Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi waliyohudhuria
katika uzinduzi wa daftari la kudumu la wapiga kura, uliyofanyika
kwenye viwanja vya Mandela mkoani Kilimanjaro Julai 18.2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akibonyeza kitufe,
wakati akizindua zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga
kura, katika viwanja vya Mandela mkoani Kilimanjaro Julai
18.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiketa jambo
na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles Kaijage,
kabla ya uzinduzi wa daftari la kudumu la wapiga kura, uliyofanyika
kwenye viwanja vya Mandela mkoani Kilimanjaro Julai 18.2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
****************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amezindua rasmi zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
na kuwahimiza vijana waliotimiza miaka 18 wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha.
“Nitoe rai kwa vijana wote wa
Kitanzania waliotimiza umri wa miaka 18 au wale ambao watatimiza umri
huo ifikapo Oktoba, 2020 wajitokeze kwa wingi na kujiandikisha katika
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hawa ndio walengwa wakuu kwa sababu
wanaingia kwa mara ya kwanza katika uchaguzi.”
“Ikumbukwe kwamba, bila
kujiandikisha hawataweza kutumia haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi
wanaowataka. Hivyo, kujiandikisha kwao kutawahakikishia ushiriki wao
katika uchaguzi wa viongozi,” amesema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu ametoa rai hiyo leo,
(Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizindua zoezi la uboreshaji wa
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililofanyika kwenye uwanja wa Mandela,
Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkuu ambaye amewasili
mkoani Kilimanjaro leo asubuhi kwa ziara ya kikazi za siku nne, ametumia
fursa hiyo kuwasisitiza vijana na wale wanaorekebisha taarifa zao
kwamba hakuna mtu atakayeruhusiwa kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2020 kama hajajiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura
ama hana kadi ya mpigakura.
Amesema zoezi hilo ambalo limeanza
leo, linafanyika kwa mara ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu
wa mwaka 2015. Amesema litafanyika nchi nzima na linatarajiwa kukamilika
Machi, 2020.
“Watakaohusika awamu hii ni
wapigakura waliotimiza miaka 18 hivi karibuni, wale watakaotimiza miaka
18 wakati wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 2020, waliohama kata au Jimbo na
kuhamia maeneo mengine ya kiuchaguzi, waliopoteza kadi au kadi zao
kuharibika, wanaohitaji kurekebisha taarifa zao mfano majina ambayo hapo
awali yalikuwa yamekosewa sambamba na kuwaondoa wapiga kura waliopoteza
sifa kama vile kufariki,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
ameziasa asasi za kiraia ambazo zimepewa vibali vya kutoa elimu ya
mpigakura, zijiepushe na ushabiki wa kisiasa na badala yake zizingatie
mwongozo wa elimu ya mpigakura uliotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Nimeambiwa, Tume imetoa vibali
vya kutoa elimu ya mpigakura kwa baadhi ya Asasi za Kiraia. Rai yangu
kwa asasi zilizopata vibali hivyo ni kuendelea kutoa elimu hiyo kwa
wananchi kwa kuzingatia mwongozo wa uliotolewa na Tume ya Taifa ya
Uchaguzi. Niendelee kuwaasa pia kutohusisha ushabiki na mijadala ya
kisiasa muda wote mtakapokuwa mkitoa elimu hiyo,” amesema.
Amesema ana imani kuwa wananchi
wakipata elimu kuhusu uboreshaji kama inavyoendelea kutolewa, basi
watahamasika kutumia haki yao ya kikatiba ya kujiandikisha katika
daftari hilo na hatimaye kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Amesema zoezi la majaribio ya
uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika Kata ya Kibuta
katika Halmshauri ya Wilaya ya Kisarawe na Kata ya Kihonda katika
Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Morogoro, lilifanyika kwa mafanikio
makubwa.
Mapema, akitoa maelezo kuhusu
zoezi hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Semistocles
Kaijage, alisema katika zoezi la sasa, Tume itaendelea kutumia
teknolojia ya kielektroniki ya Biometric (BVR) na imeandaa BVR kits 3,000.
Alisema kwa Tanzania Bara, Tume
hiyo imeongeza vituo vya uandikishaji kutoka 36,549 vilivyotumika mwaka
2015 hadi kufikia 37,407; kutokana na zoezi la uhakiki wa vituo vya
kuandikisha wapiga kura lililoendeshwa mwaka jana.
“Kutokana na hilo, vituo 6,208
vilibadilishwa majina, vituo 817 vimehamishwa kutoka mtaa mmoja au
kijiji kimoja na kwenda kingine na vituo 19 vilihamishwa kutoka kata
moja kwenda kata nyingine.”
“Kwa upande wa Zanzibar, vituo vya
uandikishaji vimeongezeka kutoka 380 na kufikia 407. Kwa sasa kila
kijiji au mtaa, utakuwa na kituo kimoja,” alisema.
Alisema vituo vya uandikishaji
vitafunguliwa saa 2 asubuhi hadi saa 12 jioni na zoezi la uboreshaji
litafanyika kwa siku saba kwa kila kituo cha kujiandikisha iwe ni
Tanzania Bara au Zanzibar.
0 comments:
Post a Comment