WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania wote wahakikishe wanaboresha
mshikamano wao pamoja na kuimarisha uzalendo kwa Taifa lao.
Ametoa kauli hiyo Jumapili, Agosti 20, 2017 wakati akizungumza na wanafunzi wa Kitanzania wanaosomea udaktari nchini Cuba.
Waziri
Mkuu yuko nchini Cuba kwa ajili ya ziara ya kikazi yenye lengo la
kudumisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili. Alisema uzalendo kwa
Taifa ni jambo muhimu.
“Uzalendo
ni muhimu sana kwa sababu tumekosa fursa nyingi za kimaendeleo kutokana
na baadhi ya wananchi kutokuwa wazalendo kwa Taifa lao.”
Kutokana
na hali hiyo Serikali inawasisitiza Wananchi kuwa wazalendo na
washirikiane kuhakikisha fursa za kimaendeleo zilizoko nchini
zinaendelezwa.
Alisema
Serikali inatekeleza miradi mingi kwa lengo la kukuza uchumi kutoka wa
chini kwenda wa kati, ni vema wananchi wakashirikiana nayo ili
kufanikisha adhma hiyo.
Pia
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wanafunzi hao kuzingatia
sheria za nchini waliyoko pamoja na kukumbuka kurudi nyumbani mara
wamalizapo masomo yao.
Alisema
Serikali inatambua uwepo wao wa kimasomo nchini Cuba na kwamba
inatarajia kupata mchango mkubwa kutoka kwao punde wamalizapo masomo
yao.
“Nawaomba
msome kwa bidii na mfaulu mitihani yenu. Elimu yenu iwasaidie katika
ajira na muweze kurejesha mikopo mliyopewa na Serikali ili iwanufaishe
wengine.”
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka Mabalozi wote wanaoiwakilisha
Tanzania katika mataifa mbalimbali kuhakikisha wanatangaza vivutio vya
utalii.
Alisema
Tanzania imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii, hivyo ni vema
Mabalozi wakavitangaza jambo ambalo litasaidia kuongeza idadi ya watalii
wanaokuja nchini.
Miongoni
mwa vivutio vya utalii vilivyoko nchini ni pamoja na mlima Kilimanjaro,
visiwa vya Zanzibar, mbuga mbalimbali zenye wanyama wa aina tofauti
tofauti.
Awali
Mwenyekiti wa wanafunzi hao, Bw. Goodchance Tarimo alimuhakikishia
Waziri Mkuu kwamba watarejea nyumbani mara baada ya kumaliza masomo yao
nchini humo.
Alisema
wao wanaimani kubwa na Serikali na wanaunga mkono jitihada zinazofanywa
na viongozi wa Taifa kwa lengo la kuboresha maendeleo pamoja na kukuza
uchumi.
“Tunapongeza
jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kujenga uchumi wa
viwanda, mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi na ujenzi wa miundombinu ya
kisasa.”
0 comments:
Post a Comment