METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, December 15, 2023

JICHO LANGU (Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi 2022 na Uchumi wa Taifa)


Na Debora Charles (Mtakwimu) 

Sensa ya watu na makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. 

Sensa husaidia nchi kupata takwimu zinazowezesha kupanga mipango ya maendeleo na kupeleka huduma stahiki kwa watu wake. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilifanya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu SURA 351 kadhalika kufuatia kukidhi takwa la Umoja wa Mataifa ambalo linazitaka nchi zote kufanya Sensa ya Watu na Makazi angalau mara moja ndani ya miaka kumi. 

Tangu kuasisiwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1964, Sensa ya Watu na Makazi imefanyika katika vipindi sita kikiwemo kipindi hiki cha mwaka 2022. Sensa zingine zilizopita zilifanyika miaka ya 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012. 

Hata hivyo kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita; chini ya uongozi mahiri na shupavu wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha kwamba Tanzania inanufaika na matokeo chanya ya sayansi na teknolojia, kwa mara ya kwanza zoezi hili limefanyika kidigitali. Pamoja na mafanikio mengine, ufanyikaji wa zoezi hili kidigitali umewezesha upatikanaji wa matokeo kwa wakati.

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watanzania wote inatajwa kuwa ni watu 61,741,120 kati yao wanaume ni 30,053,130 sawa na asilimia 48.7 na wanawake ni 31,687,990 sawa na asilimia 51.3 ya watu wote. 

Kadhalika, Tanzania Bara inatajwa kuwa na watu 59,851,347 kati yao wanaume ni 29,137,638 na wanawake ni 30,713,709 na Tanzania Zanzibar inatajwa kuwa na watu 1,889,773 kati yao wanaume ni 915,492 na wanawake 974,281.

Idadi ya watanzania tangu kuasisiwa kwa uhuru (yaani kuanzia Sensa ya mwaka 1967) imekuwa ikiongezeka na ongezeko hilo linatajwa kuwa ni mara tano zaidi ya ilivyokuwa mwanzo; kwamba mwaka 1967 Tanzania ilikuwa na watu 12,313,469 na mwaka 2022 imeongezeka hadi kufikia watu 61,741,120. Ongezeko hili linaashiria uwepo wa watu wengi nchini katika miaka ijayo. 

Uwepo wa watu wengi katika nchi unaweza kuwa fursa ya kujiletea maendeleo ya kiuchumi na hatimaye kupeperusha bendera ya nchi kimataifa. Ripoti mbalimbali, zinataja nchi zenye watu wengi zaidi duniani, kuwa ni miongoni mwa nchi zenye utajiri mkubwa.

Kwa mujibu wa takwimu za Oktoba 2022 za Shirika la Fedha la Kimataifa, China (yenye watu takribani ya bilioni 1.4) inatajwa kuwa ni nchi ya pili kwa utajiri duniani inayomiliki dola za kimarekani bilioni 18.321 na India (yenye takribani watu bilioni 1.4) kuwa ni nchi ya tano yenye kumiliki dola bilioni 3.469 za kimarekani. 

Aidha, Ripoti ya pamoja ya Shirika Fedha Duniani (IMF) na Benki ya Dunia ya mwaka 2021 inaitaja nchi ya Nigeria kuwa ni nchi ya pili kwa utajiri barani Afrika, pamoja na kuwa na idadi kubwa zaidi ya watu (wapatao milioni 206.1) barani humo.

Idadi kubwa ya watu ni fursa ya kuimarisha uchumi endapo watu hao watakuwa wazalishaji na watapatiwa huduma stahiki katika uzalishaji. China, ikiwa ni miongoni mwa nchi zenye watu wengi zaidi duniani, inatajwa kuendelea kukua kiuchumi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo; kuwa na miundombinu imara, uwekezaji katika viwanda na kuwepo kwa sera ya mageuzi na ufunguaji mlango. 

Fadhili Mpunji katika makala yake ya China kwa Macho Yangu iliyochapishwa kwenye Jarida la Daily Nation anataja sababu za nchi ya China kufanikiwa kiuchumi kuwa mojawapo ni China kuweka mpango kamili na uwekezaji wa muda mrefu kwenye sekta ya miundombinu, ikiwemo kuunganisha mikoa yote na miji yote kwa njia za ndege, reli na barabara. 

Fadhili anasema, hali hii imepelekea China kuwa ni nchi yenye mtandao mkubwa wa reli za kasi na barabara za mwendokasi ambazo zimeleta mchango mkubwa kwenye maendeleo ya biashara. 

Aidha, uwepo wa Sera ya mageuzi na ufunguaji mlango imekuwa ni kichocheo cha uwekezaji mkubwa uliotokana na wachina waliokuwa wanaishi nje ya nchi, wageni wenye asili ya China na hata wale wasio na asili ya China kuruhusiwa kufungua biashara zao. Hali ambayo imeleta ajira mpya, ujuzi mpya na kuiongezea serikali mapato yanayotokana na kodi, anafafanua.

Tanzania, ikiwa ni miongoni mwa nchi ambayo watu wake wanaongezeka, ina jukumu kubwa la kuhakikisha watu wake wanakuwa fursa na wanazalisha uchumi. Kwa kuzingatia hilo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imeweka juhudi kubwa katika kuhakikisha ongezeko hili linakuwa tija kwa nchi. Rais Samia kupitia uongozi wake, ameweza kufanya mabadiliko ya sera za uwekezaji, kuimarisha mazingira wezeshi kibiashara na diplomasia ya uchumi.

Kadhalika, ameimarisha miundombinu hususan barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari, huduma za kiuchumi na kijamii, ujenzi wa madarasa, hospitali, zahanati na vituo vya afya, huduma za maji pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika utalii.

Jicho langu linatoa wito kwa jamii hususani kwa watu wenye umri wa kufanya kazi; tuwajibike ipasavyo kutumia fursa na huduma zinazotolewa na Serikali ili kujinufaisha kiuchumi. Fursa kama ya uwepo wa elimu bure ituwezeshe kupeleka watoto wote shule ili wajipatie elimu na ujuzi wa kuzalisha. Kadhalika fursa ya upatikanaji wa huduma za afya itusaidie kujenga utamaduni wa kupima afya mara kwa mara, na kujipatia matibabu kwa wakati ili kuhakikisha jamii inakuwa na afya imara katika uzalishaji.

Taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi 2022 inatoa takwimu za makundi mbalimbali wakiwemo; watu wenye umri chini ya miaka 15, vijana, watu wenye umri wa kufanya kazi, wazee, wanawake wenye umri wa kuzaa na watanzania wanaoishi vijijini na mijini kwa kuzingatia jinsi. Jicho langu limeangazia makundi yafuatayo; 

Watu wenye umri chini ya Miaka 15 (Miaka 0-14). Kundi hili limetajwa kuwa na idadi ya watu 26,399,988 sawa na asilimia 42.8 ya watanzania wote nchini. Takwimu zinaonyesha Idadi ya watu katika kundi hili, imepungua kutokea mwaka 2002 hadi mwaka 2022. Kwa mujibu wa Takwimu za mwaka 2002, kundi hili limetajwa kuwa na asilimia 44.3 ya watu wote, mwaka 2012 asilimia 43.9, na na mwaka 2022 asilimia 42.8. 

Vijana (Miaka 15-35). Kwa Mujibu wa Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007, Kijana ni mtu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 35. Kundi la vijana nchini lemetajwa kuwa na idadi ya watu 21,312,411 sawa na asilimia 34.5 ya watanzania wote, ikiwa na maana kwamba katika kila kundi la watu 10, kuna vijana 4. Hata hivyo, idadi ya vijana nchini inatajwa kuwa ikipungua kutoka mwaka 2002 hadi 2022. 

Takwimu za mwaka 2002, zilinataja kundi hili kuwa na asilimia 35.6, mwaka 2012 asilimia 34.7 na za mwaka 2022 asilimia 34.5 ya watu wote. 

Watu Wenye Umri wa Kufanya Kazi (miaka 15-64). Takwimu zinataja, zaidi ya nusu ya watanzania wote wapo kwenye umri huu. Kundi hili lina idadi ya watu 33,000,224 sawa na asilimia 53.4. 

Hata hivyo takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watu katika kundi hili imekuwa ikiongezeka katika vipindi vitatu mfululizo vya Sensa. Mwaka 2002, lilitajwa kuwa na asilimia 51.9, mwaka 2012 asilimia 52.2 na mwaka 2022 asilimia 53.4. Aidha, idadi ya wanawake wenye umri huu inatajwa kuwa kubwa ukilinganisha na ya wanaume.

Takwimu zinaonyesha idadi ya wanaume ni 15,828,450 sawa na asilimia 52.7 ya wanaume wote nchini na idadi ya wanawake ni 17,171,774 sawa na asilimia 54.2 ya wanawake wote nchini. 

Katika mfululizo wa vipindi vitatu vya ufanyikaji wa Sensa, idadi ya wanaume na wanawake waliopo kwenye umri huu imekuwa ikiongezeka, pamoja na ongezeko hilo, wanawake wanaendelea kutajwa kuwa na idadi kubwa ukilinganisha na wanaume.

Mwaka 2002 wanawake walikuwa ni asilimia 52.9, mwaka 2012 asilimia 53.3 na mwaka 2022 asilimia 54.2 ya watu wote. Mwaka 2002 wanaume walikuwa ni asilimia 50.7, mwaka 2012 asilimia 51.1 na mwaka 2022 hadi asilimia 52.7 ya watu wote.

Uwepo wa wanawake wengi wenye umri wa kufanya kazi, ni tija kwa taifa. Hii ni kwa sababu ushiriki mkubwa wa wanawake katika masuala ya uchumi umekuwa chachu ya mafanikio kwa nchi zilizoendelea kama China. Wanawake wamekuwa kichocheo kikubwa cha kujibidisha katika kazi, nidhamu na uadilifu. Hata hivyo nchi yetu ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika ushiriki wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi. 

Nchi ya Tanzania katika mihimili yake miwili yaani Rais na Bunge inaongozwa na wanawake, jambo ambalo lilikuwa ni ndoto kubwa tangu kupatikana kwa uhuru. Kupitia uongozi huu, tunaona wanawake wengi wanaendelea kuaminiwa katika vyombo mbalimbali vya maamuzi na hivyo kusaidia kupunguza dhana kadamizi za wanawake, kadhalika na tunaona jinsi ambavyo bendera ya Tanzania inapeperushwa kimataifa katika nyanja mbalimbali hususan uchumi na hivyo kuthibitisha ile dhana ya kuwa wanawake wakipewa nafasi, hufanya mambo makubwa zaidi ya matarajio ya jamii.

Wazee (miaka 60 au 65 na zaidi). Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Wazee, Mzee ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka 60 na zaidi. Kadhalika, tafsiri ya kimataifa inaonyesha kuwa mzee ni mtu yeyote mwenye umri wa miaka 65 na na zaidi. Bila kujali tofauti ya tafsiri hizi, wazee ndiyo kundi linalotajwa kuwa na watu wachache zaidi nchini.

Takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya wazee nchini (miaka 60 na zaidi) kwa mwaka 2022 ni 3,491,983 sawa na asilimia 5.7 ya watanzania wote. Kadhalika wazee wenye umri wa miaka 65 na zaidi wanatajwa kuwa ni 2,340,908 sawa na asilimia 3.8 ya watu wote. 

Kwa kuzingatia wazee wenye umri wa miaka 65 na zaidi, uwiano wa kijinsia kwenye kundi hili unatajwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake kuliko wanaume. Takwimu zinaonyesha, idadi ya wanaume ni watu 1,031,531 sawa na asilimia 3.4 ya wanaume wote nchini na idadi ya wanawake ni watu 1,309,377 sawa na asilimia 4.1 ya wanawake wote nchini. 

Pamoja na idadi ya wanawake katika umri huu kuwa kubwa, takwimu zinaonyesha wanawake wamekuwa wakiongezeka katika vipindi vitatu mfululizo vya sensa ukilinganisha na wanaume ambao pamoja na kuwa na idadi ndogo, wamekuwa wakipungua. Takwimu zinaonyesha wanaume katika miaka ya 2002, 2012 na 2022 walikuwa ni asilimia 3.9, 3.7 na 3.4 wakati wanawake walikuwa asilimia 3.9, 4.0 na 4.1. 

Jicho langu linaangazia idadi ndogo ya wanaume katika kundi hili (wazee) kuwa inaweza kuchochewa na mitazamo hasi katika jamii. Jamii inaamini mwanaume kueleza au kuonyesha hisia zake hasa anapokuwa katika hali ya maumivu, ni udhaifu. Hali ambayo huwapelekea wanaume kuficha matatizo yao jambo ambalo linaweza kusababisha changamoto za kiafya na hata vifo. 

Wito wangu; jamii ibadili mtazamo kuhusu wanaume na elimu iendelee kutolewa kuhusu afya ya akili. Jamii inapaswa kufahamu kuwa mwanaume ana hisia sawa na mwanamke, hivyo ajengewe ujasiri wa kujieleza hasa anapokuwa katika changamoto. 

Uwiano wa kundi la Watu wenye Umri Tegemezi (Age-Dependency Ratio). Kundi hili ni uwiano kati ya watu wenye umri wa utegemezi (watu wote chini ya miaka 15 na umri wa miaka 65 na zaidi) kwa watu wote wenye umri wa kufanya kazi (miaka 15-64).

Kwa tafsiri nyingine, hii ni idadi ya wategemezi kwa watu wenye umri wa kufanya kazi. Takwimu zinataja uwiano wa kundi hili kuwa ni asilimia 87.1. Hii inamaana kwamba kuna wategemezi 87 kwa wasio wategemezi 100. Hata hivyo kiwango hiki kimekuwa kikipungua kutoka mwaka 2002 hadi sasa ambapo kwa mwaka 2002 uwiano kati ya wategemezi na wasio wategemezi ulikuwa ni asilimia 93.0, mwaka 2012 ulikuwa ni asilimia 91.5 na mwaka 2022 ulikuwa ni asilimia 87.1. 

Ongezeko la Watu Mijini. Idadi kubwa ya watanzania wanaishi vijijini kuliko mijini. Takwimu zinaonyesha idadi ya watanzania wanaoishi vijijini ni 40,201,425 sawa na asilimia 65.1 ya watanzania na idadi ya wanaoishi mijini ni 21,539,695 sawa na 34.9%. Hata hivyo, pamoja na uchache wa watu mijini ukilinganisha na vijijini, idadi yao inatajwa kuongezeka katika vipindi vitatu mfululizo vya sensa yaani 2002, 2012 na 2022, ambapo mwaka 2002 asilimia 23.1 ya watanzania wote walikuwa wanaishi mijini, mwaka 2012 asilimia 29.6 na mwaka 2022 asilimia 34.9. Ongezeko hili linatajwa kuwa ni kutokana na uhamiaji wa watu kutoka vijijini kwenda mijini pamoja na kutenga maeneo ya vijijini kuwa mijini. 

Wanawake wenye Umri wa Kuzaa (miaka 15-49). Kutokana na umuhimu wake katika uzalishaji uchumi pamoja na binadamu, Takwimu zimelitambua kundi hili na zinataja kuwa karibu nusu ya wanawake wote nchini, ni wanawake wenye umri huu. Takwimu zinataja kuwa, kundi hili lina watu 14,992,288 sawa na asilimia 47.3% ya wanawake wote nchini. Uwepo wa wanawake wengi katika kundi hili, ni fursa ya ongezeko la watu katika nchi ambao wakitumika ipasavyo wanaweza kuliletea taifa maendeleo katika uzalishaji uchumi. 

Jicho langu linaipongeza Serikali ya Awamu ya sita kwa kazi kubwa iliyoifanya katika kuhakikisha zoezi hili la Sensa linafanyika kwa weledi na umahiri mkubwa na hatimaye kuleta matokeo chanya kwa taifa. Naungana na Serikali kuiomba jamii itumie matokeo haya katika shughuli za kiuchumi na kijamii ili kuendelea kuweka mipango thabiti na utekelezaji wenye tija kwa maendeleo ya taifa. 
Share:

1 comment:

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com