METDO Tanzania

METDO Tanzania

Tuesday, April 10, 2018

UJENZI WA UKUTA MERERANI WAOKOA MAMILIONI


*Mapato yapanda kutoka sh. milioni 147 hadi sh. milioni 714

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta kuzunguka mgodi wa Mererani kutasaidia kuongeza mapato ya Serikali ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya wizi na utoroshaji wa madini ya Tanzanite.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Aprili 10, 2018) Bungeni mjini Dodoma kwenye mkutano wa 11 wa Bunge, wakati akihitimisha mjadala wa mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019.

Waziri Mkuu amesema kukamilika kwa ujenzi wa ukuta huo uliozinduliwa Aprili 6, mwaka huu Rais Dkt. John Pombe Magufuli, kutasaidia pia kudhibiti ulanguzi na biashara ya magendo pamoja na kuimarisha usalama kwenye mgodi, kwa wafanyakazi na wafanyabiashara wa Tanzanite.

“Kukamilika kwa ujenzi huo pia kutasaidia kuongeza mapato ambapo katika kipindi cha Januari hadi Machi 2018, Serikali imekusanya takriban shilingi milioni 714 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi milioni 147.1 kwa mwaka mzima wa 2017,” alisema.

Waziri Mkuu alisema kabla ya ujenzi huo, inakadiriwa kuwa asilimia 40 ya madini ya Tanzanite yaliyokuwa yanazalishwa kila mwaka, yalitoroshwa kwa njia za panya na Serikali yetu haikuambulia chochote. “Hii ni kutokana na kukosekana udhibiti wa kutosha wa madini ya tanzanite kuanzia kwenye uzalishaji hadi kwa wauzaji,” alisema.

Alisema mbali na kuwepo kwa eneo la wachimbaji ndani ya ukuta wa Mererani, pia kutajengwa maduka ya Tanzanite na viwanda vya kuongeza thamani, hususan vya ukataji, uchongaji na ung’arishaji. Vilevile, kutakuwa na maeneo ya burudani ambayo yatastawisha zaidi biashara ya Tanzanitena kuwavuta watalii wengi kwenda kutembelea eneo hilo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) itakayokuwa na urefu wa km. 1,219 utarahisisha usafiri wa mizigo na abiria na kuongeza itaongeza biashara hapa nchini pamoja na nchi za jirani.

Waziri Mkuu alisema mradi huo utakapokamilika, unatarajiwa kusafirisha tani milioni 17 kwa mwaka, ikilinganishwa na tani milioni tano za sasa na kwamba utaongeza mapato kwa Serikali ikiwa ni pamoja na kutunza barabara ambazo zimekuwa zikiharibika mapema kutokana na kusafirisha mizigo mizito.

“Reli hii ya kisasa itakuwa na uwezo wa kubeba mzigo wa takriban tani 10,000 kwa mara moja, ambayo ni sawa na malori (semi trailers) 500 yenye uwezo wa kubeba tani 20 kila moja. Hii, itasaidia sio tu kutunza barabara zetu bali pia kupunguza gharama za kukarabati barabara hizo mara kwa mara,” alisisitiza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMANNE, APRILI 10, 2018
Share:

0 comments:

Post a Comment

Copyright © WAZO HURU | Powered by Blogger Design by ronangelo | Blogger Theme by NewBloggerThemes.com