METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, August 27, 2021

KISHAPU YAJIPANGA KULETA MAPINDUZI MAKUBWA KWENYE MSIMU MPYA WA ZAO LA PAMBA 2021-2022




Mkuu wa wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga Joseph Modest Mkude amemuhakikishia balozi wa zao la Pamba nchini Aggrey Mwanri kwamba wilaya hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha msimu ujao wa kilimo cha zao hilo kwa kutumia mbinu bora na za kisasa wataleta mapinduzi makubwa.

Aidha Mkuu huyo aliipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa ubunifu wake katika kuonyesha jitihada kwenye uzalishaji wa zao hilo.

Mkuu huyo alisema hayo Agosti 23, 2021  wakati akizindua kampeni maalumu ya kuhamasisha ulimaji wa zao la pamba lenye tija kwa kutumia mbinu za Kisasa uliyofanyika wilayani humo ukiwashirikisha viongozi mbalimbali wa wilaya.

“Niipongeze sana Serikali yetu ya awamu ya sita huu ni ubunifu mkubwa sana kuteua balozi maalumu kwa ajili ya kushirikiana na viongozi wengine wa serikali kuhamasisha zao la pamba na isihishie tu kwenye pamba hata kwa mazao mengine ili kufika mbali kwenye kilimo chetu.” aliongeza

Alisema yeye  kama kiongozi wa  Serikali atahakikisha anashirikiana na wataalamu mbalimbali wa halmashauri wakiwemo maafisa kilimo wa wilaya, kata na vijiji kuhakikisha elimu iliyotolewa ya kanuni kumi za kilimo bora cha zao la pamba na inawafikia wananchi wote wa wilaya.

“Tumeshajipanga vizuri na tuna maafisa ugani kwa kila kata ntahakikisha wananipa taarifa zote za wakulima kuanzia kuandaa mashamba,  kupanda, kupalilia, kupulizia dawa mpaka kuvuna ili tuone matokeo ya mafunzo haya ya mbinu za kisasa za kilimo nbora cha zao la Pamba.

Kwa upande wao Madiwani wa Halmashauri wa wilaya ya Kishapu wameiahidi kamati ya uhamasishaji ya zao la Pamba kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu mbinu mpya kwani zinaonyesha itaongeza uzalishaji na hivyo kuongeza mapato ya Halmashauri na Mkoa kwa ujumla .

Akizungumza kwa niaba ya madiwani hao Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Willium Luhende Jijimya alisema kwamba ujumbe wa kamati ya uhamasishaji umefika mahali pake kwani madiwani ndiyo wenye wananchi hivyo kupitia wao ujumbe utawafikia wananchi wote katika kata zilizopo wilayani humo .

“ Mheshimiwa Mwanri hili limefika kwetu na litafanyika kwani kilimo ni sehemu ya shughuli zetu hivyo tutashirikiana bega kwa bega na timu yako na tunakuhakikishia hili litafanyika ili zao hili la pamba lilete tija kwenye Halmashauri yetu” alisema

“ Hawa Madiwani unaowaona hapa ni wakulima wazuri sana wa zao hilo, namshukuru sana Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya naahidi  tutatoa ushirikiano kwenu  ili Halmashauri yetu ipate mapato makubwa ya kuweza kuifanikisha Halmashauri yetu iende mbele zaidi” aliongeza

Nao baadhi ya wakulima wa zao hilo katika Halmashauri ya Kishapu waliishukuru sana Serikali kwa kuwaletea mafunzo hayo kwani ukulima waliokuwa wakiufanya awali licha ya kulima maeneo makubwa uzalishaji wa zao hilo ulikuwa mdogo ukikumbwa na changamoto mbalimbali zikiwemo wadudu, uchafu na mavuno hafifu.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake Joel Mora Bushele alisema kipimo walichokuwa wanatumia awali cha Sentimita 90 kwa sentimita 40 kilikuwa kikiwapatia miche 22,222 na kupitia kipimo kipya cha sentimita 60 kwa 30 kwa maelezo ya wataalamu kitaongeza tija kwa kuwapatia miche 44,444 na hivyo kuongeza uzalishaji na kipato.

“Mafunzo yaliyotolewa yameonyesha mwanga mkubwa sana katika zao hili, kwani ukiangalia vipimo tulivyokuwa  zamani kwenye upandaji wetu ulikuwa ukitupa miche michache sana, lakini pia tulikuwa hatuweki mbolea  wengine tulikuwa tunanyunyuzia dawa vibaya na hata wakati wa kupalilia tulikuwa tukiikata miche mingi kutokana na wingi wa miche iliyokuwa imesongana na hivyo kukosa nafasi ya kupitisha jembe. “alisema

Naye Mkulima mwingine wa zao hilo Jilala Petro Ndulu alisema hata wakati wa uvunaji walikuwa wakitumia mtindo wa Sombasomba,  ila kupitia mafunzo hayo wamejifunza namna bora ya uvunaji wa pamba na hivyo kuepusha kuchafua wakati wa kuvuna.

Julai 4, 2021 Bodi ya Pamba nchini Tanzania katika kuongeza tija ya uzalishaji wa zao hilo nchini walizindua Kampeni ya kuongeza tija katika zao hilo kwa kutumia mbinu mbalimbali za kisasa

Balozi wa zao hilo nchini Aggrey Mwanri alisema baada ya utafiti wa zao hilo kutoka nchi mbalimbali zinazolima zao waliamua kufanya mabadiliko kwenye vipimo, lakini pia waligundua kuna makosa mbalimbali yanayofanywa na wakulima na hivyo kuleta uzalishaji hafifu na usio na tija.

“Tuligundua baadhi ya wakulima hawaharibu masalio  shambani, hawapulizii vizuri dawa ya kuulia wadudu, hawapalilii vizuri, wengine wanachanganya mazao Zaidi ya mawili katika shamba moja, wengine baada ya kulima wanavuna vibaya na hivyo Pamba yetu inaonekana ni chafu dhidi ya mataifa mengine yanayolima zao hilo.” Alisema

“Kupitia mafunzo haya tumewaelekeza wakulima vipimo vipya, namna bora ya upuliziaji dawa za kuua wadudu, namna bora ya kurudishia udongo kwenye mashimo, namna na ya kupalilia, namna ya kuvuna na namna ya kutunza pamba.

“Tunaamini kama wakulima watazingatia tutarajie uzalishaji mkubwa wa zao hili katika nchi yetu na tunaamini itakuwa hivyo kwani utafiti haudanganyi” alimalizia kusema.

Timu ya uhamasishaji kilimo cha zao la Pamba kwa mbinu mpya za kisasa  iko wilayani Kishapu ikiendelea na utoaji wa mafunzo kwa lengo la kulima kilimo chenye tija na kuongeza thamani ya zao la Pamba maarufu kama dhahabu nyeupe katika kata na vijiji vilivyopo Wilayani humo.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com