Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akichangia
damu kwa ajili ya wananchi wanaofariki kwa kukosa huduma ya damu katika
hospitali mbalimbali nchini
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu akihojiwa
kuhusu umri na mambo kadha wa kadha ili kufanyika utambuzi kama damu yake
inatosha kiasi cha kutoa kwa ajili ya wengine, Mtaturu amechangia Unit 450 ya
damu yaani chupa moja.
Na Mathias Canal, Singida
Wananchi wametakiwa kufanya kazi kwa kushiriana na viongozi
na watumishi wengine wa afya ili kuleta mabadiliko na kuhakikisha kuwa maisha
ya wananchi yanakuwa bora zaidi.
Mwito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe. Miraji
Jumanne Mtaturu wakati wa uzinduzi wa uchangiaji wa damu salama, Mfuko wa Afya
(CHF) na Daftari la ufuatiliaji akinamama wajawazito Wilayani humo.
Akizungumza na wananchi wa wilaya hiyo Mtaturu amesema kuwa
pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali
suala la vifo vya kina mama wajawazito, watoto wadogo pamoja na upungufu
wa dawa katika vituo vya afya bado ni changamoto.
Amesema Takwimu zinaonyesha kuwa katika Wilaya ya Ikungi
vifo vya akina mama vinaongezeka mwaka hadi mwaka ikiwa mwaka 2013 ilikadiriwa
kupoteza akinamama 79 kwa kila vizazi hai 100,000 na hesabu hiyo imeongezeka na
kufikia 94/100,000 kwa mwaka 2014 na 201/100,000 kwa mwaka 2015.
“Hali hii haikubaliki ndugu zangu wa Kata ya Minyughe na
Wilaya ya Ikungi kwa ujumla mbaya zaidi
matatizo yanayopelekea vifo hivyo yanatokana na sababu ambazo zinaweza
kuzuilika, kwa mfano, ukosefu wa damu katika vituo vyetu vya afya na
kutozingatia vidokezo vya hatari tunavyoelekezwa wakati wa mahudhurio ya
kliniki” Alisema Mtaturu.
Sanjari na hayo Mtaturu alisema kuwa matatizo makubwa yanayopelekea vifo vya akina
mama wajawazito ni kutokuzingatia vidokezo hatari kama wataalamu
wanavyoelekeza kwenye vituo vya kutolea
huduma za afya, hali ambayo inapelekea akinamama wanaotakiwa kujifungua
Hospitalini wanalazimika kujifungulia nyumbani au kwenye Zahanati ambapo
pakitokea dharura wanashidwa kupata msaada.
Kutokana na hali hiyo Mtaturu amesema kuwa ili kuhakikisha
wajawazito wote wanaenda Kliniki na kufuata wanayoelekezwa Wilaya ya Ikungi
imeanzisha daftari la ufuatiliaji ambapo jamii itasaidia kuwakumbusha
wajawazito kwenda Kliniki na kuchukua hatua pale ambapo hawatafanya hivyo.
“Lengo kuu ni kuhakikisha akina mama wajawazito wote
wanahudhuria kliniki mapema na kuhudhuria angalau mara nne ili kupunguza
vifo ambavyo vinaweza kuzuilika Sasa ninawataka wenyeviti na watendaji wote wa vijiji kufanya
ufuatiliaji wa daftari hilo kuona kama akina mama wajawazito wanahudhuria kama wanavyotakiwa na kunipatia
taarifa ya utekelezaji wake kila mwezi.”Alisema Mtaturu
Akizungumzia suala la ukosefu wa damu salama katika vituo
vya afya Mtaturu amesema kuwa Wilaya ina mahitaji ya wastani wa Unit 1000 kwa Mwaka na kwa kuzingatia hilo
umewekwa mkakati wa kuhamasisha jamii
angalau iweze kutoa damu mara moja kila mwezi kwa kila Kata.
“Kwa Mwananchi au mtu yeyote ambaye atakuwa amepata tatizo
la upungufu wa damu na kuhitaji kuongezewa damu katika hospitali zetu
hatahitajika kulipia gharama yeyote inayohusu kuongezewa damu kwa sababu
tutakuwa tumejiwekea akiba ya damu yetu wenyewe” Alisema Mtaturu.
Aidha Mtaturu ameongeza kuwa
mabadiliko katika sekta ya Afya yanayoendelea kutekelezwa katika utoaji
huduma yana lengo la kuinua kiwango cha ubora wa huduma za afya kwa wananchi na
kuongeza kiwango cha uwajibikaji kwa wasimamizi na watoaji wa huduma hizo na
ili kufanikisha lengo hilo, madaraka, majukumu na kazi, rasilimali zaidi za
Afya zinahitajika kwa kuitaka jamii kuchangia katika mifuko ya afya ya jamii
(CHF).
Alisema Mfuko wa afya ya jamii (CHF) kwa Kaya moja itatakiwa kuchangia
Tsh. 10,000/= na atatibiwa Baba, Mama na Watoto wanne kwa mwaka mzima na
kuongeza kuwa mfuko huo hautaimarika kama hautakuwepo usimamizi imara na
unaoambatana na uadilifu.
“Miongoni mwa manufaa ya mabadiliko ya sekta ya afya ni
pamoja na jamii yenyewe kuwa na madaraka zaidi ya kuamua kuhusu huduma za afya
zinazotolewa na kushiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma hizo kwa
kuwakilishwa katika bodi ya afya ya wilaya na kamati za huduma za afya za vituo”
Alisema Mtaturu
Katika kuhitimisha uzinduzi huo Mkuu huyo wa Wilaya ya
Ikungi Mtaturu Jumanne Mtaturu alizindua rasmi matumizi ya Daftari la
ufuatiliaji kwa kuwakabidhi madaftari hayo wenyeviti wa vitongoji wa kata hiyo
pamoja na kuanza zoezi la utoaji damu kwa wilaya nzima ya Ikungi.
Jumla ya Watu waliochangia Damu ni 36 ambapo Wastani wa damu
iliyotolewa kwa mtu mmoja ni Unit 450. Hivyo tukizidisha 36 × 450 tunapata Unit
16,200 ambazo ni sawa na lita 16.2 za Damu zilizopatikana mara baada ya uzinduzi.
DC Mtaturu amehamasisha wananchi Wilayani Ikungi kujiunga na
mfuko wa Afya ya jamii (CHF) kwani itasaidia kuboresha upatikanaji wa dawa na
vifaa tiba kwa Wilaya ya Ikungi ambayo ina Kaya 53823 huku wananchi waliojiunga
na mfuko huo wakiwa ni asilimia 24% tu.
0 comments:
Post a Comment