Adeladius Makwega-WUSM
Serikali imesema kuwa BMT na TFF wakae mara moja na kusimamia kufanyika uchaguzi wa chama cha mpira wa miguu kwa wanawake ili wanawake wajiongoze wenyewe katika michezo yao maana hadi sasa wapo chini ya TFF.
“Nina taarifa kuwa uchaguzi huo umeharibika wakiwa huko Tanga, mpaka leo TFF na BMT wamenyamaza kimya. Timu za mpira wa miguu za wasichana zinafanya vizuri na Rais Samia Suluhu Hassan amewapongeza sana, wenzetu wa chini ya miaka 17 tunawaombea kila la heri katika mechi yao ya kufuzu kombe la dunia, wenzetu wa Twiga Stars na timu zote za mpira wa miguu wa wasichana zinafanya vizuri.”
Hayo yemesemwa na Naibu Waziri Pauline Gekul Jijini Dodoma Mei 20, 2022 alipokuwa akifanya kikao na Chama cha Mpira wa Netibioli nchini CHANETA walipomtembelea ofisini kwake jijini Dodoma wakiongozwa na Mwenyekiti wao Dkt. Devota Marwa.
“Ninaliangiza hili mbele ya CHANETA kwa kuwa kuna wanawake wenzetu wanacheza vizuri sana lakini wapo chini ya TFF, wao pia wakamilishe safu kama CHANETA walivyofanya pia wale wasichana wanahitaji malezi yao japokuwa wanaucheza mpira wa miguu wanahitaji chama chao pia kiwe na uongozi uliokamilika.”
Alisisitza mheshimiwa Gekul katika kikao hicho huku akisema kuwa serikali haitokubali jambo hilo kukwama hata kidogo na serikali haiwezi kukaa kimya wakati mambo hayaendi.
Naibu waziri Gekul alihitimisha tamko na agizo hilo la serikali kwa kusema kuwa Tanzania ina vipaji vya michezo vingi shida ni yule anayevifuatilia na kuvifufua tu ikiwamo vyama vya michezo.
0 comments:
Post a Comment