METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, February 27, 2020

WAFANYABIASHARA 1,950 WAPATIWA ELIMU YA KODI MKOANI IRINGA

Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakiwaelimisha wauzaji wa duka la vileo wa Mkoa wa Iringa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mkoani humo leo.
 Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Jamhuri David William (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Maafisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakati walipoingia wilayani humo kwa ajili ya kufanya kampeni ya elimu kwa mlipakodi. Wa nne kulia ni Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kusini Mhe. Mendrad Kigola na wa tatu kulia ni Meneja wa TRA Wilaya ya Mufindi Bw. Ernest Kagali.
 Afisa Msimamizi wa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Chama Siriwa akifurahia jambo na mfanyabiashara wa Mkoa wa Iringa alipokuwa akimuelimisha kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mkoani humo leo.
Jumla ya wafanyabiashara 1,950 wa Mkoa wa Iringa wamefikiwa na kupatiwa elimu ya kodi wakati wakampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyofanyika kuanzia tarehe 17 hadi 27 Februari,2020. 

Kampeni hiyo iliyoandaliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kuwafikia na kuwaelimisha baadhi ya wafanyabiashara wa Wilaya za Kilolo, Manispaa ya Iringa na Mufindi. 

Akizungumza mara baada ya kuhitimisha kampeni hiyo mkoani humo, Afisa Msimamizi wa Kodi Mwandamizi wa TRA Bi. Catherine Mwakilagala amesema kuwa, zoezi hilo limekuwa na mafanikio makubwa kwani wamefanikiwa kuwaelimisha jumla ya walipakodi 1,950. 

“Mamlaka ya Mapato Tanzania tumehitimisha kampeni ya elimu kwa mlipakodi katika mkoa huu wa Iringa na zoezi hili limekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu tumeweza kuwafikia jumla ya walipakodi 1,950 ambao wote tumewapatia elimu ya kodi na wamepata nafasi ya kutoa maoni na changamoto zao ambazo tumezipokea na nyingine tumezipatia ufumbuzi,” alisema Bi. Mwakilagala.

Kwa upande wake Meneja wa TRA mkoani humo Bw. Lamson Tulyanje ametoa wito kwa wafanyabiashara wote waliotembelewa na maafisa wa TRA kwenye maduka yao na wale waliopata elimu kupitia semina wakati wa kampeni hiyo, kutumia elimu walioipata kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati na hiari.

“Elimu ambayo wameipata wafanyabishara mbalimbali kwenye kampeni hii ya elimu kwa mlipakodi, ni vizuri waitumie katika kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa wakati ili Serikali iweze kutimiza majukumu yake ya kuwapatia huduma mbalimbali wananchi,” alieleza Bw. Tulyanje.

Bw. Richard Kilawa ni mfanyabiashara wa duka la vifaa vya ujenzi kutoka Halmashauri ya Mji wa Mafinga mkoani humo ambaye ameishukuru TRA kwa kumfikishia elimu ya kodi dukani kwake na ameahidi kuendelea kulipa kodi kwa hiari.

“Ninashukuru sana TRA kunitembelea dukani kwangu na elimu yao imenifundisha kulipa kodi kwa hiari. Hivyo, nitawashawishi wafanyabiashara wenzangu walipe kodi kwa hiari ili tujenge nchi yetu,” alisema Bw. Kilawa.  

Naye, mfanyabiashara wa mbao wa Halmashauri hiyo, Bi. Maura Ng’umbi amesema kuwa, kupitia elimu iliyotolewa na maafisa wa TRA wakati wa kampeni ya elimu kwa mlipakodi, imewasaidia kujua umuhimu wa kulipa kodi stahiki kwa manufaa ya Taifa.

Kampeni ya elimu kwa mlipakodi iliyomalizika mkoani Iringa ni mwendelezo wa kampeni zilizofanyika katika Mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam kwa lengo la kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu masuala mbalimbali ya kikodi, kupokea maoni na mapendekezo yao pamoja na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com