Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt.
Khalfan Haule akiwa amelala katika kitanda maalum kwaajili ya kujitolea
damu kusaidia ili kuunga mkono juhudi za mkoa wa Rukwa kusaidia majeruhi
wa ajali ya Morogoro iliyoua zaidi ya watu 90.
Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt.
Khalfan Haule (kushoto) akiendelea kuwahamasisha watumishi wa Ofisi ya
Mkuu wa mkoa wa Rukwa kujitolea damu ili kuunga mkono juhudi za mkoa
pamoja na kufuata maelekezo ya mkuu wa mkoa huo katika kuwasaidia
majeruhi waliungua kutokana na kulipukwa kwa lori katika eneo la msamvu
mkoani Morogoro na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 90.
Mmoja wa Watumishi wa Ofisi ya
mkuu wa mkoa wa Rukwa Joyce Mwanandenje akiendelea kujitolea damu kuunga
mkono juhudi za mkoa kusaidia majeruhi waliopata ajali Mkoani Morgoro
kutokana na kulipuka kwa lori la mafuta wiki moja iliyopita.
************
Timu ya Afya ya mkoa wa Rukwa
inayojishughulisha na ukusanyaji wa damu kutekeleza maelekezo ya mkuu wa
mkoa huo Mh. Joachim Wangabo ijumaa hii iliweka makazi yake nje ya
Ofisi ya mkuu wa mkoa ili kukusanya damu kutoka kwa watumishi wa ofisi
hiyo pamoja na wananchi mbalimbali wanaofika hapo kupata huduma
mbalimbali.
Timu hiyo inayoongozwa na mganga
mkuu wa mkoa ilianza kutekeleza maelekezo hayo tangu tarehe 14.8.2019
kwa kupita katika maeneo mbalimbali ya mji wa Sumbawanga kukusanya damu
hiyo kwa kushirikiana na timu nyingine za Afya katika ngazi ya
halmashauri ambazo nazo zinaendelea na zoezi hilo katika halmashauri nne
za mkoa huo.
Taarifa hiyo imethibitishwa na
mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu wakati alipokuwa
akiongea na vyombo vya habari huku akiendelea kuwahamasisha watumishi wa
serikali, waumini wa madhehebu mbalimbali ya dini, viongozi wa kisiasa
pamoja na wananchi wenye mapenzi mema kujitolea kutoa damu ili kuweza
kuwasaidia majeruhi walioungua kutokana na kulipuka kwa lori la Mafuta
katika eneo la Msamvu mkoani Morogoro Wiki moja iliyopita.
“Sisi kama wataalamu tumejipanga
baada ya mheshimiwa mkuu wa mkoa kutoa haya maelekezo, kazi hii
inafanyika katika halmashauri zote nne za mkoa wa Rukwa na katika
halmashauri zetu kuna timu maalum ya ukusanyaji wa damu, kwahiyo toka
agizo limetolewa timu zetu katika halmashauri zinaendelea na hiyo kazi,”
Alisema.
Akimuwakilisha Mkuu wa mkoa wa
Rukwa katika zoezi hilo la kuwahamasisha watumishi wa serikali kujitolea
damu, mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule ameendelea pia
kuwahamasisha wananchi kuanzia ngazi za mitaa na vijiji waendelee
kujitolea damu kupitia timu hiyo ya mkoa pamoja na timu za halmashauri
zilizoteuliwa maalum kwaajili ya zoezi hilo lakini pia kufika katika
hospitali ya mkoa kushiriki kujitolea damu.
“Damu inahitajika tunawaomba
wananchi waendelee kujitolea kama ambavyo ratiba ilivyotangazwa, hii
timu itakuwa inapita kwenye mitaa yetu kwenye kata zetu lakini pia kwa
wale ambao watakuwa wamekosa hiyo nafasi, bado hospitali yetu ya mkoa
itaweza kuwapokea waweze kuchangia damu kwaajili ya kuwanuru wenzetu
ambao wamepata ajali kule Morogoro,” Alieleza.
Aidha, mmoja wa watumishi
waliojitolea kuchangia damu Elvira Malema alieleza kuwa mahitaji ya damu
ni makubwa na kujitolea damu hiyo huenda kukaokoa majeruhi wengine
waliobakia na kudhani kuwa kama damu ingelikuwa ya kutosha huenda vifo
hivyo visingevuka idadi iliyopo na hivyo kuwaomba wananchi ambao
hawajafanya maamuzi ya kujitolea damu washiriki kufanya hivyo.
“Zoezi hili sikwamba linachukua
muda mwingi, ni dakika tu unatolewa damu kama una uzito unaostahili, una
damu ya kutosha, nawahamasisha watu wajitokeze kuchangia kwasababu leo
unaweza ukaona ni kitu kinachotokea kwa mtu mwingine kwasababu
hakijakufika kwenye familia yako ukadharau, kwahiyo nawahamasisha watu
wajitokeze kuchangia,” Alisema.
Kwa upande wake mmoja wa madereva
wa boda boda aliyefika katika ofisi hiyo kupata huduma Ayoub Wangoma
ameishukuru serikali kwa kuwahamasisha madereva wa bodaboda kuchangia
damu kwa kutanabahisha kuwa madereva hao wanahitaji damu kutokana na
shughuli zao zinazowaweka barabarani kila kukicha na hivyo kuguswa na
kampeni hiyo na hatimae kuamua kuunga mkono juhudi za mkoa kwa kujitolea
damu.
“Sisi ka vijana tunaojishughulisha
na bodaboda imetugusa sana na kujitoa kwa moyo kwasababu jambo kama
lile waliopoteza maisha pale kuna ndugu zetu kuna wazazi wetu, kwahiyo
tunapojitolea damu leo kwao kesho kwetu, inawezekana jambo kama lile
tunaliongelea kwa udogo lakini mbeleni huko linaweza kutokea likatuhusu
sisi wenyewe bodaboda kulingana na shughuli tunazofanya,” Alisema.
Zoezi la uchangiaji wa damu
kwaajili ya kusaidia majeruhi wa ajali ya Morogoro inatarajiwa
kuamalizika tarehe 18.8.2019 na taarifa ya jumla ya zoezi hilo kutolewa
tarehe 19.8.2019 na hatimae damu hiyo kusafirishwa kwenda sehemu husika
kulingaana na malekezo ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
No comments:
Post a Comment