METDO Tanzania

METDO Tanzania

Friday, January 17, 2020

TBS YATEKETEZA BIDHAA ZENYE THAMANI YA MIL10 KWA KUKOSA UBORA

Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati wa Shirika la Viwango Tanzania, Bi. Salome Emmanuel, akiwaonesha waandishi wa habari bidhaa zisizokidhi viwango na kuisha muda wake wa matumizi  wakati wa zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo lililofanyika leo Januari 16, 2020 katika dampo la Chidaya  Jijini Dodoma.
Sehemu ya bidhaa zilizokamatwa kwenye zoezi la kubaini  bidhaa zilizoisha muda wa matumizi zikiwa tayari kuteketezwa leo Januari 16, 2020 katika Dampo la Chidaya Jijini Dodoma. Oparesheni hiyo imefanikiwa kukamata bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni kumi.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa zenye thamani ya shilingi milioni 10 kwa kukosa kukidhi ubora.

Akizungumza wakati wa zoezi la uteketezaji wa bidhaa hizo zikiwemo vipodozi, vyakula na vinywaji, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Kati ya Shirika hilo Bi. Salome Emmanuel amesema kuwa baadhi ya bidhaa zilizoteketezwa ni zile ambazo muda wake wa matumizi umekwisha na bado wafanyabiashara wasio waadilifu walikuwa wakiendelea kuziuza.

“Ukaguzi tuliofanya kati ya mwezi Oktoba na Desemba 2019 katika mikoa ya Dodoma na Singida umetuwezesha kubaini bidhaa hizi ambazo baadhi ya bidhaa zizisokidhi viwango na nyingine muda wake wa matumizi umekwisha lakini bado wafanyabiashara  wasio waaminifu wamekuwa wakiendelea kuziuza” alisisitiza Bi. Solome

Akifafanua Bi. Solome amesema kuwa Shirika hilo litaendelea kufanya ukaguzi mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa bidhaa zilizopo sokoni zinakidhi vigezo kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa wananchi wana jukumu la kushirikiana na shirika hilo katika kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wasio waadilifu hawafanikiwi kuuza bidhaa ambazo muda wake umekwisha na ambazo hazikidhi vigezo.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara wote kuzingatia sheria na kanuni pale wanapotaka kuingiza bidhaa hapa nchini na hata wale wanaofanya uzalishaji hapa nchini.
Kwa upande wake mkaguzi wa Chakula wa Shirika hilo Bw. Abel Deule amesema kuwa  Shirika hilo linaendelea kuhakikisha kuwa wananchi wanalindwa dhidi ya bidhaa zisizo na ubora na zile ambazo muda wake wa matumizi.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa likifanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi vigezo .
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com