METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 11, 2017

HAPA KAZI TU, NI FALSAFA NA KAULI MBIU YA RAIS AU SOTE TUNAHUSIKA?

Image result for magufuli

Nimekumbuka 2015 mara baada ya uchaguzi mkuu na siku za mwanzo za uongozi wa Mheshimiwa Rais John Magufuli mara baada ya kuingia madarakani na kuunda timu ya askari wake wa mwamvuli. Kila askari wa mwamvuli mara kwa mara alijinasibisha na kauli mbiu ya mkuu wa nchi ya hapa kazi tu. Ninavyoelewa mimi, kauli mbiu hii ilijinasibisha kwa kumtaka kila mtu afanye kazi.

Kumbukumbu zaonesha katika ya wapiga kura waliojiandikisha mwaka 2015 katika daftari la kudumu la wapiga kura la Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ni watu takribani 23,254,485.

Kwa kuchukulia dhana ya wapiga kura ni watu wazima wenye miaka 18 na zaidi kwa mujibu wa sheria, maana yake wengi wao wana nguvu ya kufanya kazi na kuweza kuzalisha mali kama msingi wa utu na uwajibikaji. Aidha kufanya kazi ni wajibu wa mwanadamu aliopewa na Muumba wa Mbingu na Nchi kwa agizo, asiefanya kazi na asile.

Nikitathmini kuwa zaidi ya asilimia 70 wanajihusisha na kilimo, ufugaji na uvuvi sawia na kumbukumbu toka vyanzo mbalimbali, ina maana wakazi wa nchi hii wapatao milioni 16 wanajihusisha na shughuli za kilimo.

Aidha kwa mujibu wa taarifa ya hivi karibuni kutoka kwa katibu wa mashirika ya hifadhi ya jamii Ndugu Meshack Bandawe ni kuwa kuna miradi ipatayo 25 ya uwekezaji katika viwanda. Baadhi ya viwanda vitajishughulisha na kusindika nafaka kama vile national milling. Vingine vitahusika na kuchakata ngozi, viwanda vya sukari na shughuli zingine chungu mzima.

Kwa jicho la kudadisi na kujenga dhana ni kuwa iwapo watu walau nusu ya milioni 16 ambayo ni asilimia 70 ya waliojiandikisha kupiga kura, itajihusisha na kilimo endelevu na kuingia katika mifumo rasmi ya kilimo kama ajira rasmi, ina maana watu milioni 8 wanaweza kuwa kwenye kiwango cha kuchangia mifuko ya hifadhi ya jamii.

Kwa ufugaji wa kisasa wenye tija na kilimo cha umwagiliaji kwa mifumo endelevu, iwapo kila mkulima ataamua kujilipa shilingi milioni moja tu kwa mwezi na kiasi hicho cha fedha kikangia katika mifumo rasmi ya kulipa kodi na kuchangia katika mifuko ya hifadhi ya jamii na bima ya afya; tafsiri yake ni kuwa kwa uchache kodi ya mapato (PAYE) ingekuwa walau Trilioni 17 kwa mwaka. Na makusanyo ya mifuko ya pension ingekuwa walau trilioni 9.6 kwa mwaka.

Kwa dhana hiyo hiyo kuwa mkulima huyu atamudu huduma za kijamii kama vile kununua umeme, maji, vifaa vya kujengea makazi bora, kwa kila manunuzi anayofanya na akadai stakabadhi ya malipo, basi kuna fedha nyingi sana zingekuwa kwenye mzunguko na wafanya biashara wangeweza kuuza bidhaa na huduma kwa jamii ya watanzania wengi wakiwemo wakulima.

Kwa msingi huo huo, wa makusanyo ya kodi na fedha za mifuko ya hifadhi ya jamii, ina maana kuna ajira zingetokea TRA kama idara maalumu inayoshughulika na wakulima. Kwa upande wa pili naona kukua kwa mifuko ya hifadhi ya jamii kwa kuongeza ajira. Huenda ikaunwa Tanzania Farmers Pension Fund (TFPF) kama mfuko maalum kufanyia kazi mafao ya wakulima. Mabenki nayo kwa upande wake yatakuwa na uhakika wa kukopesha wakulima ambao wataweza kujenga au kununua nyumba na kuwa na makazi bora. Mzunguko wa wakulima milioni 8 kupita mfumo rasmi ya kibenki itakuwa na athari kwa shughuli zingine za kiuchumi (micro-enterprise activities) chungu mzima.

Nina imani na Tanzania ya viwanda inawezekana iwapo tuna wakulima wanaojua uhitaji wa kiwango malighafi za viwanada kama vile alizeti, ufuta, pamba, mahindi na mengineyo mengi. Wanajua mbegu bora, mbolea bora na wana mitambo maalum ya kupandia na kuvunia.

Kwa upande wa wafugaji wanahitaji kufahamu dhana ya kuwa na breed bora ya mifugo inayoweza kuwekwa katika eneo dogo na kuzalisha chakula cha mifugo pasipo “kuwaswaga” toka pande moja ya nchi kwenda pande nyingine ya nchi. Tukumbuke makundi makubwa ya mifugo kwa upande mwingine inaleta athari za mazingira na migogoro na wakulima pale mifungo inapokuwa mingi na mfugaji akashindwa kuidhititi inapotokea imetoroka kuingia kula miwa, mtama, mahindi au mazao yoyote yale ya kilimo.

Rai yangu kwa Rais maana wewe, ndiwe ulipewa dhamana na Watanzania, hali kadhalika wasaidizi wako kama vile waziri wa kilimo, waziri wa habari, waziri wa elimu, waziri wa fedha na mipango, waziri wa viwanda na wadau mbalimbali. Tuna wajibu kuwaelimisha na kuwawezesha wakulima na wafugaji kiufahamu kwanza na ki-miundombinu ikiwemo kuweza kumudu vifaa vya kilimo cha umwagiliaji.

Nachagiza kielimu ili kukuza ufahamu na kuleta mabadiliko ya kimtazamo. Wakulima wapate kimitambo/miundombinu. Kwani ni duniani hapa hapa kuna wanadamu waliozaliwa na mwanamke wanazalisha tani laki 3 za nyanya kwa hekta kwa mwaka na kuuza uarabuni ambako ni jangwani na wana utajiri wa mafuta. Bila shaka hata sisi tukiamua kuwekeza tunaweza kuonesha tofauti. Mkulima wa kitanzania japo akipata walau nusu ya mavuno kwenye hekta 1, maana yake anapata walau tani 150 ambazo ni sawa na wastani zaidi ya milioni 100 kwa mwaka. Kipimo cha hekta moja ni kidogo sana, kwani sera ya umwagiliaji ya Taifa ya mwaka 2009 inatambua (…Small Scale Irrigation Schemes: are the schemes with area of up to 500 ha; Medium Scale Irrigation Schemes are schemes having area between 500 ha and 2000 ha)… Kwa lugha nyingine bado tuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi katika sekta ya kilimo kwa kuwa ardhi ipo na mkulima mdogo anaeweza kufanya kilimo kwa hekta 500 akiwekeza vizuri, maana yake wakulima watakuwa na mchango mkubwa sana kwenye uchumi wetu.

Ni dunia hii, hii kuna ng’ombe mmoja anatoa maziwa lita 11,000 kwa mwaka. Si haba, mkulima wetu akipata walau nusu ya maziwa ambazo ni lita 5,500 kwa mwaka. Tafsiri yangu, mfugaji mmoja akiwa na walau ng’ombe watatu wanaotoa lita 16,500 kwa mwaka; maana yake ni kuwa mkulima huyu ana uhakika wa kuvuna walau milion 165 kwa mwaka kama atauza lita moja kwa sh. 1000. Kama wafugaji wakiwa wameungana na kumiliki kiwanda cha maziwa, tafsiri yake ni kuwa “multiplication effect” ya usindikiji una tija kubwa ukilinganisha na kuuza maziwa kama mali ghafi.

Mheshimiwa Rais na wasaidizi wako kutoka sekta mbalimbali, tuna imani nanyi kutuvusha kutoka hapa tulipo kwenda hatua ya mbele zaidi. Inawezekana tukakimbia kwa haraka sana pale ambapo umma (public) unajenga na utaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki ili sekta binafsi (private sector) ukue kwa haraka na kutekeleza wajibu wake wa kuzalisha na kulipa kodi kutokana na uzalishaji wa mazao ya shamba ambayo ni malighafi viwandani.

Uzalendo wetu tuupime kwa kukubalina kwa nia moja kuijenga Tanzania yetu. Hakuna “mjomba” kutoka ughaibuni ataijenga Tanzania mbali na sisi wenye Tanzania. Kwenye kuijenga nchi tuna wajibu kwa kukumbuka kila mara tunatakiwa kuwa na nia moja na jitihada za pamoja kama za wale watu wa kale walioamua kujenga babeli.

Tanzania ya viwanda inawezekana kabisa iwapo wakulima watasaidika kuhama kutoa kilimo cha kujikimu kwenda kulima kibiashara. Kazi tu, itakuwa falsafa ya faida kwa kila mmoja sawia na lengo la 5 ya dira ya taifa 2025. Kujenga uchumi wenye ushindani unaomfaidisha kila mmoja.

Kama vile babeli ilivyojengwa kwa nia moja na jitihada ya pamoja, hali kadhalika Tanzania tunayoitaka iwe yenye “asali na maziwa” sote tunaweza kuwa sehemu ya kuifanya itokee pasipo kumsahau mkulima kama mmoja wa wachezaji kupitia uzalishaji endelevu wenye miundombinu wezeshi, mbegu bora na pembejeo zingine ili kupata malighafi za viwanda.

Kwa pamoja tunaweza kuonesha uzalendo wetu na utaifa wetu kwa kuwa na jitihada pamoja kuijenga Tanzania yetu.

Fredrick Matuja
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com