METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, June 14, 2020

SERIKALI YAENDELEZA JUHUDI ZA KUFUFUA ZAO LA MKONGE NCHINI-MHE MGUMBA






Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba (Mb) akiwa katika ziara maalumu ya Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa mkoani Tanga tarehe 1 Juni, 2020 alimueleza waziri mkuu kuwa pamoja na mambo mengine Bodi ya Mkonge imeanza kuonyesha jitihada za kufufua zao la mkonge nchini ili kusaidia adhma ya serikali ya tano ya kuimarisha uchumi wa viwanda.
Dhumuni la ziara hiyo ilikuwa ni kutembelea na kukagua utekelezaji wa agizo lake kwa Bodi ya Mkonge alilolitoa mapema mwezi Machi, 2020 kuhusuufuatiliaji wa kufufua zao la mkonge na namna ya utekelezaji wa urejeshwaji wa mali ambazo zilitajwa kuwa zilizoporwa kinyume cha Utaratibu na Sheria.

Agizo hilo alilitoa baada ya kupokea taarifa ya Kamati Maalum aliyounda kwa ajili ya ufuatiliaji wa mali za Bodi ya Mkonge.Baadhi ya mali hizo ni majengo na mashamba ya Bodi ya Mkonge yaliyokuwa yamechukuliwa na wananchi kinyemela kwa maslahi yao ambapo baadhi yao kuweka Taasisi zao Binafsi huku Bodi hiyo ikiwa haina ofisi mkoani humo.Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu alizindua Jengo la Bodi ya Mkonge lililopo Jijini Tanga na alitembelea Taasisi ya utafiti ya Mlingano na kukagua vitalu vya zao hilo.

Mhe. Kassim Majaliwa (Mb.) pamoja na mambo mengine, alitoa maelekezo yafuatayo; kila mkoa unaolima zao la mkonge uhakikishe unawatambua wakulima wa mkonge na kuwasaidia ili kilimo hicho kiwe na tija na faida, wawekezaji wa zao la mkonge wa nje ya nchi wasaidiwe kuwekeza nchini, maafisa kilimo na ugani waende vijijini kuwasaidia wakulima wa mkonge kwa kuwapa mbinu bora za kilimo na endelevu ili kufufua kilimo cha zao hilo, wakulima wa mkonge wasisite kwenda kukopa kwenye mabenki kama vile benki ya kilimo ili kuweza kupata mitaji ya kulima mkonge.

Pia Bodi ya Mkonge ihakikishe inayatambua mashamba yake yote nchini na mashamba ambayo hayajaendelezwa yawekewe Mkakati wa kuyafufua pamoja kuwapatia wakulima wa mkonge baadhi ya mashamba hayo, Wizara ya Kilimo ihakikishe inatembelea maeneo yote nchini yaliyokuwa yanalima mkonge ili kuandaa Mkakati endelevu wa kufufua kilimo cha mkonge nchini.

Pia Bodi ya Mkonge izidi kujitangaza zaidi kupitia vyombo vya habari ili wananchi waitambue na kujua faida ya Bodi hiyo kwa wakulima wa mkonge nchini, wawekezaji wakubwa wa mkonge wahakikishe wanayaendeleza mashamba yao kwa angalau asilimia 10 (10%) kila mwaka na kama watashindwa kufanya hivyo watapokonywa mashamba hayo na mabenki ya biashara yapunguze riba ya mikopo nakuongeza muda wa urejeshaji wake (angalau miaka 3 hadi 4) kwa wakulima wa mkonge (special treatment) ili wakulima hao waweze kulima kwa tija na faida kwa maslahi mapana ya Sekta ndogo ya mkonge na Taifa kwa ujumla.

Ili kuhakikisha kilimo cha mkonge kinafufuliwa na kuimalika nchini, Mhe. Omary T. Mgumba (Mb.) alimjulisha Mhe. Waziri Mkuu kuwa, Wizara ya Kilimo kupita bodi ya Mkonge imeanza kufufua kilimo cha mkonge katika mikoa 12 nchini lakini kwa kuanza ufufuaji umeanza katika mikoa ya Tanga, Morogoro, Kilimanjaro na Pwani. Pia, wawekezaji katika Sekta ya Kilimo watapatiwa msaada wowote ule watakaohitaji katika uimalishaji wa kilimo cha mkonge nchini sanjari na kuisimamia ipasavyo Bodi ya Mkonge ili kuhakikisha inafikia malengo yake.

“Mkakati wa Wizara ya Kilimo ni kuongeza uzalishaji wa mkonge kutoka tani 30,000 zinazozalishwa sasa hadi kufikia tani 120,000 ifikapo mwaka 2024/25. Uzalishaji huo utarudisha heshima ya nchi yetu katika uzalishaji wa mkonge kama ilivyokuwa katika miaka ya 1960”, alisema Mhe. Mgumba.

Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com