Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggey
Mwandri baada ya kuwasili katika chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya
Urambo.Kulia ni Mbunge wa Urambo Mashariki Mhe. Magreth Sitta
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa chuo
cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo.Wa kwanza kulia ni Mbunge wa
Urambo Mashariki Mhe.Magreth Sitta akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Tabora
Aggrey Mwandri na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya VETA Peter Maduki
akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt. Pancras Bujulu.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akivuta utepe kuzindua chuo cha Ufundi Stadi cha
Wilaya ya Urambo.Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwandri.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya
VETA Peter Maduki wakati wa uzinduzi wa chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya
ya Urambo.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akizungumza na wananchi waliojitokeza kuhudhuria
uzinduzi wa chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo.
Mbunge wa Urambo Mashariki Mhe. Magreth
Sitta akifurahi pamoja na baadhi ya wananchi waliofika kushuhudia
uzinduzi wa chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo ya vifaa mbalimbali vya
kufundishia fani ya Umeme kutoka kwa Mwalimu wa Chuo cha VETA Urambo Ali
Musa alipotembelea karakana za chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako akipata maelezo juu ya vyerehani vya kufundishia
fani ya Ushonaji kutoka kwa Mwalimu wa fani hiyo katika Chuo cha VETA
Urambo Aines Sanduli alipotembelea karakana za chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia
Prof. Joyce Ndalichako katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali
waliohudhuria uzinduzi wa chuo cha VETA Urambo.
Jengo la utawala la Chuo cha VETA Urambo.
…………………….
Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi
na Teknolojia imetenga Sh. bilioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo 25
vya Ufundi Stadi katika Wilaya mbalimbali nchini.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa
Chuo cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo tarehe 9 Julai 2019, Prof.
Joyce Ndalichako, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia amesema ujenzi
wa vyuo hivyo ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa kuhakikisha
vijana wengi zaidi wanapata fursa za mafunzo ya Ufundi Stadi.
Prof. Ndalichako amesema vyuo hivyo
vinatarajiwa kujengwa katika Wilaya za Chunya, Kilindi, Korogwe,
Ukerewe, Igunga, Pangani, Kishapu, Rufiji, Uyui, Kwimba, Bahi, Mafia,
Longido, Mkinga, Uvinza, Ikungi, Iringa vijijini, Lushoto, Mbarali,
Monduli, Buhigwe, Ulanga, Masasi, Butiama na Chemba.
Amesema kuwa lengo la Serikali ni
kuhakikisha inakuwa na chuo cha Ufundi Stadi katika kila Wilaya na Mkoa
ili kuendana na kasi na maono ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga
uchumi wa viwanda.
“Hatuwezi kuzungumzia uchumi wa viwanda
bila kuwa na watu wenye ujuzi ambao ndio wataenda kufanya kazi katika
viwanda ndiyo maana Wizara yangu imeongeza kasi ya ujenzi wa vyuo vya
VETA nchini,” Alisema
Waziri Ndalichako amesema kuwa kwa sasa
Serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa vyuo vya Wilaya za Nkasi,
Ileje, Newala, Muleba, Kasulu, Itilima, Ngorongoro, Chato na Babati
vinavyotarajiwa kumalizika ndani ya mwaka 2019 na matayarisho
yanaendelea ya kuanza ujenzi wa vyuo vya Ufundi stadi katika Wilaya za
Kongwa, Ruangwa, Nyasa na Halmashauri ya mji wa Kasulu.
Kwa ngazi ya Mkoa, Prof. Ndalichako
amesema kuwa ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Geita na Rukwa unaendelea na
kwamba ujenzi wa vyuo vya Mikoa ya Simiyu, Ludewa na Kagera utaanza
punde.
Alisema kuwa serikali inaamini kuwa chuo
hicho cha Ufundi Stadi cha Wilaya ya Urambo kitakuwa chachu ya
maendeleo ya viwanda Mkoani Tabora na kuwataka wananchi wakitumie vyema
katika kujipatia ujuzi.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwandri
alisema kuwa chuo cha VETA Urambo kimekuja wakati mwafaka ambapo
changamoto ya ukosefu wa ujuzi ni kubwa hali inayosababisha vijana
kukosa ajira kwenye miradi mbalimbali mkoani hapo.
Aliwasisitiza wananchi wa Urambo kutumia
vyema chuo hicho kupata ujuzi wa aina mbalimbali kwa kuzingatia mahitaji
halisi ya soko la ajira ili waweze kujiajiri.
“Tufike mahali vijana wetu wa mkoa wa Tabora wakiulizwa unataka kuwa nani waseme wanataka kuwa waajiri wa watu wengine”Alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Elimu na Mafunzo ya
Ufundi Stadi Peter Maduki alisema kuwa VETA imedhamiria kuongeza
udahili wa mafunzo ya Ufundi stadi nchi nzima, kuboresha ufundishaji kwa
kuongeza vifaa na walimu pamoja na kuboresha miundombinu.
Alisema kuwa VETA imejipanga kukuza
uzalishaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwa kufanya
ubunifu utakaowezesha kuanzishwa kwa viwanda pamoja na kurahisisha
uchakataji wa mazao mbalimbali.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa VETA Dkt.
Pancras Bujulu alisema kuwa chuo cha Urambo kilitokana na kukarabatiwa
kwa majengo yaliyotumiwa na mkandarasi aliyejenga barabara ya Ndono hadi
Urambo na kisha kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo na
baadae Halmashauri hiyo kuyatoa yatumike kunzisha chuo hicho kutokana na
uhitaji mkubwa wa Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya hiyo.
Alisema jumla ya kiasi cha Sh. milioni
218 kimetumika kwa ajili ya ukarabati wa chuo hicho chenye majengo 15
yatakayotumika kwa ajili ya madarasa, karakana, ofisi, mabweni na nyumba
za walimu.
Dkt Bujulu alizitaja fani zitakazotolewa
katika chuo hicho kwa kuanzia kuwa ni Umeme wa Majumbani, Ushonaji,
Ujenzi, na Uhazili na matumizi ya Kompyuta na kina uwezo wa kudahili
wanafunzi 160 kwa mafunzo ya muda mrefu na wanafunzi zaidi ya wanafunzi
500 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka.
Aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Urambo
kuwaongezea eneo zaidi linalopakana na chuo hicho kwa ajili ya kuongeza
madarasa, karakana na mabweni ili kuongeza udahili wa wanafunzi kwa
kuongeza fani mbalimbali kama vile fani za kilimo na ufugaji, uungaji na
uchomeleaji vyuma, ufundi mekanika, ufundi bomba, n.k. kwa kadri ya
mahitaji ya soko.
Naye Mbunge wa Urambo Mashariki Magreth
Sitta aliipongeza VETA kwa kufanikisha ukarabati wa chuo hicho na
kuwataka wazazi kuwapeleka watoto katika chuo hicho wajipatie ujuzi.
Ili kuleta hamasa kwa wazazi kuleta
watoto wao katika chuo hicho, Mbunge huyo aliahidi kuwalipia ada ya
kiasi cha Sh. 60,000 kwa kila mwanafunzi kwa wanafunzi 62 kutoka katika
viijiji mbalimbali Wilayani hapo.
0 comments:
Post a Comment