Muonekano wa moja ya mabasi yaliyoundwa na Kampuni ya BM Motors iliyopo Kibaha mkoani Pwani kama linavyoonekana likiwa tayari kuanza kutumika
Kampuni ya BM Motors iliyopo Kibaha mkoani Pwani, imeingia kwenye orodha ya kampuni zinazounda na kutengeneza mabasi ya abiria hapa nchini.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw. Jonas Nyagawa amesema, karakana hiyo iliyojengwa eneo la Zegereni katika Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani inatengeneza mabasi yenye uwezo wa kubeba abiria kati ya 45 hadi 57.
Akiongea na Maafisa Habari kutoka Idara ya Habari – MAELEZO, amesema, kutoka na na msukumo wa mazingira wezeshi ya Serikali katika kuunga mkono Sera ya viwanda nchini, ameweza kufanikisha ndoto yake ya kuanzisha karakana hiyo miezi sita iliyopita.
Amesema, ni fursa pekee katika kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inahamasisha Wananchi kuanzisha viwanda nchini ili kujenga uchumi wa nchi na kuongeza ajira kwa vijana.
“Serikali imekuwa ikisisitiza uanzishaji wa viwanda ili nchi yetu ifikie uchumi wa kati na Wananchi waweze kuwa na kipato cha kati. Ili kufikia azma hiyo lazima kujengwe viwanda vingi na wananchi nao wapate ajira.”
Bwana Nyagawa amesema, vifaa vinavyotumika kuunda mabasi hayo vinatoka sehemu mbalimbali, huku asilimia 55 vikitoka nje ya nchi.
Tangu karakana hiyo ianze kufanya kazi tayari mabasi mawili yameshaundwa na yako katika hatua za mwisho za usajili ili kuanza kufanya kazi.
“Kila kitu kinawezekana, Watanzania wanapaswa kuwa na uthubutu. Karakana hii inaunda mabasi na sio kwamba vifaa vyote vinatoka nje ya nchi, vingine vinapatikana hapa hapa nchini.” Amesema.
Kufuatia uanzishwaji wa kampuni hiyo, hadi sasa imetoa ajira kwa Watanzania 15 huku baadhi yao wakiongeza ujuzi kutoka kwa Wataalamu wa nje ya nchi wanaofanya kazi na kampuni hiyo.
Frank Ngewe ambaye ni fundi mkuu wa karakana hiyo amesema, ujenzi wa karakana hiyo umekuwa mkombozi mkubwa kwa vijana hususani wale waliopata mafunzo ya uchomeleaji vyuma, umeme, rangi n.k.
“Kwanza tunamshukuru Rais wetu na Serikali kwa ujumla kwa kukazania Sera ya Tanzania ya Viwanda. Watanzania wengi hususan vijana hivi sasa wanapata ajira na kujikwamua kimaisha kutokana na kuanzishwa kwa viwanda nchini. ”Amefafanua zaidi Bw. Ngewe.
Kwa upande wake Elibariki Maleshe ambaye ni fundi bodi wa mabasi katika karakana hiyo ameeleza kwamba, vijana wanapaswa kuchangamkia fursa za viwanda ili kupata uzoefu na kujifunza zaidi vitu vipya.
''Vijana hasa wanaomaliza masomo ya ufundi wanapaswa kujikita kwenye masuala ya viwanda ili watakapomaliza masomo yao waweze kupata ajira kwenye viwanda vipya vinavyoanzishwa nchini.''
Wakati karakana hiyo ikiwa na miezi sita tu tangu ianze kufanya kazi ya kuunda mabasi, eneo hilo la Zegereni limetengewa zaidi ya ekari elfu moja kwa ajili ya viwanda vinavyojihusisha na shughuli mbalimbali ikiwa ni kuiishi Sera ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda.
0 comments:
Post a Comment