Wednesday, July 18, 2018

Biteko aonya mgodi wa Ngaka mkoani Ruvuma kuacha kukwepa kodi

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Biteko

Na George Binagi, Ruvuma

Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameutaka uongozi wa kampuni ya TANCOAL inayochimba madini ya makaa ya mawe katika machimbo ya Ngaka yaliyopo Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma kufanya kazi kwa kufuata sheria na kuacha mara moja ujanja ujanja wa kukwepa kodi.

Aidha Mhe Biteko ametoa muda wa mwezi mmoja kwa kampuni hiyo kuwa imelipa serikalini malimbikizo yote ya mrabaha ambayo yanafikia hadi bilioni mbili kabla haijaandikiwa Samansi ya makosa inayoweza kusababisha kunyang’anywa leseni ya uchimbaji.

Mhe Biteko aliyasema hayo jana Julai 17, 2018 alipofanya ziara katika mgodi huo na kukuta uongozi wa kampuni ya TANCOAL unalipa mrabaha serikalini kwa bei ya kununulia madini mgodini badala ya bei ya mwisho ya kuuzia madini baada ya kusafirishwa.

Alisema kifungu cha 87 cha sheria ya madini, kifungu kidogo cha sita kinaeleza wazi kwamba kodi ya madini itatathiminiwa kwa bei ya mwisho ya kuuzia huku kifungu cha 18 kikitoa mamlaka kwa mtu yeyote anayesafirisha madini kuwa na leseni ya kuchimba madini ama leseni ya Wakala lakini kampuni ya TANCOAL inatoa leseni yake kwa wateja ili kusafirishia madini hayo mwanya ambao unatumika kukwepa kodi.

Mhe Biteko alisema kitendo cha wanunuaji wa madini ya makaa ya mawe kutumia leseni ya TANCOAL kusafirishia madini hayo ni kinyume cha sheria ambapo wao wanakwenda kuyauza kwa bei ya juu mara tatu zaidi huku TANCOAL ikilipwa mrabaha wa dola 44 kwa tani moja.

Awali Mkuu wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina Mndeme alisema watanzania wanapaswa kuwa wazalendo na kumuunga mkono Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika kusimamia rasilimali za Taifa ikiwemo madini huku akitoa rai kwa taasisi ya NDC (National Development Corporation) kuweka wawakilishi wake katika eneo la mgodi wa Ngaka pamoja na eneo la mizani ili kufuatilia taarifa za uuzaji wa madini ya makaa ya mawe.

Kaimu Meneja wa kampuni ya TANCOAL, Edward Mwanga alisema wateja wao ikiwemo kampuni ya Lake Ciment, Dangote Ciment pamoja na Tanga Ciment hawana leseni ya kusafirishia madini ndiyo maana kampuni ya TANCOLA hutoa leseni yake kwa kampuni hizo.
Mkuu wa Mkoa Ruvuma Mhe Christina Mndeme akizungumza kwenye kikao baina ya Naibu Waziri na uongozi wa kampuni ya TANCOAL.
Kaimu Meneja wa kampuni ya TANCOAL, Edward Mwanga akizungumza kwenye kikao hicho
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akikagua eneo la Bandari Kavu lililopo Kijiji cha Amani Makolo wilayani Mbinga
Naibu Waziri wa Madini Mhe.Doto Biteko akikagua eneo la machimbo ya makaa ya mawe Ngaka wilayani Mbinga
Machimbo ya Ngaka yanapochimbwa madini ya Makaa ya Mawe ambayo hutumika kwa ajili ya uzalishaji wa umeme wa viwandani

No comments:

Post a Comment