Wabunge Chadema wawaangukia viongozi wa dini
WABUNGE wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kaskazini, wamewaomba maaskofu na mashehe kusaidia kumshauri Rais John Magufuli akubali kuruhusu vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara.
Walisema endapo viongozi hao wa dini, watafanikiwa katika ushawishi wao, nchi itaepuka uwezekano wa kuingia kwenye machafuko kutokana na utekelezaji wa Operesheni Ukuta waliyotangaza kuanza Septemba Mosi mwaka huu.
Akizungumza kwa niaba ya wabunge wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Godbless Lema, alisema ni viongozi wa dini pekee ndio wanaweza kusaidia kumshauri Rais Magufuli ili vyama vya siasa, viruhusiwe kufanya mikutano ya hadhara.
Alisema msimamo wa wabunge wa Chadema wa Kanda ya Kaskazini ni kufanya mikutano kuanzia Septemba Mosi ili kudai uhuru wa vyama vya siasa wa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, kama njia ya kukuza demokrasia nchini.
"Wakati bado tunasuguana sisi na vyombo vya dola, tunawaomba viongozi wetu wa dini maaskofu, mashehe na wachungaji wamshauri Rais wetu ili atuachie uhuru huu ambao ni wa kikatiba ,” alisema Lema.
Alisema hivi sasa viongozi wa vyama vya upinzani nchini, wananyimwa demokrasia kwa kiwango kikubwa, hivyo watafanya maandamano hayo wakiwa na lengo moja tu la kudai uhuru wa Kikatiba ambao alisema serikali imeupoka.
Alisema agizo kwamba viongozi wa siasa wanaruhusiwa kufanya mikutano katika maeneo waliyochaguliwa, hawakubaliani nalo kwa vile linapingana na dhana ya ukuaji wa demokrasia.
“Suala la kuruhusu kiongozi kufanya mikutano katika eneo lake hatukubaliani nalo kwani kufanya hivyo ni kuuwa demokrasia. Ina maana kama chama hakina mwakilishi katika eneo fulani hakitaruhusiwa kufanya mkutano, hivyo chama hakiwezi kukua..."
"Lakini wakati Rais anasema haya, tumemwona Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher ole Sendeka ambaye si Mbunge, akifanya mkutano wa hadhara Longido hivi karibuni, hivyo hili la kutubana sisi wapinzani tu hatukubaliani nalo,” alisema Lema.
Mwenyekiti wa Wabunge Kanda ya Kaskazini, Joseph Selasini alisema kuwa wao kama wabunge wa kanda hiyo, wanaunga mkono maazimio ya Kamati Kuu ya kufanya mikutano na maandamno ili kupinga kuzuiwa kwa vyama vya siasa kufanya shughuli zake kwa mujibu wa sheria.
Alisema zipo hatua zinazochukuliwa na serikali ya sasa katika kudhibiti uendeshaji wa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu, hatua alizodai hazijawahi kuchukuliwa na awamu nyingine za uongozi wa nchi.
Akitaja baadhi ya kasoro, Selasini alisema ni zuio la Bunge kuoneshwa ‘Live', zuio la mikutano ya vyama vya siasa, na kuongeza kwamba zipo taarifa kwamba baadhi ya vyombo vya habari, vitazuiwa kurusha habari za upinzani ili kuviua, jambo alilosema litarudisha nyuma maendeleo ya nchi.
"Hali hii lazima tuipinge kwa nguvu zetu zote, maana yapo madhara makubwa kwa mambo haya kuachwa kuendelea kutokea na mwisho nchi haitakuwa na maendeleo yanayokusudiwa,” alisema Selasini.
Alisema wabunge hao wa Kanda ya Kaskazini, wanaomba Jeshi la Polisi kumuachia huru au kumpeleka mahakamani mara moja Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ili haki itendeke.
Kwa upande wake, Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari alisema ili CCM iweze kujipatia ushindi mkubwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, inapaswa kusimamia utekelezaji wa Ilani yake ya 2015/2020, badala ya kushughulika na upinzani.
Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alisema chama hicho kimekamilisha maandalizi yote kwa ajili ya kufanya mikutano ya hadhara kuanzia Septemba Mosi, kama ilivyoazimiwa na Kamati Kuu ya chama hicho hivi karibuni.
0 comments:
Post a Comment