Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akijibu
hoja za wabunge mbalimbali waliochangia wakati wa kujadili Taarifa ya
Kamati ya Kudumu ya Ukimwi Bungeni Dodoma
Na mwandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama
amesema kuwa mapambano ya kukabiliana na tatizo la Dawa za Kulevya
ni jukumu la kila mwananchi na wala sio suala la kuiachia Serikali peke
yake.
Ameyasema hayo bungeni jana wakati
akijibu hoja za wabunge waliochangia juu ya Taarifa ya Kamati ya Kudumu
ya UKIMWI na Dawa za Kulevya iliyoibua maswali kwa Serikali kuendelea
kupambana na wanaoshiriki katika biashara haramu ya dawa za kulevya
nchini.
Waziri Mhagama alieleza kuwa dhamira ya
Serikali ni kuhakikisha jamii yote kwa ujumla inakuwa mstari wa mbele
katika kutokomeza tatizo hili linalowaathiri vijana kwa kiasi kikubwa.
“Mapambano haya ni yetu sote, yasichague
mtu na iwe agenda ya Kitaifa inayowahusu Watanzania wote na ikumbukwe
kuwa tatizo la dawa za kulevya lina historia tangu mwaka 1990 na
Serikali imekuwa ikipambana kwa jitihada nyingi hivyo niombe watanzania
wote tuunge mkono vita hii ili kumaliza kabisa tatizo hili”. Alisema
Waziri
Aliongezea kuwa, dhamira hii ya Serikali
ilianza kuonekana tangu kuwepo kwa sheria namba 9 ya mwaka 1995 hadi
ilipofanyiwa marekebisho mwaka 2014 na kubaini kuwa asilimia 56 ya nguvu
kazi ya vijana ndiyo imeathiriwa na tatizo la dawa za kulevya.
Aidha pamoja na mapambano hayo, tayari
sheria namba 5 ya mwaka 2015 na miundo ya mapambano inaelekeza namna ya
kupambana na vita dhidi ya dawa za kulevya.
Kwa upande wake Waziri wa Katiba na
Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe alieleza Bunge kuwa ziwepo jitihada za
makusudi za kuunga mkono mapambano haya yawe ya Watanzania wote kwa
kutoa wito kwa jamii kutoa ushirikiano na kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam Mhe.Paul Makonda kwa namna alivyojidhatiti kupambana na wote
wanaoshiriki katika biashara hizi za dawa ya kulevya.
“Nieleza wazi kuwa jitihada za Serikali pekee hazitoshi ni lazima jamii iunge mkono kwa kuwafichua wanaojihusisha na mtandao huu wa Dawa za Kulevya na Mhe.Paul Makonda nampongeza kwa kuthubutu kuingia kikamilifu katika vita hii”.Alisema Mwakyembe
Alimalizia kwa kueleza kuwa, kinachohitajika ni dhamira ya dhati na si fedha, hivyo Serikali imedhamiria kukomesha kabisa tatizo hili nchini.
0 comments:
Post a Comment