Na Nasri Bakari, Dar es salaam
Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe. Kisare Makori Leo Jumanne, Mei 23, 2017 ameiagiza ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo kuanza mchakato wa ujenzi wa soko la Sinza A lililopo katika Kata ya Sinza jijini Dar es Salaam.
Agizo hilo amelitoa wakati akizungumza na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao sokoni hapo alipozuru katika eneo hilo kwa dhamira ya kujionea hali halisi ya soko.
Mhe Kisare ametaja umuhimu wa soko Hilo kwa wafanyabiashara na wananchi kuwa kwa wafanyabiashara wanajipatia ujira wao huku wananchi wakipata urahisi wa huduma Bora kwa gharama nafuu.
Sambamba na hayo pia Mkuu wa Wilaya aliagiza wafanyabiashara kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi katika kufanya shughuli zao huku akiwasisitiza kulipa Kodi kwa mujibu wa taratibu za nchi.
"Kuna wafanyabiashara wanafanya shughuli zao bila kufuata utaratibu hao naahidi nitakula nao sahani moja, pia nawasisitiza mlipe kodi kwani itasaidia kufanya mambo mengine ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa soko hili" alisema Mhe. Makori.
Pia Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwafungia maduka yao wale wote watakaoenda kinyume na kanuni pamoja na taratibu ikiwemo kutolipa kodi.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa soko hilo Mwenyekiti wa soko Ndg Salum Hassan alimuomba Mkuu wa Wilaya kufika mara kwa mara katika soko hill ili kujionea hali halisi iliyopo na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.
Hata hivyo Mhe Makori ameahidi kurudi Katina eneo hilo ili kujionea utekelezaji wa maagizo yote aliyoyatoa.
Imetolewa Na;
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo
0 comments:
Post a Comment