Wizara za
mambo ya ndani ya Ujerumani inataka kuwazuwiya wahamiaji kutofika
kabisa katika mwambao wa Ulaya ulioko katika bahari ya Mediterenia kwa
kuwachukuwa baharini na kuwarudisha Afrika.
Kwa kile
kitakachokuwa mabadiliko makubwa kwa nchi hiyo yenye sera za ukarimu
mkubwa wa kuomba hifadhi wizara hiyo imesema Umoja wa Ulaya unapaswa
kuwa na sera kama ile ya Australia ambapo kwayo wahamiaji wanaodukizwa
baharini wanapelekwa katika makambi yalioko katika nchi nyengine
kushughulikia mchakato wao wa kuomba hifadhi.
Gazeti la
Ujerumani la "Welt am Sonntag" limeripoti Jumapili (06.11.2016
)likimkariri msemaji wa wizara hiyo akisema kufuta uwezekano wa kufika
Ulaya kunaweza kukawashawishi wahamiaji kuepuka kufunga safari zenye
kuhatarisha maisha yao na zenze gharama kubwa.
Kwa
mujibu wa wizara hiyo lengo lazima liwe kuwaondolea sababu makundi
yanayosafirisha watu kwa magendo na kunusuru maisha ya wahamiaji
kutokana na safari hizo za hatari.
Wizara
hiyo inapendekeza wahamiaji wanaochukuliwa katika bahari ya Mediterenia
ambao takriban wote wameondokea kutoka nchi iliyokumbwa na mzozo ya
Libya wapelekwe Tunisia,Misri au mataifa mengine ya Afrika kaskazini
kuomba hifadhi Ulaya kutokea nchi hizo.
Hifadhi iombwe nje
Iwapo maombi yao ya kuomba hifadhi yatakubaliwa hapo tena wahamiaji wanaweza kusafishwa kwa usalama kwenda Ulaya.
Wizara
hiyo inaongozwa na Thomas de Madziere mwanachama wa cha Christian
Demokratik cha Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye amekuwa
akikosolewa kwa sera yake ya kuwafungulia milango wahamiaji ambapo chama
hicho kimekuja kupoteza kura kwa Chama Mbadala kwa Ujerumani AfD katika
uchaguzi wa majimbo wa hivi karibuni.
Wizara
hiyo inasema pendekezo hilo liko katika hatua ya mwanzo na kwamba hakuna
mpango madhubuti juu ya pendekezo hilo au mazungumzo katika ngazi ya
Ulaya lakini wanasiasa wa upinzani wamelaani pendekezo hilo.
Bernnd
Riexinger kiongozi wa chama cha upinzani cha sera za mrengo wa kushoto
cha Die Linke amesema itakuwa ni kashfa ya kibinaadamu na hatua nyengine
zaidi ya kufuta haki ya kupatiwa hifadhi.
Amesema
maombi ya kuomba hifadhi yanapaswa yajazwe Ujerumani ili kuhakikisha
waombaji wanapatiwa msaada wa kisheria na ameuita mfumo wa Australia
kuwashughulikia wahamiaji haukubaliki kabisa.
Wahamiaji waendelea kuwasili
Askari wa
mwambao wa Italia amesema hapo Jumamosi zaidi ya wahamiaji 2,200
wameokolewa kwa siku hiyo moja katika bahari ya Mediterenia na miili
kumi ilipatikana.
Shirika
la Kimataifa la Uhamiaji limesema wiki iliopita kwamba watu 159,496
walifika Italia kwa njia ya bahari mwaka huu na 4,220 walikufa
wakijaribu kuingia Ulaya kwa njia hiyo hilo likiwa ni ongezeko la watu
3,777 kwa mwaka mzima wa 2015.
Wengi
waliohatarisha maisha yao kwa kuvuka bahari hiyo mara nyingi wanakuwa
katika maboti yaliofurika yanayoendeshwa na makundi yanayosafirisha watu
kwa magendo ambao wanakimbia mizozo na ukandamizaji kutoka kwenye nchi
zao.DW
0 comments:
Post a Comment