Wahitimu wa darasa la Saba katika shule
ya Msingi Nalopa wakitumbuiza wageni mbalimbali wakati wa sherehe ya
Mahafali iliyofanyika jana katika viwanja vya shule hiyo iliyopo jijini
hapa. (Picha na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Wazazi
na Walezi wa wanafunzi wa shule ya Msingi Nalopa wakimsikiliza Kamanda
wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna Charles Mkumbo ambaye alikuwa
mgeni rasmi kwenye sherehe ya Mahafali ya kuhitimu darasa la Saba (Picha
na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha)
Mgeni
rasmi wa sherehe ya Mahafali ya darasa la Saba katika shule ya Msingi
Nalopa Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles
Mkumbo akimkabidhi cheti mmoja wa wahitimu (Picha na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha)
Kamanda
wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna (DCP) Charles Mkumbo
akiwahutubia wageni waalikwa katika sherehe za Mahafali ya wanafunzi wa
darasa la Saba wa shule ya Msingi Nalopa (Picha na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha)
……………………………………………………………..
Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Wito umetolewa kwa wazazi, na kuelezwa kwamba mbali na kujitahidi kuwasomesha watoto wao katika
shule mbalimbali kwa lengo la kuwapatia elimu bora wametakiwa pia
kuzingatia kuwapa makuzi mema ili uhalisia wao kimuonekano uendane na
elimu wanayoipata.
Hayo
yameelezwa jana na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha Naibu Kamishna
(DCP) Charles Omari Mkumbo wakati wa sherehe ya mahafali ya wahitimu wa
darasa la saba katika shule ya Msingi Nalopa iliyopo jijini Arusha.
Kamanda
Mkumbo ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika mahafali hayo alisema kwamba,
wanafunzi hao kwa sasa wanakwenda katika hatua nyingine ya kimasomo
lakini pia umri wao unaongezeka na kukumbana na changamoto mbalimbali,
hivyo wazazi wanatakiwa waendelee kuwakuza kimaadili ili elimu yao iwe
na manufaa kwao na kwa jamii.
Alisema
elimu wanayoipata ikiendana na maadili itawasaidia kuepuka kujiingiza
katika vitendo vya uhalifu kama vile matumizi ya dawa za kulevya na
uhalifu mwingine wowote na hatimaye kuonekana kuwa wa thamani machoni
mwa watu.
Kamanda
Mkumbo aliwataka wanafunzi hao kuongeza bidii katika masomo yao hasa ya
Sayansi ili idadi ya wataalamu wengi katika kada mbalimbali iongezeke
hasa katika huu ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia ambao ushindani wa
soko la ajira umekuwa mkubwa.
Akimkaribisha
mgeni rasmi kuwatunuku vyetu wahitimu hao ambao walifanya vizuri
kimasomo, kinidhamu, uongozi, kimichezo na kujituma, Mlezi wa shule hiyo
Balozi Mstaafu Bw. Daniel Ole Njoolay alitumia nafasi hiyo kumpongeza
Kamanda huyo kwa kuzidi kuimarisha hali ya usalama katika mkoa wa Arusha pamoja na changamoto mbalimbali zilizopo.
Awali
akizungumza katika Mahafali hayo Meneja wa shule hiyo yenye wanafunzi
461 Bw. Edward Njoolay alisema kwamba, awali akisoma wasifu wa shule
hiyo alisema kwamba mwaka 1999 ilikuwa kama “Day Care” lakini ushawishi
wa wazazi uliwawezesha kufanikiwa kufikia hatua kubwa kimiundo mbinu na
kitaaluma.
Shule
hiyo imefanikiwa kutoa wahitimu wa darasa la saba mara nane ukiondoa
wahitimu wa jana na wote walifanikiwa kufaulu na kuendelea na masomo ya
Sekondari ambapo mwaka 2016 ilishika nafasi ya saba katika shule bora za
Halmashauri ya jiji la Arusha zilizofanya mtihani wa darasa la saba.
0 comments:
Post a Comment