kuanzisha maonyesho ya kikanda na maeneo ya kimkakati ikiwemo Dodoma, ambako ni rahisi kufikika, Mwanza, Kigoma na Kagera na Mbeya ambako kote huko tutagusa nchi jirani,” alisema Chiza
0 comments:
Post a Comment