Na Ismail Ngayonga,MAELEZO
DAR ES SALAAM
RIPOTI ya Shirika la
Kilimo Duniani (FAO) inasema mahitaji
ya bidhaa za kilimo yanatarajiwa kukua kwa asilimia 15 katika kipindi cha
muongo mmoja ujao huku, ukuaji wa uzalishaji wa bidhaa za kilimo ukitarajiwa
kuongezeka kwa kasi zaidi na kusababisha mfumuko wa bei.
Aidha ripoti hiyo iliyotolewa mwezi
Julai mwaka huu inatoa utafiti unaolenga mwelekeo wa miaka kumi ijayo katika
soko la bidhaa za kilimo na samaki katika viwango vya kitaifa, kikanda na
kimataifa.
Katika ripoti hiyo
inaelezwa kuwa miongoni mwa changamoto kubwa inayowakabili wakulima katika
Mataifa yanayoendelea ikiwemo Tanzania ni pamoja na ukosefu wa masoko ya mazao
yao ndani na nje ya nchi.
Changamoto hiyo
imekuwa ikiwakwaza sana wakulima katika miaka ya nyuma wakulima kiasi cha
baadhi ya wakulima wa baadhi ya mazao kadhaa kuamua kuachana kabisa na
uzalishaji wa mazao husika ikiwemo zao la kahawa na korosho.
Changamoto za
wakulima kukosa masoko haziwaathiri wakulima pekee, bali hata serikali hivyo ni
suala linalogusa pande zote, kwa sababu serikali nayo inategemea kupata mapato
kutokana na usafirishaji wa mazao nje.
Hata hivyo, matumaini
yameanza kuonekana kutokana na hatua kadhaa ambazo zinachukuliwa na Serikali ya
Awamu ya Tano katika kuboresha sekta ya kilimo ikiwemo kuhimiza uongezaji wa
thamani ya mazao na kuweka bei elekezi ya mazao, ambayo inampa motisha mkulima.
Akiwasilisha Hotuba
ya Makadirio ya Bajeti ya Mapato na Matumizi kwa mwaka 2019/2020, Waziri wa
Kilimo, Japhet Hasunga anasema Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na
Biashara imeendelea kutekeleza mipango na mikakati ya kupata masoko na kuongeza
thamani ya mazao ya kilimo.
Waziri Hasunga
anasema Ili kuongeza juhudi zaidi za utafutaji wa masoko ya mazao ya kilimo,
Wizara katika mwaka 2018/2019, imeanzisha kitengo cha masoko ya mazao ya kilimo
ambacho kitahusika na kutafuta masoko ndani na nje ya nchi na kufanya utafiti
na uchambuzi wa kina wa mahitaji ya mazao na bidhaa za kilimo.
“Wizara pia
iliboresha mifumo ya masoko ya mazao ya kimkakati kwa kufanya utafiti wa
mahitaji ya masoko na kuimarisha vyama vya ushirika, kusimamia mikataba baina
ya wanunuzi na wakulima” anasema Waziri Hasunga.
Anaongeza kuwa matokeo
ya awali ya utekelezaji ya mifumo hiyo, yameonesha kuwepo kwa tija kwa mkulima,
bei nzuri, takwimu na ubora wa mazao, ambapo bei kwa mazao ya kahawa, korosho
na kakao kwa soko la ndani ziliimarika ikilinganishwa na masoko ya nje.
Akitolea mfano
Hasunga anasema bei ya kahawa ya Arabika katika soko la dunia ilikuwa ni Dola
za Marekani 107.04 ikilinganishwa na Dola 112 katika soko la ndani kwa gunia la
kilo 50, bei ya kahawa ya Robusta katika soko la dunia ilikuwa Dola 73.90
ikilinganishwa na Dola 87.13 katika soko la ndani kwa gunia la kilo 50.
Akifafanua zaidi
anasema Serikali pia imeendelea kutafuta masoko ya zao la muhogo ikiwemo
kuingia Makubalino ya Itifaki ya Usafi baina ya Tanzania na Serikali ya China
kuwezesha kuuza zao hilo nchini China.
“Hadi mwezi Machi
2019, kampuni tano za Dar Canton Investment, Jielong Holdings (T) Company,
EPOCH Agriculture Development, Gelimesha Company na Tanzania Export Processing
Zone (TAEPZ) zimesajiliwa kwa ajili ya kuuza muhogo nchini China” anasema
Waziri Hasunga.
Hasunga anasema katika
mwaka 2018/ 2019, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ilipanga kununua tani
14,000 za mahindi na tani 6,000 za mbegu za alizeti, ambapo hadi kufikia Machi
2019, Bodi imenunua mahindi tani 7,230 na alizeti tani 621 na kusaga tani
1,003.0 za mahindi ambazo zimetoa tani 802.4 za unga wa mahindi na tani 208.9
za pumba.
Kwa mujibu wa Hasunga
anasema Tani 1,003.0 za unga wa mahindi zenye thamani ya Shilingi 561,680,000
na tani 208.9 za pumba zenye thamani ya Shilingi 45,570,000 ziliuzwa katika
mikoa ya Iringa, Mwanza, Dodoma na Dar es Salaam.
Waziri Hasunga
anasema ili kujiimarisha zaidi, Bodi imefunga mashine za kukamua mafuta ya
alizeti na kusaga mahindi katika eneo la Kizota Jijini Dodoma hadi Machi, 2019
ufungaji wa mashine za kusaga mahindi umefikia asilimia 90 na alizeti asilimia
65.
Mkakati wa Serikali
wa kuimarisha masoko ya mazao ni muhimu na wenye tija kwa sababu unalenga
kuwatafutia wakulima ufumbuzi wa kero yao ya muda mrefu ya masoko, ambayo pia
imekuwa ikisababisha serikali isinufaike zaidi na pato
Aidha masoko ya mazao
pia yatasaidia kuchochea kasi ya ukuaji wa viwanda ambavyo Tanzania imepania
kuvijenga katika wakati huu wa kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
0 comments:
Post a Comment