Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Malietha Kasoga akitoa taarifa ya maendeleo ya kilimo na umwagiliaji. |
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda. akizungumza wakati wa uzinduzi huo. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba akihutubia wakati akifungua kongamano hilo la siku mbili. |
Na Dotto Mwaibale, Iramba
SERIKALI katika msimu wa kilimo wa 2022/2023 imeutengea Mkoa wa Singida mgawo wa mbegu bora za alizeti aina ya Certified 1 zenye ruzuku ya Serikali kilogram 500,000 zenye thamani ya Sh.2,500,000,000 ambapo bei kwa kilo moja sasa itakuwa ni Sh.5,000 badala ya Sh.8,000.
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba wakati akifungua
kongamano la uzinduzi wa msimu wa kilimo 2022/2023 katika Uwanja wa Ukumbi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Iramba Septemba 27,2022.
Alisema pia Serikali itatoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote
watakaojiandikisha kwenye mfumo maalum wa kupata ruzuku ambapo kwa sasa zoezi
la usajili linaendelea katika halmashauri zote saba za Mkoa wa Singida na kuwa bei ya mbolea yenye ruzuku iliyotangazwa na Serikali kwa mfuko wa kilo 50 kwa
mbolea ya UREA ni Sh.70,000 kutoka Sh.124,734, DAP Sh.70,000 kutoka Sh.131,
676, NPKs Sh.70,000 kutoka Sh.122, 695, CAN sH.60,000 kutoka Sh.108, 156 na
mbolea ya SA mfuko wa kilo 50 ni Sh.50,000 kutoka Sh.82,852.
Alisema Mkoa wa Singida kwa bajeti ya mwaka 2022/2023 umetengewa fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu
katika miradi ya umwagiliaji ya Halmashauri ya Wilaya ya Iramba.
Akizungumzia lengo la kongamano hilo alisema ni kuunga mkono na kutekeleza
kwa vitendo jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za kuinua na kuthamini mchango
wa kilimo hapa nchini.
"Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa moyo wa dhati ameongeza bajeti ya
kilimo kutoka Sh.294.1 Bilioni hadi Sh.751.1 Bilioni sawa na ongezeko la asilimia 155.34"
alisema Serukamba.
Akitoa taarifa ya maendeleo ya kilimo, umwagiliaji na ushirika Afisa Kilimo
wa Halmashauri ya Wilaya ya Iramba, Malietha Kasoga alisema kwa msimu wa
2022/2023 wilaya hiyo imepanga kutekeleza Agenda 10/30 ya kuwainua wakulima na
wafugaji kwa asilimia 10 hata kabla ya kufikia mwaka 2030 hiyo ni pamoja na
kutekeleza agizo la Rais la kuweka msukumo kwenye uzalishaji wa mazao ya
chakula na biashara yakiwemo mazao ya kimkakati ya alizeti, pamba na mtama
ili kukidhi mahitaji ya ndani na ziada kwa ajili ya soko la nje.
Mkuu wa Wilaya ya Iramba Suleiman Mwenda alisema changamoto kubwa ni soko
la mazao ya kilimo hasa zao la dengu ambapo hivi sasa bei yake kwa kilo ni
Sh.830 bei ambayo haina tija kwa mkulima.
Aidha Mwenda alisema wilaya hiyo imetenga Sh.8 Bilioni kwa ajili ya kutengeneza skimu za umwagiliaji ekari 6,000 katika eneo la Masimba.
0 comments:
Post a Comment