Mwanasheria Mkuu wa Serikali amuunga mkono Jecha
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, George Masaju amemuunga mkono Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha, kwa kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana na kusema hatua hiyo ni halali kutokana na sababu zilizotajwa.
“Ukichukua kasoro zote na hii ya mgombea kujitangaza mshindi... ni tatizo kubwa, lazima mtaingia kwenye matatizo iwapo huyu kajitangazia ushindi halafu matokeo yamtangaze mshindi tofauti na huyo,” alisema Masaju.
Akizungumza kwenye kipindi cha Siku 100 za Serikali ya Awamu ya Tano, kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC1), juzi usiku, Mwanasheria huyo alisema ZEC iko huru kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar na uamuzi uliofanywa na Mwenyekiti wa Tume hiyo ni kitendo halali.
Masaju alisema kasoro zote zikichunguzwa, ikiwemo hiyo ya mgombea kujitangazia ushindi, kulikuwa na kila sababu ya kufuta matokeo hayo ili uchaguzi urudiwe.
Alisema iwapo dosari hizo, zingeachwa bila kufanyiwa kazi, hata wagombea wasio na sifa ya kushinda katika uchaguzi huo, wangesema na wao ni washindi hivyo kungetokea machafuko ambayo yangeweza kuleta matatizo makubwa zaidi.
Ila kwa hatua iliyochukuliwa na ZEC ni jambo sahihi la kurudisha amani na kupanga tarehe nyingine ya kurudia uchaguzi huo, ili kasoro hizo zirekebishwe na mshindi apatikane kwa haki na kuepuka machafuko.
Masaju alisema awali Rais John Magufuli wakati akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu achaguliwe, alisema atashirikiana na Rais wa Zanzibar kumaliza suala la uchaguzi, ila hakusema ataingilia uhuru wa Tume.
“Rais alipohutubia Bunge kwa mara ya kwanza aliahidi kushirikiana na Rais wa Zanzibar kumaliza suala la uchaguzi, ila hakusema ataingilia uhuru wa Tume na ndicho alichofanya, Zanzibar ina amani,” alisema Masaju.
0 comments:
Post a Comment