Mkoa wa Katavi umejipanga kuzindua kitabu cha Uwekezaji “KATAVI INVESTIMENT GUIDE” utakaofanyika katika Ukumbi mpya wa Manispaa ya Mpanda tarehe 3 Machi 2020.
Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mhe Juma Homera amebainisha hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo tarehe 27 Machi 2020.
Amesema kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kitabu hicho anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa huku lengo la uzinduzi wa kitabu hicho ikiwa ni kuhakikisha serikali ya mkoa wa Katavi inakuwa na nyenzo muhimu ya kujenga uchumi.
Homera amesema kuwa kufuatia uzinduliwa kwa kitabu hicho wawekezaji na wadau mbalimbali watapata fursa ya kuzitambua fursa zilizopo katika mkoa wa Katavi na kuwawezesha wawekezaji katika nyanja mbalimbali itakazokuwa ni lango kuu la uchumi kusini magharibi mwa nchi.
Aidha, Rc Homera amesema kuwa kabla ya siku ya uzinduzi serikali ya mkoa itafanya ziara ya kutembelea sehemu za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutembelea hifadhi ya Taifa ya Katavi na mwambao wa ziwa Tanganyika ili kujionea vivutio na fursa za uwekezaji.
Ameongeza kuwa tukio la kutembelea vivutio litawafanya wawekezaji kutoka nje ya mkoa kupata fursa ya kukutana na wawekezaji wa ndani ili kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati ya pamoja ya kiuwekezaji.
Ameitaja kauli mbiu ya uzinduzi huo kuwa ni "Katavi Lango Kuu la Uchumi kusini Magharibi mwa Tanzania; Wekeza Katavi kwa Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda", ambapo kauli mbiu hiyo inalenga kuhamasisha wadau kuwekeza katika Mkoa wa Katavi sambamba na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania, DRC Congo, Burundi, Rwanda na Zambia.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment