Monday, February 25, 2019

SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI KUTEKELEZA MRADI WA UENDELEZAJI NA UPATIKANAJI WA MBEGU ZA MAZAO JAMII YA MIKUNDE NA NAFAKA AFRIKA (AVISA)

Mgeni Rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza ushirikiano wa serikali kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo wakati akifungua mkutano wa Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (AVISA) uliofanyika katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha, leo tarehe 25 Februari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Baadhi ya washiriki wakifatilia mkutano wa Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (AVISA) uliofanyika katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha, leo tarehe 25 Februari 2019.
Mgeni Rasmi-Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akizungumza wakati akifungua mkutano wa Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (AVISA) uliofanyika katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha, leo tarehe 25 Februari 2019.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe Gabriel Daqarro akizungumza kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi kufungua mkutano wa Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (AVISA) uliofanyika katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha, leo tarehe 25 Februari 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano wa Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (AVISA) uliofanyika katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha, leo tarehe 25 Februari 2019. 

Na Mathias Canal, Wizara ya kilimo-Arusha

Serikali imeeleza kuwa imejipanga kuweka mazingira wezeshi katika kutekeleza Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (The Accelerated Varietal Improvement and Seed Delivery of Legumes and Cereals in Africa project-AVISA). utakaosimamiwa na kutekelezwa kwa ukamilifu nchini Tanzania.

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo leo tarehe 25 Februari 2019 wakati akifungua mkutano wa Mradi wa uendelezaji na upatikanaji wa mbegu za mazao jamii ya mikunde na nafaka Afrika (AVISA) uliofanyika katika ukumbi wa Mount Meru Hotel Jijini Arusha.

Katika ufunguzi huo wa mkutano wa siku tatu, Mhe Hasunga alisema kuwa ana mategemeo makubwa kuwa katika mradi huo msukumo mkubwa utawekwa katika uhaulishaji wa teknolojia kupitia uimarishaji wa mashirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili matokeo ya mradi yaweze kuonekana kwa walengwa.

Alisema, Kilimo kimeendelea kuwa uti wa mgongo wa uchumi katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania. “Kwa mfano, hapa Tanzania kilimo kinachangia asilimia 29.1 katika pato la taifa na karibia asilimia 65.5 ya nguvu kazi inategemea kilimo”

“Hata hivyo, kwa Afrika kilimo kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ukame, upungufu kwa rutuba katika udongo, kuongezeka kwa magonjwa na wadudu wa mazao vipando, miundombinu hafifu, kipato kidogo kwa wakulima, upokeaji mdogo wa teknolojia, soko lisilokuwa la uhakika na bei ndogo za mazao, kutegemea kilimo cha jembe la kutumia mkono na mifumo hafifu ya uzalishaji na usambazaji wa mbegu bora. Hivyo, hali hii inasababisha uzalishaji mdogo, ubora mdogo wa mazao na kuwafanya wakulima kubakia kuwa wadogo na kulima kwa kujikimu tu sio kibiashara” Alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema kuwa, ana matumaini makubwa kuwa Mradi huo utaimarisha mafanikio yaliyopatikana kutoka kwenye miradi ya utafiti iliyotangulia ya Mikunde (Tropical Legumes -TL), Uendelezaji wa Tija katika Mazao ya Mtama na Ulezi (Harnessing Opportunities for Productivity Enhancement for Sorghum and Millets - HOPE) na Harvest Plus ambayo ilifadhiliwa na Shirika la Bill & Melinda Gates Foundation (BMGF) kwa ajili ya kuendeleza uzalishaji wa mbegu na usambazaji wake.

Aidha, BMGF imekuwa ikifadhili miradi hiyo katika nchi saba (7) za Afrika zikiwemo Tanzania, Uganda, Ethiopia, Burkina Faso, Ghana, Mali na Nigeria katika utafiti wa  dengu, karanga, maharagwe, kunde, mtama na ulezi. Hivyo, Mradi huo wa AVISA utaendeleza na kuimarisha mashirikiano kati ya Vituo vya  Kimataifa vya Utafiti wa Kilimo (CGIAR) na Mifumo ya Kitaifa ya Utafiti wa Kilimo katika nchi za Afrika (NARS) katika kuendeleza uzalishaji na usambazaji wa mbegu za aina ya nafaka na mikunde zinazohimili maeneo ya ikologia ya ukame.

Manufaa mengine ni kuimarisha na kuongeza madini ya chuma na zinki katika mazao ya maharagwe na ulezi katika mradi wa HarvestPlus unaofadhiliwa na BMGF kupitia CIAT (Maharage) na ICRISAT (Ulezi). Hivyo, kuwekeza Miradi miwili ya TL-III na HOPE ambapo itaongeza tija kwenye mazao husika na  kujenga uwezo wa utafiti kwenye nchi zetu za Afrika.

Mkutano huo ulihudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe Gabriel Daqarro, Wawakilishi Shirika la Bill & Mellinda Gates, likiongozwa na Dkt Jeff Ehlers, Mkurugenzi Mkuu ICRISAT: Dkt Peter Carberry, Wakurugenzi wa Taasisi za Utafiti za Kanda: CIAT, ICRISAT and IITA, Wawakilishi wa Shirika la Syngenta, Wakurugenzi Wakuu, Taasisi za Utafiti wa Kilimo kutoka: Uganda, Ethiopia, Nigeria, Burkina Faso, Ghana, Mali and Tanzania, Wakurugenzi wa Wizara ya Kilimo na Wakuu wa Taasisi zake Wawakilishi wa Makampuni ya Mbegu, Wawakilishi wa Mashirika yasiyo ya Serikali pamoja na Wawakilishi wa Vyama vya Wakulima.

MWISHO

No comments:

Post a Comment