METDO Tanzania

METDO Tanzania

Monday, September 19, 2016

Serikali Kuwasaidia Watanzania Kushiriki Katika Ujenzi wa Tanzania ya Viwanda

Serikali imeahidi kuwasaidia wazalishaji wadogo wa bidhaa mbalimbali zikiwemo bidhaa za ngozi kwa kuwajengea uwezo wa kuzalisha bidhaa nyingi na bidhaa bora, ili wazalishaji hao wageuke ni viwanda vidogo, ili uchumi wa Tanzania ya Viwanda, viwanda hivyoviwe vinamilikiwa na Watanzania wakiwemo wazalishaji wadogo wa bidhaa mbalimbali.
Ahadi hiyo imetolewa jana na Katibu Mkuu, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Prof Adolf Mkenda kwenye mkutano wa wazalishaji wa bidhaa za ngozi  uliokwenda sambamba na maonyesho ya siku moja ya bidhaa za ngozi nchini yaliofanyika jana kwenye Viwanja wa Maonyesho ya Saba Saba, vya Mwl. J.K.Nyerere, Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
 
Prof. Mkenda alisema , serikali ya awamu ya tano ina nia ya dhati ya kuwawezesha Watanzania kuumiliki uchumi wa taifa kwa kuweka mazingira wezeshi na vivutio mbalimbali na masharti nafuu kwa Watanzania kushiriki katika Tanzania ya Viwanda, ila ametoa changamoto kwa wazalishaji hao kuunganisha nguvu zao kwa pamoja na kuunda viwanda vidogo vidogo hivyo kuwa rahisi kusaidiwa kwa pamoja kuliko mmoja mmoja.
 
Prof. Mkenda alisema “Serikali inavipaumbele vya kuwawezesha wazawa kuanzisha viwanda ili kukuza bidhaa za Tanzania ikiwemo bidhaa za sekta za ngozi, hivyo mnapaswa kuwa na ujasiri wa kuzalisha na kutumia fursa hiyo kwa ajili ya ushindani”
 
Pia alitumia muda huo kuwahamasisha wazalishaji hao kutumia soko la pamoja la jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) pamoja na soko la SADC maana wanahaki ya kuuza kwenye kanda hizo.

 Na aliwaasa kutumia taasisi zingine za serikali zinazoweza kuwainua kwenye sekta hiyo ili kuondokana na changamoto mbalimbali watambue kuwa serikali inajipanga kukomesha bidhaa za mtumba nchini ili kuboresha soko la bidhaa bora zinazozalishwa katika nchi yetu.
 
Prof. Mkenda alimalizia kwa kutoa changamoto kwa Mamlaka ya Biashara Tanzania, kuandaa maonyesho mbalimbali yakiwemo maonyesho ya kisekta, ili viwanja vya maonyesho vya Saba Saba vitumike wakati wote wa mwaka mzima kwa maonyesho mbalimbali, na sio kipindi cha Saba Saba tuu mpaka Saba Saba nyingine, na kutoa vito kwa Tantrade kutoa maeneo ya kudumu kwa wajasiliamali na wazalishaji wadogo wadogo wapate maeneo rasmi ya kuonyesha bidhaa zao wakati wote.
 
Naye kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade), Edwin Rutageruka akijibu changamoto za Katibu Mkuu, alisema kwa kuanzia,  TanTrade ipo tayari kuwapa mafunzo ya ujasiliamali ya namna watakavyoweza kupenya kwenye masoko mbalimbali ili kukuza sekta hiyo ya ngozi, na kutenga eneo maalum kwa wazalishaji wadogo wadogo wa bidhaa mbalimbali na wajasiliamali kuonyesha bidhaa zao na pia kuanza mchakato wa kuutumia uwanja wa maoyesho ya Saba Saba kuendeshea magulio ya masoko ya Jumamosi na Jumapili, (Saturday Market na Sunday Market).

Mwenyekiti wa chama cha wazalishaji wa bidhaa za ngozi (TALEPPA)Dedan Munisi, alisisitiza sasa umefika wakati kwa Watanzania sio tuu kwa kuonyesha uzalendo wa kuthamini bidhaa za ndani, bali kuzinunua na kuzitumia bidhaa zinazozalishwa na Watanzania wenyewe, na kuwataka kuacha kasumba ya kudharau chako na kuthamini cha mwenzio kwa kutukuza bidhaa za nje kwa kudhani zina ubora zaidi kuliko zile zinazolishwa nchini, na kusisitiza bidhaa za ngozi zinazozalishwa nchini zina ubora wa hali ya juu kuliko bidhaa za nje.

Kwa upande wao, Wazalishaji hao wakiongozwa na Denis D. Kileo mzalishaji wa bidhaa za ngozi kutoka Woiso Original Products alisema changamoto kubwa ni watanzania kutoweza kutofautisha viatu vya ngozi bandia kutoka nje ya nchi vyenye ufanano na bei kuwa chini hivyo sekta hiyo  kudumaa  ni wakati sasa wauzaji wa maduka mbalimbali nchini kuwaamini wazalishaji na bidhaa za sekta ya ngozi na kuvipeleka mbele sokoni bidhaa zao ili kupanua masoko.

Naye Bi. Cecilia China mtafiti kutoka TIRDO aliwashauri wazalishaji wa bidhaa za ngozi kutumia taasisi za serikali za kisayansi nchini ili kuondokana na changamoto mbalimbali zinazowakabili kwenye sekta hiyo ili kupunguza gharama kwenye uzalishaji wa bidhaa zao na waweze kushauriwa kitaalam njia bora ya uzalishaji wenye kukidhi soko la ndani na nje ya nchi. 
 
Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) (TanTrade) ikishirikiana na na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wameandaa mkutano huo wa wazalishaji wa bidhaa za ngozi kwa lengo la kuwakutanisha wadau wa serikali na sekta binafsi ili kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kuendeleza sekta hiyo ambayo inamchango mkubwa uchumi wa taifa kuelekea kenye Tanzania ya viwanda.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com