METDO Tanzania

METDO Tanzania

Sunday, May 17, 2020

NAIBU WAZIRI MGUMBA AWAPONGEZA WATAFITI KWA UZALISHAJI WA MBEGU BORA

 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akimsikiliza Mkuu wa Kituo cha Utafiti TARI Hombolo Dkt. Lameck Makoye ndani ya shamba la kuzalisha mbegu bora za mtama lenye ukubwa wa hekta 20
 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akiangalia shamba la kuzalisha mbegu za uwele katika ziara yake ya kujionea shughuli za uzalishaji wa mbegu katika Kituo cha TARI Hombolo
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba akiangalia suke la ulezi kwenye shamba la kuzalisha mbegu bora katika ziara yake ya kujionea shughuli za uzalishaji wa mbegu katika Kituo cha TARI Hombolo

Na Issa Sabuni, Wizara ya Kilimo-Dodoma

Naibu Waziri Kilimo Mhe. Omary Mgumba amewapongeza Watafiti wa Kituo cha Utafiti Hombolo (TARI – Hombolo) kwa kuanza kutekeleza kwa vitendo agizo la kuongeza uzalishaji wa ndani wa mbegu bora za mazao ya jamii ya nafaka zinazovumilia mvua kidogo kama ulezi, uwele na mtama.

Naibu Waziri Mgumba ameyasema hayo mapema leo tarehe 17 Mei, 2020 mara baada ya kutembelea Kituo cha Utafiti Hombolo ili kujionea maendeleo ya utafiti wa mazao ya kilimo pamoja na ufikishaji wa teknolojia mbalimbali zilizogunduliwa na Watafiti kwenda kwa Wakulima.

Mhe. Mgumba amesema amefurahi kuona TARI Hombolo imeanza kutekeleza lengo la Serikali la kujitosheleza kwa mbegu bora na kupunguza uagizaji wa mbegu bora kutoka nje ya nchi.

Mhe. Mgumba amesema katika kipindi hiki cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano upatikanaji wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 36,614 mwaka 2015/2016 hadi tani 76,725 mwaka 2019/2020 sawa na ongezeko la asilimia 110.

“Uzalishaji wa ndani wa mbegu bora, umeongezeka kutoka tani 20,604 mwaka 2015/2016 hadi tani 69,173 mwaka 2019/2020. Uzalishaji huo umepunguza uagizaji wa mbegu bora kutoka nje ya nchi kutoka tani 16,009 mwaka 2015/2016 hadi tani 7,552 mwaka 2019/2020 sawa na punguzo la asilimia 53. Amekaririwa Mhe. Naibu Waziri Mgumba.

Naye Mkuu wa Kituo cha TARI Hombolo Dkt. Lameck Makoye amesema malengo makuu ya Kituo hicho ni kufanya utafiti, kusambaza teknolojia kwa njia mbalimbali na kuzalisha mbegu za mazao yanayovulia mvua za wastani kama ulezi, uwele na mtama.

Dkt. Makoye ameongeza kuwa Kituo cha TARI Hombolo kwa kushirikiana na Taasisi ya ICRISAT wamefanikiwa kufanya utafit za zao la mtama na kupata mbegu bora ‘Hybrid’ 36.

Aidha TARI Hombolo kwa kushirikina na Kampuni ya Advantha Seed International imefanikiwa kufanya utafiti kwa mazao ya ulezi, uwele na mtama maalum kwa ajili ya malisho ya mifugo kama ng’ombe, mbuzi na kondoo na kuja na mbegu bora kama Sugar Graze, Mega Sweet, BMR Rocket, Jumbo Rocket na Nutrified.

Naibu Waziri Mgumba ameagiza pia kwa Taasisi hiyo kuendelea kujikita katika Miradi mikubwa ambayo italeta tija kwa Taasisi; Ukiwemo Mradi wa kuzalisha mbegu za mtama aina ya MACIA ambayo inasoko kubwa kwa ajili ya kutengeneza ‘beer’ aina ya IGO ambapo Wakulima wengi wamepata soko la uhakika kutoka Kiwanda cha Bia cha TBL.

Watumishi wa TARI Hombolo wamemueleza Naibu Waziri Mgumba kuwa kuna changamoto kadhaa ambazo zinahitaji utatuzi ili Taasisi ijiendeshe kwa tija, moja ya chamaoto hizo ni majengo kwa ajili ya kuhifadhi mbegu bora, eneo kubwa la kuzalishia mbegu, maeneo ya kilimo ya Kituo kuvamiwa pamoja na vitendea kazi kama matrekta madogo na makubwa ajili ya kulima eneo kubwa na kuvuna kwa kutumia zana bora.

Naibu Waziri Mgumba aliahidi kushughulikia changamoto zote hizo kwa kushirikiana na Viongozi wengine wa Wizara ya Kilimo.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com