METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, February 28, 2016

Waziri wa Elimu Prf Ndalichako Awasimamisha Kazi vigogo watatu

 
JOYCE Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, amewasimamisha kazi watumishi watatu wa Bodi ya Taasisi ya Elimu nchini (TET) kwa kushindwa kusimamia   sheria ya manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu ili kupisha uchunguzi

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Maimuna Tarishi ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, amesema watumishi hao hawakutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuruhusu vitabu hivyo kuchapishwa vikiwa na mapungufu.

“Mnamo tarehe 22 Januari mwaka 2016 bodi hiyo ilishauriwa kusitisha uchapaji wa vitabu uliokuwa ukifanywa na kampuni ya Yukos Enterprises Ltd baada ya kubainika kuwa na mapungufu, lakini haikusitisha,” amesema Tarishi na kuongeza.

“Serikali iliamua kusitisha uchapishaji wa vitabu hivyo ili isiendelee kupokea vitabu vyenye mapungufu, hata hivyo taasisi ya elimu haikusitisha uchapishaji wa vitabu hivyo, badala yake kampuni hiyo ilichapisha vitabu vyote ilivyopangiwa,” amesema Tarishi.

Tarishi amesema ufuatiliaji uliofanywa na wizara katika bohari ambayo ilikuwa inapokea vitabu hivyo, ulibaini kuwa vitabu vilivyowasilishwa na kampuni ya Yukos vilikuwa na kasoro.

“Kutokana na kasoro hizo, Taasisi haikutekeleza wajibu wake wa kusimamia uchapaji wa vitabu na uzingatiaji wa sheria ya manunuzi kikamilifu,” amesema.

Kutokana na mapungufu hayo, Wizara imetoa maagizo ya kuondolewa kwa baadhi ya vitabu vilivyowasilishwa kwenye bohari ya serikali ifikapo tarehe 29 Februari mwaka huu.

“ Taasisi ya Elimu iwasimamishe kazi mara moja watumishi wafuatao ambao walikuwa na jukumu la kusimamia sheria ya manunuzi na kazi ya uchapaji wa vitabu ili kupisha uchunguzi,” amesema.

Amewataja watumishi hao kuwa ni  Peter Bandio, aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Vifaa vya Kielimu, Pili Magongo Mwanasheria wa TET na Jackson Mwaigonela Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi.

Mapungufu yaliyoonekana kwenye vitabu hivyo ni  upungu wa mwingiliano wa rangi, upungufu wa kurasa katika vitabu, ukataji usiozingatia vipimo,vitabu kuchakaa kabla ya matumizi na mpangilo mbaya wa kurasa.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com