Friday, November 10, 2017

TAWLAE Kuunganisha Wakulima na Tafiti

Chama cha Wanawake  Wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Mazingira, Tanzania Association of Women Leaders in Agriculture and Environment  ( TAWLAE) leo wamefungua rasmi mkutano wa mwaka  wa 21 ambao mgeni rasmi alikuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Bi Butano Philipo kwa  niaba ya Waziri wa  Mazingira  Mhe. January Makamba, mkutano  ambao umefanyika  leo katika Viwanja vya Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Akiongea katika mkutano huo Mwenyekiti ya Chama cha Wanawake Viongozi katika kilimo na mazingira Dkt. Sofia Malote amesema, Lengo kubwa la mkutano huo ni kuunganisha wakulima na tafiti mbalimbali  zilizoandaliwa na wataalamu hao.
Maadhimisho hayo ya 21 yamebeba kaulimbiu isemayo  Uchumi wa Viwanda Tanzania Wanawake tupo tayari, hapa kazi tu.
Aidha Dkt. Sofia Malote amesema kazi ya TAWLAE ni kuwaunganisha wakulima wadogo au wakubwa na tafiti mbalimbali ambazo  zimetafitiwa hapa nchini  ili kuongeza uwekezaji na ajira kwa watanzania katika kilimo. 

Akizungumza  katika wasilisho lake Dkt. Malote amesema kilimo kilikuwa na faida ndogo kwa sababu utalaamu, teknolojia na juhudi zilikuwa bado hazijatumika vizuri kwenye kilimo hivyo ni jukumu la TAWLAE kuhakikisha kuwa wanaleta mapinduzi ya kilimo katika uchumi wa viwanda.
Ili kuingia katika uchumi wa viwanda  ni lazima uzalishaji  wa kilimo uwe na  tija, kuwepo na uboreshaji wa masoko na teknolojia ambapo wataalamu wanawake ndio wanajukumu kubwa katika kuleta mapinduzi ya kilimo alisema Dkt.Malote

Mwenyekiti wa chama cha wanawake viongozi TAUWLAE Dkt. Sofia Malote wakati akiongea na wanachama katika mkutano wa 21 uliofanyika leo katika Viwanja vya Mifugo

No comments:

Post a Comment