Na Mathias Canal, Iringa
Kuboresha Kilimo kwa wakulima nchini Tanzania kutoka kilimo cha chakula pekee katika familia mbalimbali mpaka kufikia kilimo cha biashara ni njia mojawapo ya kujenga mazingira wezeshi ya kujitoa katika wimbi la umasikini nchini.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Mheshimiwa Richard Kasesela wakati akifunga warsha ya siku tatu iliyofanyika katika ukumbi wa Hazina Mjini Iringa ya kuwajengea wadau uelewa wa pamoja kuhusu programu ya kuendeleza sekta ya kilimo Awamu ya pili nchini Agricultural sector Development Programme (ASDP 2), Programu inayotarajiwa kutekelezwa katika kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2017/2018 hadi 2027/2028.
Dc Kasesela alisema kuwa Programu hiyo ya ASDP 2 iliandaliwa baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya ASDP 1 iliyotekelezwa kuanzia mwaka 2006/2007 hadi 2013/2014 huku akiwapongeza waandaaji wa warsha hiyo ambao ni OFISI ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na kutaraji kutekelezwa na wadau mbalimbali kama vile Wizara za sekta ya kilimo, Wahisani, Sekta binafsi, Taasisi zisizo za kiserikali, Wakulima Wafugaji, na Wavuvi.
Dc Kasesela alisema kuwa wataalamu wa kilimo wanapaswa kutumia ujuzi wao kuwafundisha wananchi mbinu za kisasa za kilimo ikiwemo kutumia teknolojia katika kukuza kilimo hususani kilimo cha umwagiliaji kwani nchini Tanzania kuna maji mengi ambayo hayatumiki ipasavyo.
Hata hivyo alisema kuwa Mkoa wa Pwani na Dar es salaam pekee endapo wataalamu wake wakiamua kujikita katika kilimo kuna uwezekana mkubwa wa kuzalisha mpunga na mazao mbalimbali ikiwemo mbogamboga na matunda kutokana na ardhi ya rutuba iliyopo sambamba na maji mengi.
Dc Kasesela amesema kuwa Utekelezaji wa ASDP 2 utazingatia malengo ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano (2016-2021), Mkakati wa Taifa wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na Dira ya maendeleo ya Tanzania (2025).
Aidha amewasihi wataalamu hao sambamba na wananchi kwa ujumla kutumia fursa ya kulima kwani kilimo ni mkombozi pekee na wa haraka katika kujikwamua na umasikini endapo zitatumika mbinu bora za kilimo.
Sambamba na hayo pia alisema kuwa hakuna mwisho wa kujifunza hivyo kupitia mafunzo hayo watumie ujuzi walioupata sambamba na kuendelea kujifunza zaidi ili kuwa na maarifa mengi yenye tija na manufaa kwa wakulima wa Mikoa ya Dar es salaam na Pwani na Taifa kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment