Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo akitia saini kitabu cha
wageni mara baada ya kufika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu kabla
ya kukagua kazi ya usambazaji umeme mkoani humo. Kulia ni Katibu Tawala
Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini na kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya REA,
Dkt. Andrew Komba
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo (wa tatu kulia) akikagua
kazi ya usambazaji umeme katika Kijiji cha Sesele wilayani Bariadi. Wa
Pili kulia ni Mjumbe wa Bodi ya REA, Dkt. Andrew Komba na wa Pili
kushoto ni Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Rehema Mashinji.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo (wa tatu kulia)
akizungumza na vibarua wanaofanya kazi ya kusambaza umeme katika Kijiji
cha Mwasubuya wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu. Wa Pili kulia ni Mjumbe
wa Bodi ya REA, Dkt. Andrew Komba na wa kwanza kulia ni Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Amos Maganga.
Kazi ya usimikaji nguzo ikifanyika
katika Kijiji cha Mwasubuya wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu kupitia
mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa kwanza
(REA III).
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Wakili Julius Kalolo (wa tatu kushoto) akipata
maelezo kuhusu kazi ya usambazaji umeme vijijini mkoani Simiyu. Anayetoa
maelezo ni Mkurugenzi wa kampuni inayosambaza umeme mkoani Simiyu,
Whitecity Guangdong JV, Nuhu Mringo (wa kwanza kulia). Wa Pili kulia ni
Mjumbe wa Bodi ya REA, Dkt. Andrew Komba.
Kazi ya usambazaji umeme
ikifanyika katika Kijiji cha Sesele wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu
kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, mzunguko wa
kwanza (REA III).
……………….
Na Teresia Mhagama, Simiyu
Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini
(REA) imempa siku 14 mkandarasi wa umeme vijijini mkoani Simiyu
kuongeza kasi ya usambazaji umeme katika vijiji alivyopangiwa la sivyo
Bodi hiyo haitasita kuchukua hatua mbalimbali za kimkataba ikiwemo ya
kusitisha mkataba.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Wakili
Julius Kalolo alisema hayo tarehe 16 Novemba, 2019 wilayani Busega
mkoani Simiyu mara baada ya kukagua kazi ya usambazaji umeme katika
Vijiji mbalimbali vya wilaya ya Bariadi na Busega akiwa amembatana na
Mjumbe wa Bodi hiyo, Dkt Andrew Komba na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa REA,
Mhandisi Amos Maganga.
” Bodi haijaridhishwa na kasi ya
mkandarasi huyu kwani amepewa kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 152
vya Mkoa wa Simiyu lakini mpaka sasa amesambaza katika vijiji 54 ambayo
ni takribani asilimia 30 tu ya kazi anayopaswa kufanya hivyo tumempa
siku 14 aonyeshe mabadiliko la sivyo tutachukua hatua.” Alisema
Wakili Kalolo alieleza kuwa,
Serikali imetimiza jukumu la kutoa malipo kwa mkandarasi huyo ili kazi
ya usambazaji umeme ifanyike kwa kasi hivyo visingizio vya ucheleweshaji
wa kazi havikubaliki kwani kwa mujibu wa mkataba wa mkandarasi huyo
anapaswa kumaliza kazi mwezi Aprili mwaka 2020.
Aidha, alimwagiza mkandarasi huyo
kampuni ya Whitecity Guangdong JV, kuwasilisha mpango kazi wake kwa Bodi
hiyo, Mameneja wa TANESCO mkoani Simiyu pamoja Ofisi ya Katibu Tawala
Mkoa wa Simiyu ili kuweza kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa kazi
anazofanya.
Awali Bodi hiyo ilikutana na
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini ambapo, Mjumbe wa Bodi
ya REA, Dkt. Andrew Komba alitoa shukrani kwa viongozi wa mkoa wa Simiyu
kwa kufuatilia utekelezaji wa kazi ya usambazaji umeme vijijini.
Aidha, aliomba kasi hiyo iongezeke
ili Mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu, Mzunguko wa
Kwanza (REA III) ukamilike kwa wakati.
Alisema kuwa, msukumo wa
kuwafuatilia wakandarasi unahitajika ili kutimiza lengo la Serikali la
kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyopo katika mpango wa REA III
mzunguko wa kwanza ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
Aidha alitoa wito kwa viongozi wa
Serikali katika ngazi mbalimbali za mkoa, kuhamasisha wananchi kujiunga
na huduma ya umeme kwani Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika
kuwasambazia umeme wananchi hivyo wanapaswa kuunganisha umeme kwa wingi
na kuutumia katika shughuli za kiuchumi na kijamii
0 comments:
Post a Comment