Jengo la amani na usalama lililopo makao makuu ya Umoja wa Afrika (AU) Mjini Addis Ababa nchini Ethiopia jana tarehe 29 Januari, 2017 limetangazwa rasmi kuwa litaitwa Mwalimu Julius Nyerere.
Jengo
hilo limepewa jina hilo rasmi katika hafla ya chakula cha mchana
iliyofanyika leo na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Marais mbalimbali wa
nchi wanachama wa Umoja wa Afrika, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe.
Antonio Guterres, Mawaziri na Mabalozi mbalimbali wanaohudhuria Mkutano
wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaoendelea Mjini
hapa.
Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Rais Magufuli aliwashukuru
viongozi wote wa Umoja wa Afrika kwa kuamua jengo hilo liitwe jina la
Mwalimu Julius Nyerere ikiwa ni kutambua mchango wake katika kupigania
amani na usalama na amebainisha kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa Mwafrika
halisi na kiongozi mahiri na shupavu.
“Na
kwa hakika naweza kusema kuwa alikuwa mmoja wa viongozi bora kabisa
ambaye amewahi kutokea katika Bara letu, katika maisha yake yote Mwalimu
Nyerere alipambana ili kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Afrika,
alikuwa mmoja wa waanzilishi wa umoja huu, sisi Watanzania kwa hakika
tunajivunia sana Mwalimu Nyerere kuwa Baba wa Taifa” alisema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Dkt. Magufuli aliongeza
kuwa Mwalimu Nyerere alitoa mchango mkubwa katika kupambana na ubaguzi
na unyonyaji wa kila aina, alisaidia ukombozi wa nchi nyingi za Afrika,
na hata alipong’atuka katika hatamu za uongozi wa Taifa la Tanzania
aliendelea kutoa mchango wake kupigania amani katika nchi za Afrika.
“Wito
wangu kwenu, waheshimiwa viongozi ni kwamba, sambamba na kumuenzi
Mwalimu Nyerere kwa jengo hili, itakuwa ni jambo jema zaidi kama
tutajitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kuishi maisha ya viongozi
wengine hodari wa Bara hili wakiwemo Hayati Kwame Nkhrumah, Ahmed Ben
Bella, Sekou Toure, Gamal Abdel Nasser na bila kusahau shujaa wetu
mwingine Hayati Nelson Mandela” alisisitiza Rais Magufuli.
Mkutano wa 28 wa wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika unaendelea leo tarehe 30 Januari, 2017 hapa Addis Ababa.
0 comments:
Post a Comment