WAZIRI
MKUU Kassm Majaliwa amesema wakati umefika wa kuwa na watumishi wenye
weledi wa kutosha kwenye Halmashauri zote nchini na pia hazitakiwi kuwa
pango la wezi, wazembe au jalala la kutupa wabadhilifu walioshindikana
kwingineko.
Aidha,
Waziri Mkuu amesemma Serikali za Mitaa na Halmashauri zote nchini
zinatakiwa zianze kujitathmini na kujipanga vizuri zaidi kuona ni kwa
namna gani zitakuwa chachu ya maendeleo ya viwanda vinavyotarajiwa.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumatatu, Januari 30, 2017) wakati
akifungua Kikao cha Baraza la Mashauriano (RCC) mkoani Dodoma. Amesema
kikao ni chombo muhimu na endapo kitatumika vizuri kitaweza kusaidia
kusukuma maendeleo ya Mkoa na kupunguza migogoro kwenye Halmashauri.
Amesema
Serikali itaendelea kuongeza kiwango cha ruzuku kwa Halmashauri zote
nchini kwa kadiri uwezo utakavyoruhusu na kusisitiza kwamba fedha hizo
lazima zisimamiwe vizuri na zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo
inayowagusa wananchi.
“Endapo
itabainika kwamba kuna baadhi ya Sheria zinazokwamisha utendaji katika
Mamlaka za Serikali za Mitaa, hatutasita kuzifanyia mapitio na hatimaye
kuzibadili ili ziendane na azma yetu ya kutoa huduma bora kwa wananchi,”
amesema.
Amesema
Serikali ina maslahi makubwa kwa Serikali za Mitaa, sio tu kwa kuwa ni
Serikali kamili katika ngazi hiyo, bali pia kutokana na ukweli kwamba
kero nyingi za wananchi ziko katika ngazi hiyo.
Waziri
Mkuu amesema vyanzo vingi vya mapato ya Serikali vinapatikana kwenye
Halmashauri huku changamoto kubwa ikiwa ni kulegalega kwa Halmashauri
nyingi katika ukusanyaji wa mapato ya kodi na yasiyo ya kodi jambo
linalozorotesha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Hivyo
Waziri Mkuu ametoa rai kwa Halmashauri hizo kuendelea kuboresha huduma
kwa wananchi na kutatua kero zao kikamilifu na kwa wakati pamoja na
kubuni vyanzo vipya vya mapato na kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato.
Pia
zihakikishe malipo yote yanafanyika kwa njia za kielektoniki na
zihamasishe vijana na akina mama wajiunge kwenye vikundi vya uzalishaji
mali na kuwapatia stadi za kazi na mikopo yenye masharti nafuu ili
waweze kuwa chanzo cha mapato hapo baadaye.
Amesema
watendaji wa Halmashauri wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya rushwa
na ubadhilifu wa mali za umma na uzembe kazini na watakaobainika kufanya
vitendo hivyo wachukuliwe hatua kali za kisheria na kinidhamu.
“Someni
taarifa ya CAG (Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali) na
kutoa majibu ya kina ya namna mtakavyodhibiti mianya ya rushwa na
ubadhilifu kama ilivyoainishwa kwenye ripoti hizo,” amesema.
Hata
hivyo amesema kila Halmashauri iandae mpango wa utekelezaji wa Ilani ya
CCM kwenye maeneo makubwa ya kipaumbele kama vile ujenzi wa miundombinu
ya shule, maboresho kwenye sekta ya afya (ujenzi wa hospitali,
zahanati na vituo vya afya).
“Endeleeni
kuwa na mahusiano mazuri miongoni mwenu, mfanye kazi kwa kuzingatia
sheria, kanuni na taratibu. Kila mmoja kwa nafasi aliyonayo atimize
wajibu wake na kuzingatia mipaka ya nafasi yake. Punguzeni migogoro,
matusi, dharau, bezo na vitisho. Mshirikiane na jamii ione mpo wamoja,”
amesema.
0 comments:
Post a Comment