METDO Tanzania

METDO Tanzania

Saturday, August 27, 2016

KONGAMANO LA DIASPORA LIMENIFUNZAMENGI…!

 
 Neno La Wakati Mwema

‘BRIDGING TANZANIA TOURISM AND INVESTMENT : ’A NEW OUTLOOK :” KIUNGANISHI CHA UTALII NA UWEKEZAJI: MTIZAMO MPYA

Na Mathias Canal

Baada ya safari nyingi mfululizo hatimaye leo nimeingia Mkoani Singida ambapo nitakuwa hapa kwa mapumziko ya siku kadhaa

Ndugu zangu kwanza Napenda kuchukua nafasi hii na kutoa shukrani za dhati kwa Mhe. Dkt Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kuwa mwenyeji na kukubali kuwa mgeni rasmi katika kongamano la Tatu la Diaspora lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Zanzibar Beach Resort, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar. Uwepo wake katika Kongamano hilo ni ishara kubwa ya mapenzi ya dhati aliyonayo kwa Diaspora na kutambua umuhimu wa mchango wao katika kuleta maendeleo ya nchi yetu.

Katika hotuba ya Dkt Shein alisema kuwa Serikali zote mbili zimepanua fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii, biashara, viwanda, kilimo, ufugaji, uvuvi wa bahari kuu, ujenzi wa nyumba, na sekta nyengine mpya zinazoibuka katika uchumi wa nchi ikiwemo sekta ya mpya ya gesi na mafuta ambayo kwa Zanzibar inatarajiwa kuimarika katika miaka michache ijayo.
Miongoni mwa mengi yaliyonivutia ilikuwa ni pale Dkt Shein alipowataka Wana “Diaspora” kuendelea kuwa na ujasiri na kuwa tayari kuzichangamkia fursa hizo kama wanavyofanya wana “Diaspora” kwa kuleta mabadiliko makubwa katika nchi zao ikiwemo Ghana, Brazil, Ethiopia na India.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ilianzisha Idara ya Diaspora mwaka 2010 kwa lengo la kuwatambua Watanzania wanaoishi ughaibuni na kuwahamasisha katika kuchangia maendeleo ya nchi kwa kutumia mitaji, ujuzi na elimu wanayoipata wakiwa nje ya nchi kwa manufaa ya Taifa lao.Tangu ilipoanzishwa Idara, kumekuwa na jitihada mahsusi za kuwahamasisha na kuwashirikisha Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Balozi Mahiga akimkaribisha Rais wa Zanzibar, Dk Shein kwenye ufunguzi wa Kongamano la tatu la Diaspora alisema kuwa lengo la makongamano hayo ambayo mpaka sasa yamefanyika kwa miaka mitatu mfululizo wakati wa utawala wa Rais mstaafu Jakaya Mrisho Khalfan Kikwete limefanyika mara mbili na wakati wa utawala wa serikali ya awamu ya tano chini ya utawala wa Dkt John Pombe Joseph Magufuli tayari limefanyika mara moja kuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi ya kuwakutanisha Diaspora na Taasisi mbalimbali zilizopo nchini ili kutumia nafasi hiyo kubadilishana mawazo, elimu na ujuzi katika kuleta maendeleo nchini. Azma hiyo pia inalenga kuongeza fursa za uwekezaji na kupanua soko la bidhaa la biashara ndogondogo na za kati ndani na nje ya nchi.

Kongamano la Mwaka huu limebeba kauli mbiu isemayo ‘Bridging Tanzania Tourism and Investment : ’A new Outlook :” kwa kiswahili tunasema kiunganishi cha utalii na uwekezaji: mtizamo mpya ikiwa ni azma ya Serikali kuleta mwonekano mpya wa kujenga Tanzania yenye matumaini ya uchumi wa kati. Diaspora wakiwa wadau wa maendeleo wana nafasi kubwa ya kuimarisha maendeleo ya utalii na sekta ya uwekezaji kwa mustakabali wa ukuaji wa uchumi wa nchi yetu tukufu ya Tanzania.

Ufanisi wa Kauli Mbiu hii imechaguliwa ili kuweka msisitizo wa jitihada za Serikali katika kukuza sekta ya utalii na uwekezaji katika uchumi wa nchi, ili kuongeza nafasi za ajira nchini. Ambapo Kongamano hilo limekuwa ni chachu ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii na uwekezaji nchini kwa kushirikiana na Diaspora wetu katika nchi wanazoishi.

Miongoni mwa kauli nilizozinukuu kwa Dkt Shein ni pamoja na pale aliposema kuwa kwa upande wa Zanzibar, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kutayarisha Sera ya “Diaspora” ambayo itapitishwa wakati wowote kuanzia hivi sasa ambapo baada ya kukamilika itafafanua na kuweka wazi dira na dhamira za Serikali katika utekelezaji wa masuala muhimu yanayohusiana na Diaspora. Alieleza kuwa Sera hiyo itaelekeza njia bora za kutuma na kupokea fedha pamoja na kuimarisha misaada ambayo wamekwua wakiitoaa kwa ajili ya utekelezaji wa mipango ya maendeleo sambamba na kubainisha sheria na wahusika muhimu katika kuyashughulikia masuala ya “Diaspora”.

katika siku mbili za Kongamano hilo lililoanza Jumatano Agosti 24 na kumalizika Agosti 25 kulikuwa na uwasilishwaji wa mada zilizotolewa na Watendaji Wakuu wa Wizara, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi Lengo mahsusi ikiwa ni kuwapatia washiriki, hususani Diaspora ufahamu na fursa mbalimbali zilizopo katika sekta ya utalii na uwekezaji ambao unachangia katika maendeleo ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Ushiriki wa Kongamano hilo ulijumuisha vikundi vya wafanyabiashara, Taasisi mbalimbali za utalii, Diaspora waliorejea baada ya kuishi ughaibuni kwa muda mrefu na wadau wengine kutoka taasisi za umma na binafsi ziilizopo nchini.

Vilevile, kama ilivyokuwa mwaka jana, Kongamano la mwaka huu lilihudhuriwa na maafisa kutoka Ofisi za Balozi zetu nje ya nchi. Lengo la kuwashirikisha maafisa hao ilikuwa ni kuhakikisha kuwa wanafuatilia utekelezaji wa maazimio yaliyopitishwa wakati wa Kongamano.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwanasihi Wana “Diaspora” waendelee kuwa mabalozi wazuri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi wanazoishi pamoja na kuwa mfano wa tabia njema ili waendeleze sifa ya ukaribu, urafiki na usalama ambayo Tanzania na raia wake wamejijengea na kutambulika katika mataifa yote duniani.

“Zielezeeni sifa nzuri za nchi yetu pamoja na watu wake”,alisema Dk. Shein na kuwataka Wana ‘Diaspora” kuendelea kuishi kwa kuzingatia misingi ya urafiki na udugu huku mkiwa na mapenzi makubwa baina yao pamoja na nchi yao ya asili.

Sambamba na hayo, Dk. Shein aliwataka wana ‘Diaspora’ kuendeleza utamaduni wa kuja kutemebea nyumbani kila baada ya muda, jambo ambalo ni muhimu na linaimarisha mapenzi baina yao na ndugu, jamaa na wazazi wao.

Dk. Shein pia, alitumia fursa hiyo kuwataka Wana “Diaspora” wakija nyumbani kufanya jitihada za kuja na watoto wao ili nao wapate fursa za kuyaona mambo mbali mbali ili waweze kuyathamini mambo ya nchi yao ya asili.

“Jengeeni utamaduni wa kuja nyumbani mara kwa mara kwa ajili ya kufuatilia mambo yenu na fursa zilizopo, msipende kuagiza, zingatieni ule usemi maarufu wa lugha yetu kuwa “kuagiza kufyekeza”, aliongezan Dk. Shein.

Viongozi hao walitoa shukurani kwa Taasisi za Umma na Taasisi binafsi pamoja na mashirika mbali mbali ya serikali na yasiokuwa na serikali yaliosaidia kuchangia Kongamano hilo pamoja na kulidhamini.

Katika ushiriki wangu pia nimejifunza namna ambavyo baadhi ya watanzania wanasifika katika mataifa ya nje kwa usambazaji wa dawa za kulevya ambao nchi mbalimbali ikiwemo Afrika ya kusini umebatizwa jina maarufu sasa Dawa za kulevya (UNGA) sasa unaitwa Mweupe. Jambo hili limenifedhehesha sana lakini limenipa taswiranzuri kujua kuwa Tanzania yangu sasa inahitaji zaidi kujikita katika kukemea Biasharahii haramu ya Dawa za kulevya kama ambavyo imeweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kukemea wizi wa fedha za umma.

Naaaam ‘BRIDGING TANZANIA TOURISM AND INVESTMENT : ’A NEW OUTLOOK :” KIUNGANISHI CHA UTALII NA UWEKEZAJI: MTIZAMO MPYA

KONGAMANO LA DIASPORA LIMENIFUNZAMENGI…!

Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal
0756413465
Singida

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com