Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo (Aliyesimama) Boniface Jacob akisisitiza jambo wakati wa kikao cha kazi na Wenyeviti wa Manispaa hiyo, Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo na kulia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo Ramadhan Kwangaya
Wenyeviti wakisikiliza kwa makini maelekezo mbalimbali wakati wa kikao cha kazi kilichoendeshwa na Mwenyekiti wa kikao hicho Mhe Boniface Jacob ambaye ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo (Picha zote na Nassir Bakari)
Pichani ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo wakati wa kikao
kutoka kushoto ni Naibu Meya wa Manispaa ya Ubungo Ramadhan Kwangaya Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo na Afisa Utumishi wa manispaa ya Ubungo Ndg Ally Juma akishauri jambo wakati wa kikao cha kazi na Wenyeviti wa Manispaa hiyo
Usikivu ni jambo la busara kikaoni
Mstahiki
Meya wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob akizungumza wakati wa kikao cha kazi na Wenyeviti wa Manispaa ya Ubungo.Na Mathias Canal, Dar es salaam
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo amewataka wenyeviti wa Mitaa iliyopo katika Manispaa hiyo kutumia vyema nafasi zao za uongozi kwa kuwatumikia wananchi kwa haki huku akiwasihi kuishauri serikali katika majukumu yake ili kuwa na maendeleo chanya katika maeneo yao sawia na kupunguza lawama za mambo yaliyopita ili kuwa na Manispaa imara yenye ukusanyaji mzuri wa mapato.
MD Kayombo amewasihi wenyeviti hao kuwa na mahusiano mazuri baina yao na maafisa watendaji wa Mitaa kwani kufanya kazi kwa Ushirikiano na Upendo ndio silaha pekee ya kuimarisha utendaji na ufanisi wa ukusanyaji wa mapato katika Mitaa.
MD Kayombo ameyasema hayo Wakati wa kikao cha kazi pamoja na wenyeviti wa Mitaa kilichokuwa na dhamira ya kushauriana namna bora ya kuimarisha mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ili kuwa na uchumi imara, kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa hiyo Mtaa wa Kibamba CCM na kuhudhuriwa pia na Wakuu wa Idara na Vitengo.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa atazuru kata hadi Kata ili kubaini wapi kumwepwaya na kipi kipaombele katika maeneo husika ili kuanza nayo katika kuimarisha maendeleo ya wananchi.
Hata hivyo wenyeviti wote wamekabidhiwa Bendera, Rejista, Vitini vyenye miongozo ya kisheria sambamba na vitini vinavyobainisha majukumu ya Wenyeviti wa Serikali za Mitaa ili kutoingiliana katika utendaji na viongozi wengine wakiwemo watendaji wa Mitaa na Kata.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ubungo Boniface Jacob ambaye pia ndiye alikuwa mwenyekiti wa kikao hicho amesema kuwa wenyeviti wanapaswa kuwasimamia vyema wananchi kulipa kodi kwani hiyo ndiyo njia pekee ya Manispaa kujisimamia yenyewe na kujiendesha kirahisi.
Mstahiki Meya ametumia Kikao hicho kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa hiyo Ndg John Lipesi Kayombo kwa uongozi wake imara na uliothubutu kwani umewafanya wananchi katika Manispaa hiyo kuwa walipaji wazuri wa kodi.
Jacob amesema kuwa mipango ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo ni kuifanya Manispaa hiyo kuwa ya mfano na kuzishinda Manispaa zingine katika Jiji la Dar es salaam.
Kuhusu Posho za wenyeviti wa Mitaa, Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo amewasihi wenyeviti kuwa na subira kwani wanaandaa mpango imara kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo ili kuwalipa malimbikizo ya posho zao zote wanazodai.
Pia amewasihi wenyeviti hao kutumia Uhuru wao kikatiba kuwafungulia kesi wale wote wanaowaonea, kuwazalilisha na kuwakejeli kwa kuwafungulia kesi katika mahakama kwa mujibu wa sheria.
0 comments:
Post a Comment