Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akiwasili Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera alipofanya ziara ya kushtukiza katika halamashauri hiyo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye halmashauri hizo.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akimsikiliza Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera Novatus Babu alipofanya ziara ya kushtukiza katika halmashauri hiyo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye halmashauri hizo.
Naibu waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline Mabula akikagua jalada la ardhi katika ofisi ya masijala ya ardhi katika Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera alipofanya ziara ya kushtukiza katika halmashauri hiyo kufuatilia maelekezo aliyoyatoa kwenye halmashauri hizo. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri Sospiter Mwishamba na kushoto ni Mpimaji Ardhi Vedastus Masige
Na Munir Shemweta, Biharamulo
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angeline
Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya wilaya ya
Biharamulo mkoani Kagera kujipanga na kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza
migogoro ya ardhi na wasipotekeleza majukumu yao vizuri atawawajibisha.
Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri ya
wilaya ya Biharamulo katika ofisi za halmashauri hiyo mkoani Kagera, Dk.
Mabula alisema pamoja na changamoto zinazoikabili sekta ya ardhi katika
halmashauri hiyo lakini watumishi wa sekta hiyo wanapaswa kujipanga na kufanya
kazi kwa ushirikiano ili kuweza kupunguza migogoro ya ardhi na wakati huo
kuwawezesha serikali kukusanya mapato kupitia sekta ya ardhi.
"Kama kazi haziendi migogoro ya ardhi haiwezi kuisha na
ninyi hapa mna viwanja vichache lakini mmeshindwa kuviingiza katika mfumo hivyo
mkimaliza kuviingiza viwanja hivyo hapo mnaweza kurekebisha takwimu"
alisema Dk Mabula.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amewataka
wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaziangalia idara za ardhi katika
halmashauri zao kwa kuwa hakuna miradi inayokamilika bila kuhusisha ardhi hivyo
sekta hiyo ni muhimu na inapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa.
Ameiagiza halmashauri ya wilaya ya Biharamulo kupitia idara ya
ardhi kuhakikisha inatoa ilani za madai kwa wadaiwa wa kodi ya ardhi mia tano
katika kilindi cha wiki moja na kueleza kuwa watakaoshindwa kulipa basi
wafikishwe katika mabaraza ya ardhi. Hata hivyo, Dk Mabula ameshangazwa
na halmashauri hiyo kushindwa kutoa hati za madai wakati ina wadaiwa wa kodi ya
ardhi wapatao 2000.
Akigeukia suala la utoaji hati za ardhi , Dk Mabula
ameshangazwa na kasi ndogo ya utoaji hati ambapo katika kipindi cha ropo ya
pili ya mwaka 2018/2019 idara hiyo imeweza kuandaa hati 31 kati ya 200 huku
baadhi ya hati zikiwa katika ofisi ya Kaimu Mkuu wa Idara ya ardhi tangu
mwezi Novemba 2018 bila kusainiwa wakati hati zinaweza kutolewa ndani ya mwezi
mmoja.
Aidha, Dk Mabula ameitaka halmashauri ya Biharamulo
kutambua mali zake na kuhakikisha maeneo yake yanakuwa na hati za ardhi
sambamba na kulipa kodi ya pango la ardhi. Kwa mujibu wa Dk Mabula maeneo
mengi ya halmashauri yanekuwa na mgogoro kutokana na kukosa hati na wakati huo
kushindwa kulipa kodi ya ardhi.
Mapema Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi ambaye ni Afisa Ardhi
Mteule katika halmashauri ya wilaya ya Biharamulo Novatus Babu alimueleza
Naibu Waziri Mabula kuwa halmashauri hiyo imepima jumla ya viwanja 3, 101
katika maeneo ya Biharamulo Mjini, Nyakanazi, Runazi,
Lusahunga na Nyakahura na jumla ya viwanja 2, 191 vimeingizwa katika mfumo huku
viwanja 200 vikiwa havijaingizwa.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkuu huyo wa Idara halmashauri ya Wilaya ya
Biharamulo katika kilindi cha robo ya pili 2018/2019 imeweza kukusanya kiasi
cha shilingi 38, 022, 624 kati ya milioni 150 ilizopangiwa katika kipindi cha
mwaka 2018/2019.
No comments:
Post a Comment