Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
WAZIRI
wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Selemani
Jafo amewasimamisha kazi Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya ya Kigoma Ujiji
na Pangani Tanga kutokana na Ofisi zao kupata hati chafu katika Ripoti ya
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo Jumanne (Machi 27, 2018), Waziri Jafo alisema Ofisi
yake imetekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais Dkt. John Pombe kuhusiana na
ripoti ya CAG kuwataja Watendaji hao kuzembea na kusababisha taasisi zao kupata
hati chafu.
Aliwataja Wakurugenzi
waliosimamishwa kazi na kupisha uchunguzi kuwa ni Bi. Hanji Godigodi, Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani na Bw. Sabas Damian Chambasi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Pangani.
“Namwagiza Katibu Mkuu
Ofisi ya Rais TAMISEMI aunde timu ya Wataalamu kuchunguza utendaji kazi wa
Wakurugenzi hao na kunipatia taarifa ndani ya wiki tatu kuanzia leo” alisema
Waziri Jafo.
Kuhusu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji mkoani Kigoma, Bw. Judethadeus Mboya
ambaye kustaafu utumishi, Waziri Jafo alisema uchunguzi dhidi yake utaendelea
kufanyika ili kubainisha kuhusika kwake katika kuisababishia halmashauri hiyo
kupata hati chafu.
Akifafanua zaidi Waziri
Jafo alisema katika taarifa hiyo ya CAG ya mwaka 2016/17, ripoti hiyo
ilibainisha kuwa katika ngazi za Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuliwepo na jumla
ya vitabu 379 vya makusanyo ya mapato ambavyo havikuwasilishwa kwa CAG kwa ajili
ya kufanyika ukaguzi wa mahesabu yake.
Aliongeza kuwa kutokana
na taarifa hiyo, Ofisi yake itawasiliana na Wakurugenzi wote kuhakikisha kuwa
inawasilisha vitabu hivyo vyenye taarifa na nyaraka za ukaguzi katika ofisi ya
CAG haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa Jafo
alisema kwa sasa Serikali imepata mafanikio makubwa sana katika suala zima la
udhibiti wa matumizi ya fedha za Serikali katika mamlaka za Serikali za Mitaa
ikilinganisha na miaka ya nyuma ambao hali ya matumizi haikuwa nzuri.
Waziri Jafo alizipongeza
Halmashauri 166 zilizopata hati safi na kuendelea kufanya vizuri katika
kusimamia taratibu za matumizi ya fedha za umma pamoja na kuzitaka halmashauri
16 zilizopata hati isiyoridhisha kufanya maboresho katika utendaji kazi ili
kupata hati safi.
“Kwa upande wa
Halmashauri zilizopata hati chafu naziagiza zibadilishe mienendo ya utendaji
kazi katika halmashauri zao sambamba na kuyaagiza Mabaraza ya Madiwani
kusimamia vyema Halmashauri hizi katika mipango ya matumizi ya fedha za
Serikali” alisema Jafo.
MWISHO
0 comments:
Post a Comment