Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 16 Mei 2019 wakati wa mkutano wa kumi na tano wa Bunge la Bajeti Jijini Dodoma.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo, Dodoma
Serikali
iko katika mchakato wa kufanya ukaguzi na tathmini ya kina ya miradi yote ya
umwagiliaji nchini ili kufanya uhakiki wa eneo la umwagiliaji kwa lengo la kubaini
ubora wa miradi, thamani ya fedha, gharama za mradi na mahitaji halisi ya sasa
ya kuboresha, kuendeleza na kuongeza miradi mipya ya umwagiliaji.
Aidha,
baada ya tathmini hiyo Serikali itaendelea kutafuta fedha ndani na nje ya nchi
ili kuhakikisha mabwawa na skimu za umwagiliaji nchini ikiwemo mradi wa
umwagiliaji katika bonde la Mkomazi zinaendelezwa na kuwanufaisha wananchi wa
Mombo na taifa kwa ujumla.
Naibu
Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) ameyasema hayo Bungeni Jijini Dodoma leo
tarehe 16 Mei 2019 wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini
Mhe Timotheo Mnzava aliyetaka kufahamu mpango wa Serikali katika utekelezaji wa
mradi wa Umwagiliaji katika Bonde la mto Mkomazi.
Alisema
kuwa katika miaka ya 1980 Serikali kupitia washirika wa maendeleo, Wakala wa
Ushirikiano wa Kitalaam wa kimataifa wa Serikali ya Ujerumani (Germany Agency for Technical Cooperation
Ltd) ulifanya upembuzi yakinifu (Feasibility studies) kwa ajili ya
kuendeleza kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mkomazi katika tarafa ya
Mombo, Halmashauri ya Korogwe. Hata hivyo taarifa za upembuzi yakinifu na
usanifu zilibaini kuwa ujenzi wa bwawa hilo ungesababisha kuongezeka kwa maji
katika ziwa Manga na kupelekea kuzama kwa Kijiji cha Manga Mikocheni pamoja na
mashamba ya wakulima.
Mhe
Mgumba alisema kuwa kutokana na changamoto
hiyo katika mwaka 2014/2015, wataalam wa ofisi ya kanda ya umwagiliaji ya
Kilimanjaro walifanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu uliofanywa katika
eneo hilo kwa lengo kuepusha uwezekano wa kufurika kwa Ziwa Manga, kuzama kwa
Kijiji cha Manga Mikocheni na Mashamba ya wakulima kutokana na ujenzi wa bwawa.
Mapitio hayo yalibaini uwezekano wa ujenzi wa bwawa na mradi wa umwagiliaji katika
eneo hilo bila kuathiri wakazi wa eneo hilo. Mapitio ya usanifu huo yalibaini
kuwa ujenzi wa bwawa pekee utagharimu Shilingi
1,543,736,877.
Aidha, akijibu swali la
Mbunge wa Kondoa Mjini Mhe Edwin Mgate Dannda aliyetaka kufahamu ni lini andiko
la mradi wa Kilimo cha Umwagiliaji katika Kijiji cha Mongoroma, Kata ya Serya wenye
eneo la ekari 3000 utaanza utekelezaji wake, Mhe Mgumba alisema kuwa katika bajeti ya mwaka 2010/2011 Serikali kupitia Idara
ya Umwagiliaji ilituma Shilingi milioni
300 kwa ajili kuendeleza miradi ya umwagiliaji ya Kisese, Kidoka na Mongoroma
Serya katika Halmashauri ya Wilaya ya
Kondoa wakati huo.
Alisema Kati
ya fedha hizo Shilingi 143,265,000 zilitumika kwa ajili ya kufanya upembuzi
yakinifu na usanifu katika mradi wa Mongoroma Serya uliopo katika Kata ya Serya.
Kazi zilizofanyika ni pamoja na upimaji wa sura ya ardhi (Topographical Survey),
usanifu wa kina (detail design), matayarisho ya gharama za ujenzi, tathmini ya rasilimali
maji (Hydrological survey), tathmini ya awali ya mazingira, utafiti
wa udongo (Soil analysis) na masuala ya jamii.
Aliongeza
kuwa Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Mongoroma Serya ulibaini
kuwa bwawa hilo lingegharimu Shilingi bilioni 4 kwa wakati huo. Aidha, bwawa
hilo lingekuwa na uwezo wa kumwagilia zaidi ya hekta 3,000 na kunufaisha zaidi
ya wakulima 12,000 kwa ajiili ya kilimo cha
umwagiliaji, matumizi ya binadamu, unyweshaji wa mifugo na wanyama pori pamoja
na ufugaji wa samaki katika vijiji vya
Mongoroma, Serya na Munguri.
Mgumba
alisema Serikali iko katika mchakato
wa kufanya tathmini ya kina kwa miradi yote ya umwagiliaji nchini ili kubaini
thamani ya fedha, ubora wa miradi na mahitaji halisi ya uboreshwaji,
uendelezwaji na kuchagua miradi michache kwa utekelezaji wa ujenzi kwa miradi
yenye TIJA, matokeo na manufaa makubwa kwa wakulima na Taifa kwa ujumla. Aidha,
baada ya tathmini hiyo na kutegemea upatikanaji wa fedha serikali itahakikisha
bwawa hilo na skimu zingine zitajengwa.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment