METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, August 10, 2021

NAIBU WAZIRI MABULA ASIKITISHWA WAMILIKI KUTOLIPIA GHARAMA ZA UPIMAJI TABORA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi Hati ya ardhi Fatuma Ali Mohamed wakati wa kikao chake na watendaji wa sekta ya ardhi na viongozi wa halmashauri za mkoa wa Tabora akiwa katika ziara ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi Agosti 10, 2021. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Igunga Sauda Mtondolo.
 Sehemu ya watendaji wa sekta ya ardhi mkoa wa Tabora wakifuatilia maelekezo yanayotolewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya siku moja mkoani Tabora
Rehema Migilla mbunge wa Ulyankulu mkoani Tabora  akizungumza katika kikao baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na watendaji wa sekta ya ardhi mkoa wa Tabora 

Na Munir Shemweta, TABORA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesikitishwa na wamiliki wa ardhi mkoa wa Tabora waliopimiwa maeneo yao katika zoezi la urasmishaji makazi kushindwa kulipia gharama za upimaji kwa wakati na hivyo  kushindwa kumilikishwa maeneo.

Akizungumza na watendaji wa sekta pamoja na halmashauri za mkoa wa Tabora leo Agosti 10, 2021 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa mkoa – Mwana kiyungi, Dkt Mabula alisema, haileti maana serikali inaamua kurasimisha makazi lakini wananchi hawaoneshi mwamko jambo linalokwamisha mipango ya Wizara ya Ardhi katika kumilikisha ardhi wananchi.

Alisema, lengo la kuanzishwa zoezi la urasimishaji makazi holela ni kutaka kuwamilikisha wananchi makazi yao sambamba na kuwawezesha kiuchumi.

 ” Hatutaki kuwa na wananchi ambao wamepimiwa maeneo yao halafu kwa makusudi hawataki kulipia gharama za upimaji na kwa bahati nzuri Kamishna hapa Tabora amejitahidi kutoa elimu kwa wananchi” alisema Dkt Mabula.

Hata hivyo, Dkt Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri na manispaa za mkoa wa Tabora kuhakikisha wanarudi katika maeneo wanayoishi wananchi kwa lengo la kutoa elimu kuhusu faida na hasara za kumilikishwa ardhi.

Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Tabora Jabir Singano alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Mabula kuwa mkoa wa Tabora umefanya jitihada kubwa ili kukwamua kazi za urasimishaji makazi holela ambapo  tangu kuanzishwa ofisi yake idadi ya viwanja vilivyopimwa ni 12,875 na ankara ambazo wamiliki wake wamelipia ni  935 kati ya ankara 3747 zilizotolewa.

“Changamoto kubwa katika zoezi la urasimishaji makazi hapa Tabora ni muitikio mdogo wa wananchi katika kuchangia gharama za upimaji licha ya baadhi ya kampuni za upimaji kupima viwanja” alisema Singano.

Kwa upande wake Afisa Kodi wa Wizara ya Ardhi Rehema Kilonzi aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi mkoa wa Tabora kuhakikisha kujiwekea mikakati ya ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi pamoja na uingizaji viwanja katika mfumo badala ya kusubiri maekekezo kutoka makao makuu ya Wizara.

” Kila mkoa una mazingira yake hivyo mhamasishe wananchi katika maeneo yenu kulingana na misimu ya upatikanaji fedha, hiyo itarahisha upatikanaji pesa ya kodi ya ardhi” alisema Rehema.

Naye Afisa Tawala wa Wizara ya Ardhi Baraka Mraha aliwahimiza watumishi wa sekta ya ardhi Mkoa wa Tabora  kuzingatia sheria, taratibu na kanuni wakati wa utekelezaji majukumu yao na kuwaeleza kuwa wizara  haitasita kuchukua hatua kwa wale watakaokiuka taratibu.

Aidha, Mraha alihimiza watumishi wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Tabora kujaza OPPRAS kwa wakati na kwa  mujibu wa sheria ili kuthibitisha utendaji wao wa kazi.

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula yuko mkoani Tabora kwa ziara ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani humo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com