METDO Tanzania

METDO Tanzania

Thursday, June 14, 2018

BITEKO AELEKEZA TUME YA MADINI KUPELEKA TIMU YA WAKAGUZI WA MADINI WILAYANI ULANGA

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi kijijini Ipanko Wilaya ya Ulanga wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro ya kukagua shughuli za uwekezaji wa migodi.
Baadhi ya wananchi kijijini Ipanko wakimsikiliza kwa makini Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko alipokuwa katika ziara ya kikazi katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kukagua shughuli za utendaji wa wawekezaji wa migodi .
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi kijijini Ipanko Wilaya ya Ulanga wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro ya kukagua shughuli za uwekezaji wa migodi.
Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akizungumza na wananchi kijijini Ipanko Wilaya ya Ulanga wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili mkoani Morogoro ya kukagua shughuli za uwekezaji wa migodi.

Na Fredy Mgunda, Morogoro

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amemuelekeza Katibu Mtendaji wa Tume ya madini Profesa Shukurani Manya kupeleka haraka timu ya wakaguzi wa migodi Wilayani Ulanga kwa ajili ya ukaguzi wa migodi na yeyote atakayebainika kukiuka sheria mgodi wake utafungwa .

Mhe Biteko metoa agizo hilo akiwa Kijini Ipanko katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Morogoro na kubaini kasoro zisizovumilika kwenye uchimbaji wa madini wilayani humo.

Akizungumza na baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara kijijini hapo Mhe Biteko alisema kuwa taarifa kutoka Wilayani Ulanga zinaonyesha kuwa wananchi na wafanyakazi wanaeleza kuwa madini yanapatikana mara kwa mara lakini hutoroshwa kuelekea Arusha na Dar es salaam.

"Na hapa nawahakikishia kuwa taarifa za ofisi ya madini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonyesha mirabaha na tozo mbalimbali zilizolipwa na wenye leseni hazizidi milioni 25 wakati wafanyabiashara wa madini kwenye mji wa Mahenge wamelipa tozo na kodi mbalimbali zisizozidi milioni 16" Alikaririwa Mhe Biteko

Mhe Biteko alizitaja kasoro alizozibaini katika ziara yake hiyo kuwa ni pamoja na kutowekwa bayana taarifa za Uzalishaji wa madini pamoja na mauzo yake, Uchimbaji usiofuata taratibu na unyanyaswaji wa wananchi kwenye maeneo ya machimbo hayo.

“Wawekezaji wanapaswa kutambua kuwa wanapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi katika uwekezaji wao ikiwa in pamoja na kuwa na mahusiano mazuri na jamii inayowazunguka” Alisisitiza Biteko

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko amesema kuwa serikali inatambua kuwa kuna wawekezaji wasiokuwa waaminifu ambao kwa makusudi kabisa wanathubutu kuidanganya serikaki.

“Jamani wana Ipanko nchi hii tumeibiwa sana sasa ifike mwisho tusema hapana haiwezekani tena kwenye serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli tuendelee kuibiwa madini yetu na kuwanufaisha watanzania ambao wapo nje ya nchi yetu, Rais kashasema na sisi wasaidizi wake tunaungana naye kwamba iwe mwisho kuchezewa kwa rasilimali zetu”

“Chonde chonde nyie viongozi wetu wa ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya na mkoa tunaomba msituangushe mnapaswa kuwaelekeza wawekezaji hawa kufuata ipasavyo taratibu na sheria za nchi” alisema Biteko

Biteko alieleza kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli inapenda sana kuwa na wawekezaji wengi wenye tija ambao sio wababaisha na ambao wamekuja nchini kuiba rasilimali za watanzania.

Aidha, Biteko alisema kuwa haiwekani muwekezaji akawekeza Bilioni 42 halafu akachangia madawati na mifuko ya saruji katika jamii kama ndio mchango wake, haiwezekani wanapaswa kuchangia kulingana na kiasi ambacho wamewekaza kwa faida na manufaa ya wananchi.

“Mimi binafsi hainiingi akilini kuona muwekezaji amewekeza pesa nyingi kama hizo halafu kwenye shughuli za kimendeleo amechangia kiasi kidogo namna hiyo kwangu nasema haiwezekani na nchi hii kwa sasa sio ya kuchezewa tena” alisema Biteko

Lakini pia Naibu waziri huyo alimpongeza Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mhe Goodluck Mlinga kwa kuwapigania wananchi wake kwa kuzifikisha kero mahali husika na kutafutiwa ufumbuzi.

Nao baadhi ya wananchi akiwemo Pangarasi Kanyali, Cyprian Kanyali, Micky Sengo, Doedatus Moholeli, Hilda Linoma na Fredrick Kazimoto  walimpongeza Naibu Waziri wa Madini Mhe Biteko kwa kufika kijiji hapo na kusiliza kero zao kwani wana amini zitatafutiwa ufumbuzi kwa kufuata sheria na katiba ya nchi.

“Toka sisi tuzaliwe hatujawahi kutembelewa na waziri na kusikiliza kero zetu kama ambavyo wewe umefika kijijini kwetu leo hii tunajisikia wenye amani na furaha kwa kuwa tunajua kero zetu tunazifikisha moja kwa moja kwa kwa Rais wetu kupitia wewe waziri” Walisema wananchi hao

Awali Mbunge wa Jimbo la Ulanga Goodluck Mlinga alisema kuwa lengo la waziri kufika katika kijiji hapo ni kujionea kero wanazokumbana nazo wananchi kupitia wawekezaji wa sekta ya madini na kuzitafutia ufumbuzi.

“Huku ni mbali sana Mheshimiwa Naibu Waziri lakini kuna madini mengi ambayo ndio utajiri wa nchi hii hivyo tunapaswa kuwa makini na hawa wawekezaji maana wamekuwa wakiibia sana serikali yetu” Alisema Mlinga

MWISHO.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com